Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju ameiomba Klabu ya Mpira inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara Simba Sports Club kuungana na Serikali katika kutoa elimu kuhusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, Ukatili wa Kijinsia, kulinda na kuwalea wazee.

Mkurugenzi Mkuu wa Klabu ya Simba Babra Gonzalez akimkabidhi zawadi mmoja wa wazee anayehudumiwa katika Makazi ya Wazee Nunge Kigamboni Mkoani Dar Es Salaam.

Mpanju aliyasema hayo Agosti 02, 2022 katika Makazi ya Wazee Nunge, Kigamboni Mkoani Dar Es Salaam wakati Klabu hiyo ilipowatembelea Wazee wanaohudumiwa katika Makazi hayo.

Mpanju amesema kuwa mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ni jukumu la kila mmoja, hivyo ikiwa ni moja ya Klabu ya Mpira yenye mashabiki wengi wakiungana na Serikali kutoa elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili, Jamii itafikiwa na kunusuru Wanawake na Watoto kufanyiwa Vitendo hivyo.

“Ndugu zangu vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto vinafanywa na ndugu wa karibu na vinafanyika katika nyumba zetu, tuunganishe nguvu tupambane kutokomeza vitendo hivi” amesema Mpanju.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju akizungumza wakati wa tukio la utoaji wa msaada lililofanywa na Klabu ya Simba katika Makazi ya Wazee Nunge Kigamboni Mkoani Dar es Salaam.

Ameongeza kuwa kitendo cha klabu hiyo kushuka chini kwa wananchi ni jambo la kuigwa na wadau wengine kwani ni kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwahudumia wananchi hasa makundi yenye mahitaji.

Aidha, Mpanju ametumia hadhara hiyo kuitaka Jamii kuwatunza Wazee wao na kuhakikisha wanawapatia huduma muhimu kwani Wazee hao walitimiza majukumu yao ya kuwalea na kuwatunza wakati wa ujana wao.

“Tuzingatie Malezi bora kwa watoto na familia zetu kwani tunaona Watoto wanawatelekeza Wazee wao vijijini na wao wanaishia mijini hili sio suala jema tuwalee watoto wetu vyema na wao waje watulee tukiwa Wazee” amesisitiza Mpanju

Akitoa taarifa ya Makazi hayo Afisa Mfawidhi Jackilina Kanyamwenge amesema makazi hayo yanahudumia jumla ya wazee 21 kwa sasa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamekuwa wakitoa huduma muhimu zikiwepo za chakula na matibabu.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na mashabiki wa Klabu ya Simba mara baada ya kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wazee wa Makazi ya Wazee Nunge Kigamboni Mkoani Dar es Salaam.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Klabu ya Simba Babra Gonzalez amesema Klabu hiyo itashirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kuhakikisha elimu inaifikia jamii kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ,elimu ya Malezi kwa Mtoto na kuwatunza Wazee katika jamii.

Nao baadhi ya Wazee wanaohudumiwa katika Makazi hayo wameishukuru Klabu ya Simba kwa kuwakumbuka, kuwatembelea na kuwapa mahitaji mbalimbali yatakayowasaidia katika kupata huduma muhimu ikiwemo chakula