NA RESTITUTA FISSOO, MANYARA
Ni ukweli usiopingika kuwa ili kufikia azma ya Serikali ya kufanya kilimo kuwa biashara, kukuza kipato, matumizi ya sayansi na teknolojia vinahitajika ili kuongeza uzalishaji na tija kwa mkulima.
Hata hivyo, teknolojia mpya ya kubadilisha vinasaba vya mimea (GMOs) imeleta hofu kwa wakulima hususani mkoani Manyara kiasi cha kuibua hitaji kwa Serikali kuingilia kati.
Hali hiyo inajadiliwa kwenye Mkutano Mkuu wa 10 wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima (MVIWATA) uliofanyika mkoani Manyara mwishoni mwa mwaka jana, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwamo wakulima.
Licha ya wakulima kuwa na hofu na matumizi ya teknolojia hiyo, asasi zisizokuwa za kiserikali zinatetea haki za wakulima. Miongoni mwa asasi hizo ni PELUM Tanzania na wadau tofauti wa mazingira wanahofia matumizi ya teknolojia hiyo, kwamba yakiruhusiwa yanaweza kuleta athari na kuharibu utaratibu wa asili wa kilimo nchini.
Athari zinazotajwa ni pamoja na bei kubwa ya mbegu. Mara nyingi bei ya mbegu iliyobadilishwa vinasaba inakuwa kubwa kuliko ile ya asili, hali itakayosababisha wakulima wadogo na zaidi wenye kipato cha chini kushindwa kumudu gharama zake. Kwa hali hiyo, ni wazi kwamba matumizi ya mbegu hizo yatakuwa na tija kwa wakulima wenye kipato cha juu na kati.
Uhakika wa chakula
Teknolojia ya vinasaba vya mimea inamlazimu mkulima kununua mbegu kila msimu wa kilimo, kwa hali hiyo inaendelea kuwa ni vigumu kwa wakulima wadogo kumudu gharama hizo. Matokeo ya tafiti yaliyowasilishwa kwenye mkutano huo yanaonesha kuwa asilimia 70 ya wakulima wadogo wa Tanzania hutumia mbegu katika mfumo usio rasmi.
Wakulima hao wanazalisha zaidi ya asilimia 90 ya mahitaji ya chakula nchini, hivyo kuleta teknolojia ambayo itawalazimisha (wakulima) kununua mbegu kila mwaka.
Changamoto nyingine inayoleta hofu ni biashara, kwani yapo baadhi ya mataifa ambayo yamepiga marufuku kilimo na mazao ya viinitete, hivyo kuingia katika kilimo kunaweza kukosesha taifa baadhi ya fursa za kibiashara hasa katika nchi zilizopiga marufuku.
Athari za kimazingira
Hofu nyingine ni kuhusu uharibifu wa mazingira kutokana na kile kinachoelezwa kuwa viinitete vina uwezekano wa kuambukiza, kuchafua na kuathiri viumbehai vingine.
Taarifa zinaeleza kuwa hivi sasa mpango unaofanyika ni kutekelezwa kwa mradi wa majaribio ya teknolojia hiyo, ukihusisha mahindi ya ‘wema’ huko Makutupora mkoani Dodoma.
Katika jitihada nyingine, Serikali imetengeneza kanuni za kusimamia teknolojia hiyo ikiwa ni vipengele vinavyohimiza uwazi katika manufaa na udhibiti wa viinitete.
Moja ya kanuni hizo ni pamoja na ile isemayo, iwapo yatatokea madhara ya kiafya, kiuchumi au kimazingira, kampuni inayomiliki mbegu husika italazimika kutoa fidia kwa aliyepata madhara hayo.
Mkulima Clement Maleyeki wa Kijiji cha Dongobesh aliyeshiriki mkutano huo, amehoji uhakika wa mbegu hizo kustahimili magonjwa, wadudu na mabadiliko ya tabianchi?
Kwa sababu kampuni zinazotengeneza mbegu hizo wanadai zinastahimili magonjwa, wadudu na ukame.
Mratibu wa MVIWATA mkoani Manyara, Martin Pius, amesema mbegu hizo zinafanyiwa utafiti hivyo uwezo wake katika kustahimili mabadiliko ya tabianchi na magonjwa haujajulikana.
Amesema kutokana na hali hiyo, ipo haja kwa wakulima kubaki katika matumizi ya mbegu za asili zinazopaswa kuboreshwa zaidi ili zitosheleze mahitaji ya mkulima na kumwezesha ashiriki kilimo cha uhakika na cha biashara.
Pius amesema wakulima wanapaswa kuhamasishwa kulima mazao yanayostahimili mvua chache kwa vile maeneo mengi hususani mkoani Manyara, hayapati mvua za kutosha kila mwaka.
“Hivyo kila kaya inashauriwa itenge eneo la angalau ekari moja kulima mazao yanayostahilili mvua chache kwa ajili ya usalama wa chakula,” amesema Pius alipozungumza na JAMHURI. Mazao yenye thamani yanayopewa kipaumbele mkoani humo ni ngwara, alizeti, ufuta, karanga na mbogamboga.
Takwimu zinaonesha kuwa Mkoa wa Manyara una eneo lenye ukubwa wa hekta 30,997 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini eneo linalotumika ni hekta 11,715 sawa na asilimia 3.4 ya eneo linalofaa kwa umwagiliaji, hivyo Pius anashauri, “Serikali kwa kutumia maafisa wa ugani wafanye kazi ya kuhamasisha kilimo cha umwagiliaji kwani kuna maeneo makubwa ambayo bado hayajatumika.”
Kuhusu upatikanaji wa ruzuku ya pembejeo iliyoanza mwaka 2008, hoja za wajumbe kadhaa wa mkutano huo zinaeleza kuwapo changamoto kadhaa zikiwamo bei kubwa ya gharama na huduma hiyo kuwafikia wakulima wachache.
Pia imebainika kuwapo changamoto ya ukosefu wa elimu kuhusu matumizi ya pembejeo hasa mbolea, hali inayoibua na kuendeleza mawazo potofu kuwa mbolea ya viwandani inaharibu udongo, bei kubwa inayosababisha wakulima wadogo kutonunua mbolea na gharama zinazotozwa na maabara kwa mkulima kupima sampuli ya udongo.
Changamoto nyingine inatajwa kuwa ni bei ndogo ya mazao isiyoendana na gharama kubwa za uzalishaji wa mazao ikiwamo pembejeo kama mbolea, hivyo kuwapo hitaji la Serikali kupita wataalamu wa kilimo, kutoa elimu ya umuhimu wa matumizi ya mbolea kupitia mashamba darasa.
kwa mujibu wa Afisa Kilimo Mkoa wa Manyara, Samwel Tluway, takwimu za mkoani humo zinaonesha kuwapo wataalamu wa ugani 405 (ingawa wapo waliopunguzwa katika kampeni ya udhibiti wa vyeti bandia) ambao wanasimamiwa na halmashauri za wilaya. Idadi hiyo inatajwa kuwa ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya wakulima na mahitaji yao.
“Kutokana na kupunguzwa waliokuwa na vyeti bandia na wengine kustaafu, wamebaki wataalamu wa ugani 350. Hata hivyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza watendaji wa kata na vijiji watumike kuratibu shughuli za kilimo katika maeneo yao,” amesema Tluway.
Aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera (marehemu), aliwahi kuwaonya maafisa ugani mkoani humo kuondokana na hulka ya kukaa ofisini, badala yake wakayatembelee mashamba, kukutana na kuwasaidia wakulima namna bora ya kilimo cha kisasa.