Na Mwandoshio Wetu,JamhuriMedia,Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kt. Dorothy Gwajima ameitaka jamii kujadili mfumo mzuri wa kuwasaidia watoto wanaoomba mitaani ili misaada hiyo iweze kupelekea watoto hao kutimiza ndoto zao.
Gwajima ametoa wito huo alipofanya ziara ya kukusanya maoni ya wananchi katika soko Kuu la Majengo Jijini Dodoma tarehe 28 Septemba, 2022 kuhusu kutumia utaratibu wenye tija wa kuwasaidia watoto hao.
Amesema watoto wanaoomba mitaani hususani kwenye mikusanyiko kama stendi za mabasi, sokoni na barabarani wanatokana na sababu nyingi na imebainika kuwa wako watoto wengi ambao ni matokeo ya kutumikishwa yaani nyuma yao kuna watu wananufaika.
“Kati ya watoto mnaowasaidia wako waliotumwa kufanya kazi hiyo na kuwasilisha hesabu hiyo kwa watu wazima wanaowatumikishaā€¯ amesisitiza Waziri Dkt. Gwajima.
kt. Gwajima ameongeza kuwa, Serikali peke yake haitaweza kutatua tatizo hilo bila kuelimisha jamii undani wa watoto wanaoomba mitaani na tija ya misaada ambayo jamii inatoa.
Vilevile, amehimiza wananchi kushirikiana na Serikali kuweka mfumo mzuri wa kuwasaidia watoto waliothibitika kuwa na uhitaji ili wanufaike mathalani, kuwapeleka kwenye vituo rasmi vya kutunza na kuendeleza watoto, hali itakayochangia jamii kuachana na kusaidia watoto barabarani badala yake kuelekeza misaada hiyo kwenye vituo hivyo.
Aidha, mfumo huo utafanya watoto kuacha kukimbilia barabarani kwa sababu hakuna misaada tena na badala yake wenye uhitaji wataamua kuripoti kwenye vituo rasmi ambako watafanyiwa tathmini na kuwekewa mpango mzuri wa kusaidiwa na kuendelezwa.
“Mahitaji ya Mtoto ni pamoja na kulala mahala salama, Afya njema, asome shule, aepukane na ukatili wa kubakwa, madawa ya kulevya na adha zingine kama hizo hivyo, kuwasaidia wakiwa mtaani kama ombaomba huenda ukawa siyo utaratibu wenye tija kwa kesho njema ya mtoto kwani huenda wanaonufaika ni wanaomtumikisha na wanaotoa misaada nao hawafahamu ” amesema Dkt. Gwajima.
” Pia kuna kila sababu ya jamii tutafakari mfumo mzuri wa kusaidiana wakati haki nyingine za watoto pia zikizingatiwaā€¯ amesema Dkt. Gwajima.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa jiji la Dodoma walioshiriki mkutano huo wamepongeza jitihada hizo za Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum huku wakisema sasa huu ndiyo utakuwa muarobaini wa kuhakikisha changamoto za kutumikisha watoto mitaani zinaisha.
“Nakubaliana vitengenezwe vituo kama mtu anataka kusaidia aende kwenye kituo, siyo kuomba, jamii tusaidiane. Kuna watu wengine walemavu wanaweza kufanya kazi au Biashara na kupata faida kuwe na utaratibu mzuri wa kuwasaidia Hawa wapate kazi zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi” amesema mfanyabiashara Dida Zungu.
Naye Godson Rugazana mkazi wa Majengo jijini Dodoma amesema wito wa Waziri Dkt Gwajima ni mzuri hasa kwa wale kuhusu kupunguza tatizo la Ombaomba na Watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani ambao hawana mahali pa kutegemea vijengwe vituo mahali kadhaa ambapo Jamii inakuwa rahisi kuwasaidia.