Bondia maarufu wa zamani wa ngumi za uzito wa juu George Foreman amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 76, kwa mujibu wa taarifa ya familia yake.

Familia yake iliandika kwenye Instagram Ijumaa usiku: “Mioyo yetu imevunjika.”Mhubiri mwenye imani kubwa, mume mwaminifu, baba mpendwa, na babu na babu mkubwa mwenye fahari.

“Aliishi maisha yaliyojaa imani isiyoyumba, unyenyekevu, na kusudi thabiti.” Taarifa hiyo iliongeza: “Mwanaharakati wa kibinadamu, mshindi wa Olimpiki, na bingwa wa dunia wa uzito wa juu mara mbili. Alikuwa mtu mwenye kuheshimika sana – mtu wa nidhamu, msimamo, na mtetezi wa urithi wake, akipambana bila kuchoka kulinda jina lake zuri kwa ajili ya familia yake.”

Akiwa maarufu kwa jina la Big George kwenye ulingo wa masumbwi, Mmarekani huyu alijenga moja ya taaluma za kipekee na za kudumu zaidi katika mchezo huo, akishinda medali ya dhahabu ya Olimpiki mwaka 1968 na kutwaa taji la dunia mara mbili kwa tofauti ya miaka 21.

Ushindi wake wa pili ulimfanya kuwa bingwa mzee zaidi katika historia akiwa na umri wa miaka 45. Foreman alipoteza taji lake la kwanza kwa Muhammad Ali katika pambano lao maarufu ‘Rumble in the Jungle mwaka 1974. Hata hivyo, rekodi yake ya masumbwi ya kulipwa ilijumuisha ushindi wa ajabu wa mapambano 76, huku 68 kati yao akiwashinda wapinzani wake kwa knock-out, karibu mara mbili ya idadi ya Ali.

Alistaafu masumbwi mwaka 1997.