Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali imezindua kampeni ya Kitaifa ya elimu ya mmonyoko wa maadili ambayo itafanyika kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Juni hadi Desemba mwaka huu huku akiwataka wazazi na walezi kufanya vikao vya mara kwa mara na watoto wao ili kuondoa changamoto ya mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Akizindua muongozo huo ambao ulienda sambamba na maadhimisho ya siku ya familia duniani Waziri wa maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalumu Dk.Doroth Gwajima amesema jamii lazima iwe na utaratibu wa kukaa na watoto kuzungumzia masuala ya maadili.

Amesema,”katika kuhakikisha tunapinga kwa nguvu mmonyoko wa maadili tunaoushuhudia sasa siku ya leo nitazindua kampeni maalumu kampeni ya kitaifa ya elimu ya mmomonyoko wa maadili ambayo itafanyika kwa kipindi cha miezi sita ambapo tutaenda kufika hadi katika ngazi ya chini,”amesema
Katika hatua nyingine Dk.Gwajima amesema vitendo ya ukatili vimeongezeka kutoka visa 11,499 mwaka 2021 hadi kufikia visa 12,123 mwaka jana.
Amesema mikoa kinara kwa vitendo vya ukatili ni Arusha, Mbeya, Kinondoni, Tanga na Mwanza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Fatma Taufiq alisema jamii ikiwa na malezi na makuzi bora masuala ya ukatili hayatakuwepo huku akisisitiza kila mtu kwa imani yake kumrudia mwenyezi mungu.
Amesema kama jamii itazingatia maadili mema familia zitakuwa na amani na tukikengeuka watakaoumia zaidi ni watoto hivyo kila familia ni budi kuwa na upendo .

“Tunamshukuru Rais Dk.Samia Kwa namna ambavyo anafanya kazi ya kupeleka maendeleo Kwa wananchi na leo tumekutana hapa Kwa ajili ya kujadili jambo la mwingi ambapo tunasisitiza wanafamilia kujenga ustawi na kuendelea kuikumbusha jamii kuwa wajibu wa kuitunza familia ni wa kila mtu.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo John Jingu alieleza kuwa maadhimisho ya siku ya familia kimataifa,inatokana na maadhimio ya kimataifa tangu 1993 likitaka mataifa yote kufanya siku ya familia kila Mei 15.
Amesema siku hii hutumika kutafakali namna ya kufanya malezi na kauli mbiu ni imarisha maadili na upendo Kwa familia imara.
Kwa upande wake Naibu Waziri WA Kilimo ambaye pia ndiye Mbunge wa Dodoma Mjini Antony Mavunde amesema familia ni taasisi muhimu kwa ajili ya ustawi wa jamii .

“Leo ni siku muhimu kuhakikisha tunaishi katika maadili kuwalea na kuwatunza watoto.Dodoma kuna wakati tulipata ya kuwa na watoto wengi wa mitaani ukiwauliza changamoto yao ni kutoluelewana na familia siku ya leo tutapata fursa ya kuelimisha jamii kuhusu suala la malezi Bora.

