Na Mwamvua Mwinyi, JanhuriMedia, Pwani
KIWANDA cha marumaru cha Goodwill pamoja na kiwanda cha kutengeneza vioo cha Sapphire -Mkiu , Mkuranga Mkoa wa Pwani ,kimetoa misaada mbalimbali kwa ajili ya waathirika wa mafuriko Rufiji .
Kati ya misaada hiyo ni pamoja na mifuko 70 ya unga wa sembe yenye kilo 50 kila mmoja ,mifuko 10 ya mchele,na mifuko kumi ya sabuni.
Akipokea misaada hiyo kutoka kwa Ofisa raslimali watu wa kiwanda cha Goodwill na Sapphire Jerry Malandu, Katibu Tawala Mkoa wa Pwani ,Rashid Mchatta aliwashukuru Goodwill na Sapphire kwa michango yao na mkoa umepokea .
“Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, nimepokea misaada hii,na tunawashukuru Goodwill na Sapphire Kwa hiki mlichochangia “
Akikabidhi misaada hiyo kwa niaba ya uongozi wa viwanda hivyo Meneja Rasilimali watu Jerry alieleza ,wameshiriki kutoa msaada kwa wananchi wa Rufiji baada ya kuguswa na changamoto za mafuriko yanayowakabili.
“Tumeleta kidogo tulichopata kulingana na biashara tunazozalisha na kuuza za uuzaji wa tiles na vioo, na kurudisha kidogo kwa Jamii, tumeleta unga wa mahindi kg70, mchele viroba 10, sukari na sabuni viroba 20” alifafanua Jerry.
Wadau mbalimbali wanasisitizwa kuendelea kujitokeza kutoa misaada kwa wahanga wa mafuriko yaliyowakumba wananchi kwenye baadhi ya maeneo, mafuriko ambayo yametokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali mkoani Pwani.