Na Christopher Lilai, Lindi

Lindi ni miongoni mwa mikoa ambayo bomba kubwa la gesi asilia itokayo mkoani Mtwara limepita kuelekea Kinyerezi jijini Dar es Salaam. 

Kwa kiasi kikubwa gesi hiyo inatumika kufua umeme wa viwandani na majumbani kwa kiasi kidogo.

Hata hivyo, licha ya kupitiwa na rasilimali hiyo kubwa, wananchi wa mkoani Lindi bado hawajanufaika moja kwa moja na uwepo wa gesi hiyo asilia.

Mara baada ya kutangazwa kwa mradi huo wa bomba la gesi, wakazi wengi wa mikoa ya Lindi na Mtwara wakaamini kuwa sasa umefika wakati wa wao nao kunufaika na rasilimali hiyo.

Walijua kuwa hilo litatokea kutokana na kuelezwa kuwapo kwa fursa anuai zikiwamo ajira za moja kwa moja au mbadala zitokanazo na uwekezaji katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, vikiwamo viwanda.

Wakazi wengi wa Lindi na Mtwara waliamini pia kuwa gesi hiyo itaanza kutumika majumbani, hivyo kuwapunguzia gharama za nishati ya kupikia. 

Kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), serikali ilieleza kuwa wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara wangepewa kipaumbele katika hilo.

Pia ilielezwa wakati huo kuwa kwa kuanzia, nyumba zipatazo 100 mkoani Lindi zitaunganishwa na gesi hiyo huku Mkoa wa Mtwara ukiahidiwa kuanza na nyumba 300.

Ahadi hiyo ilitolewa wakati wa sherehe za uzinduzi wa mradi wa gesi majumbani katika Kijiji cha Mnazi Mmoja mkoani Lindi. 

Lakini, miezi mingi imepita tangu ahadi itolewe na hadi sasa hakuna hata nyumba moja iliyounganishiwa nishati hiyo nafuu ya kupikia. Bado wananchi wanaendelea kuishi na matumaini ingawa ni dhahiri kuwa itafika wakati matumaini hayo yatatoweka iwapo ahadi hiyo haitatekelezwa kwa muda mrefu.

Pamoja na unafuu wa gharama, lakini wataalamu wanaeleza pia kuwa matumizi ya gesi yatapunguza kwa kiasi kikubwa athari kwa mazingira, kwani yatapunguza matumizi ya kuni na mkaa kama nishati za kupikia.

Mjasiriamali, Zainabu Ali Chingolele, mkazi wa Kijiji cha Mnazi Mmoja katika Manispaa ya Lindi, ndiye pekee aliyebahatika, kwani nyumba yake ilifungiwa mfumo wa matumizi ya gesi asilia kama sehemu ya sherehe za uzinduzi wa mradi huo. Hadi leo yeye ndiye anabaki kuwa mtu pekee

anayetumia gesi asilia kwa ajili ya kupikia.

Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Mama Chingolele anasema alifurahi sana alipochaguliwa kuwa mtu wa kwanza kufungiwa mfumo wa gesi ya kupikia nyumbani kwake.

Anasema anajiona mwenye bahati kwani tangu mradi huo uzinduliwe Julai mwaka jana, hakuna mtu mwingine aliyeunganishiwa gesi nyumbani kwake.

Akieleza uzoefu wake wa matumizi ya gesi kama nishati ya kupikia, mama huyo anabainisha kuwa ina manufaa makubwa kwani licha ya kuwa rahisi lakini pia haichafui hali ya hewa kama kuni.

“Sasa hivi hakuna tena shida ya nyumba kuchafuka kwa moshi au majivu ya kuni au mkaa,” anasema.

Anasema iwapo mradi huo ungetekelezwa kikamilifu, ni dhahiri wakazi wa eneo hilo wangekuwa wamepiga hatua kubwa kimaendeleo, kwani wangeweza kutunza fedha nyingi na muda unaotumika kutafuta kuni na mkaa.

“Mazingira yetu pia yangekuwa mazuri kwani tungeacha kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa. Hivi sasa kuni zinapatikana mbali sana na makazi ya watu kwani miti ya karibu imekatwa na

Kumalizika, hivyo watu wanatumia muda mrefu kwenye kutafuta kuni,” anasema.

Aliiomba serikali kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa mradi huo wa gesi majumbani kwani unaonekana kama ulizinduliwa kwa lengo la kutaka kura kwa wananchi na si kuwasaidia

kuondokana na adha ya upatiakaji wa nishati ya kupikia.

“Kwa kweli wananchi wameshaanza kusema uzinduzi ule ulikuwa ni moja ya kufanya kampeni za uchaguzi uliopita na si kumsaidia mwananchi ili kunufaika na gesi,” anasema Chingolele

mwenye watoto tisa.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mihogoni katika Kata ya Mnazi Mmoja, Asha Ismail Hassan, alibainisha kuwa wananchi wa mtaa huo walipata matarajio makubwa ya kuanza kunufaika na

uwepo wa gesi itokayo Mtwara, ambapo bomba lake limepita kwenye maeneo yao.

Amesema kuwa kupitia matumizi ya gesi wangeweza kupunguza makali ya maisha kwani matumizi ya nishati ya mkaa kwa sasa ni gharama kubwa. Anasema kwa mwezi mmoja wanalazimika

kutumia takriban Sh 50,000 ambapo kwa matumizi ya nishati ya gesi wangeweza kutumia Sh 15,000 tu, hivyo kiasi kinachobaki wangeweza kutumia kwa matumizi mengine, ikiwamo kununua

chakula au kusomesha watoto.

“Kwa sasa kupitia matumizi ya mkaa tunatumia kiasi kikubwa cha fedha kwa kimfuko kimoja ambacho kinaweza kutumika kwa siku saba tunanunua kwa Sh elfu 15,000 hivyo gesi tuliona ndiyo mkombozi wetu,” anasema Asha.

Diwani wa Kata ya Mnazi Mmoja, Saidi Mchinjita, amekiri kuutambua mradi huo na kuwa wananchi waliupokea vizuri kwa matumaini makubwa lakini hadi sasa hajui ni kwa nini

haujatekelezwa.

Mchinjita ametoa ushauri kwa serikali kupitia TPDC kuharakisha utekelezaji wa mradi huo na kuomba kuwashirikisha wananchi wenyewe kwa kuwapa elimu ya utumiaji na uchangiaji, kwani

wananchi wakipatiwa elimu ya kutosha juu ya wapi wanatakiwa wawajibike katika kuhakikisha gesi inaingia kwenye nyumba yake itarahisisha uchagngiaji kwa hiari.

“Naomba serikali kuwaelimisha wananchi watambue wajibu wao hasa kiasi gani wanawajibika kuchangia kama ambavyo wanachangia kwenye umeme, kwa kuwa hali ya upatikanaji wa

nishati za kupikia kwa sasa ni tatizo sana kwenye maeneo yetu,” anasema diwani huyo ambaye wakati mradi huo unazinduliwa hakuwa mwakilishi wa kata hiyo.

Shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asili zilianza hapa nchini miaka ya 1950 kupitia Kampuni ya Agip kutoka Italia.

Kampuni hiyo ilifanya ugunduzi wa kwanza katika Kisiwa cha Songosongo kilichopo Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi mwaka 1974, ambapo ulifuatiwa na ugunduzi mwingine katika eneo la

Mnazi Bay lililopo mkoani Mtwara mwaka 1982. Hata hivyo, gesi asili hiyo haikuendelezwa kwa kuwa ilionekana haina manufaa ya kiuchumi kwa wakati huo.

Baada ya ugunduzi huo TPDC iliendelea kufanya utafiti ikiwa ni pamoja na kuchimba visima mbalimbali kwa ajili ya kuthibitisha kiasi cha gesi asilia kilichopo katika maeneo ambako gesi asilia

iligunduliwa. Hadi Novemba 2014 kiasi cha gesi asilia iliyogunduliwa nchini ni futi za ujazo trilioni 53.28.

Ili kuhakikisha nchi inanufaika na rasilimali ya gesi asilia iliyogunduliwa, serikali kupitia TPDC imekamilisha mradi wa ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi asilia katika maeneo ya

Msimbati, mkoani Mtwara na Songosongo mkoani Lindi, pamoja na kutandaza bomba la kusafirishia hiyo gesi kutoka Mtwara kupitia Somanga Fungu, ambapo lengo la serikali ni

kuhakikisha kuwa gesi hiyo mbali ya matumizi mengine itumike katika kuzalisha umeme na matumizi ya majumbani, ambapo tayari baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam wameanza

kunufaika pia kutumia gesi hiyo kwenye magari.

Aidha, kunatarajiwa kujengwa kiwanda cha kusindika gesi asilia kwa matumizi ya ndani na nje ambacho kitajengwa eneo la Likong’o katika Manispaa ya Lindi. Mradi huo unatarajiwa

kugharimu takriban dola za Marekani kati ya bilioni 40 na 60.

Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano wa TPDC, Dk.Wellington Hudson, ameeleza kuwa mkakati wa kuwaunganishia wananchi gesi majumbani ambao uzinduliwa mwaka 2020 ni kwa ajili ya mikoa ya Lindi na Mtwara na kuwa mradi huo bado upo.

Amesema kinachosababisha ucheleweshaji wa utekelezaji wake ni ukosefu wa fedha na kuahidi kuwa kwenye mwaka huu wa fedha serikali imetenga fedha kwa kuendelea na utekelezaji wa

mradi huo.

“Bado serikali inaona umuhimu wa kuwafikishia wananchi gesi asilia majumbani kwa ajili ya matumizi ya kupikia.

Kilichokwamisha ni fedha lakini kwenye bajeti hii tayari zimetengwa, hivyo utakamilika,” anasema Dk. Hudson.