Mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali yasiyokuwa ya kodi umezidi kuimarika kuthibitisha umuhimu wake katika kuongeza mapato, pongezi kwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuanzisha Government e-Payment Gateway kwa kifupi GePG.
Katika kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa mapato ya ndani unaongezeka na usimamizi wake unaboreshwa, Wizara ya Fedha na Mipango imebuni na kuunda mfumo wa kielektoniki unaotumika kukusanya fedha zote za umma.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James, mfumo wa GePG ulianzishwa ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizokuwamo serikalini katika ukusanyaji wa fedha za umma.
Anazitaja changamoto hizo kwamba ni pamoja na gharama kubwa za miamala inayohusu makusanyo ya fedha za umma, utaratibu usio rafiki kwa mlipaji wa huduma za umma unaoanzia namna anavyopatiwa Ankara na anavyolipia ankara yake.
Dotto anasema changamoto nyingine ni namna ya kuthibitisha malipo, anavyopatiwa stakabadhi hadi anavyopatiwa huduma; kulikuwa na machaguo machache ya njia za kulipia (mabenki, mitandao ya simu za mkononi au mawakala) kwa sababu kuongeza machaguo kulikuwa kunaongeza gharama za ukusanyaji kwa taasisi.
Anasema ilipohitajika kufungamanisha mfumo wa ankara wa taasisi na mifumo ya ulipaji (kama vile mabenki, mitandao ya simu za mkononi na mawakala wakubwa (aggregators) gharama ilikuwa kubwa, kwa sababu kila mfumo ulifungamanishwa peke yake; haikuwa rahisi kupata taarifa ya makusanyo yanayofanyika kwa wakati huo huo (Real time collection reports).
“Taasisi zilikuwa zinasimamia mikataba mingi inayohusu makusanyo ya fedha za umma kwa kuwa kila njia ya kulipia ilitakiwa kuwa na mkataba wake; kulikuwa na utofauti katika viwango ambavyo kila taasisi ilikuwa inalipia kama gharama ya miamala kwa njia ileile ya malipo (Kwa mfano; benki/mtandao mmoja wa simu ulikuwa unatoza viwango viwili tofauti kwa taasisi mbili za umma anazozikusanyia fedha za umma).
“Fedha zinazokusanywa na taasisi ya fedha hazikuwa zinaingia moja kwa moja kwenye akaunti ya taasisi inayotoa huduma mpaka baada ya kipindi fulani ili kuruhusu usuluhishi wa miamala kufanyika kwanza, hivyo kuchelewesha fedha kwenda kuwahudumia wananchi,” anasema Katibu Mkuu Dotto.
Anasema ili kukabiliana na changamoto hizo na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa fedha za umma, Wizara ya Fedha na Mipango ikishirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ilibuni na kutengeneza Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji Mapato ya Kodi, Maduhuli, Tozo na Huduma Mbalimbali za Serikali (GePG).
“Huu ni mfumo unaowezesha ukusanyaji wa fedha za umma kielektroniki. Mfumo huu umebuniwa na kutengenezwa na wataalamu wa ndani wa Serikali. Mfumo huu upo kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma (PFA) ya mwaka 2001 kupitia marekebisho ya mwaka 2017 (Sura 348), na Waraka wa HAZINA Namba 3 wa mwaka 2017.
“Sheria ya Fedha za Umma inawataka maafisa masuuli wote kukusanya fedha za umma kupitia mfumo wa GePG. Mfumo huu ulianza kutumika rasmi Julai 2017, ambapo ulianza na taasisi saba (7). Kwa sasa mfumo huu unatumiwa na taasisi za umma zaidi ya 670, mfumo huu ndio unatoa kumbukumbu namba (Control number) ya kulipia huduma na tozo mbalimbali za Serikali.
“Kuanzishwa kwa mfumo wa GePG kumeleta faida kubwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa uwazi na udhibiti katika ukusanyaji wa fedha za umma, kupata taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu makusanyo, kuwa na viwango na utaratibu unaofanana katika ukusanyaji wa fedha za umma kwa taasisi zote za umma.
“Kuchochea ubunifu katika ukusanyaji wa fedha za Serikali na sekta ya fedha kwa ujumla kwa kuweka mazingira rafiki na ya usawa kwa wakusanyaji, kutoa huduma bora na rahisi ya malipo ya fedha za umma, hivyo kuchochea ongezeko la makusanyo, fedha kufika haraka katika akaunti kuu za makusanyo zilizoko Benki Kuu.
“Kuwasaidia benki na mitandao ya simu kuwa na sehemu moja tu ya kuunganisha mifumo yao na mifumo ya taasisi za umma (Single point of Linkage), hivyo kuzifikia taasisi za umma na kutoa huduma za kifedha kwa urahisi na kuziwezesha benki na mitandao ya simu kuwa na mazingira rafiki na ya usawa katika ukusanyaji wa fedha za umma.
“Kuzisaidia taasisi za umma kupunguza gharama zitokanazo na uwekezaji katika miundombinu ya Tehama pamoja na “Software Development” katika suala la ukusanyaji wa mapato, urahisi katika usuluhishi wa miamala na usuluhishi wa taarifa za kibenki, kupunguza gharama za miamala inayohusu ukusanyaji wa fedha za umma,” anasema Dotto.
Mwaka wa Fedha 2020/21, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilitoa kazi kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuufanyia tathmini ya kiutendaji Mfumo wa GePG. Katika taarifa hiyo imebainika kuwa Mfumo wa GePG umewezesha kuongezeka kwa makusanyo ya Serikali kwa ujumla wake na kwa taasisi moja moja.
Anatoa mfano wa makusanyo ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yameongezeka kutoka Sh bilioni 95 hadi Sh bilioni 115. Baada ya kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki, Wakala wa Vipimo (WMA) mapato yao yameongezeka kutoka kiasi cha Sh bilioni 1 kwa mwezi kabla ya mfumo wa GePG mpaka kiasi cha Sh bilioni 2.5 kwa mwezi baada ya kujiunga na GePG.
Katibu Mkuu huyo anasema taasisi nyingine zimepunguza gharama walizokuwa wanalipia ada za miamala ya kielektroniki inayohusu makusanyo ya fedha za umma, huku akitoa mfano wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lililokuwa likilipa zaidi ya Sh bilioni 38 kwa mwaka kwa mawakala wa kuuza umeme. Baada ya kufunga mfumo wa GePG kwa sasa shirika halilipi chochote.
Naye Mkurugenzi wa Mifumo ya Kifedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, John Sausi, amesema kuwa wakati umefika sasa kwa Watanzania kutumia mfumo huo wa GePG ili kuwa na uhakika wa malipo yao.
“Ndugu zangu wahariri naomba mtumie fursa mlizo nazo katika kuhakikisha kuwa mnawaelimisha Watanzania kuhusu umuhimu wa kutumia mfumo huu wa GePG ili fedha zinazolipwa kupitia “CONTROL NUMBER” zifike moja kwa moja serikalini, mfumo huu unaiwezesha Serikali kuona mapato yote kupitia mfumo huu na kuhakikisha fedha za umma hazipotei,” anasema Sausi.
Sausi amewataka Watanzania kuhakikisha wanaepuka kulipa pesa taslimu kwa kuwa mfumo huo sasa umepitwa na wakati na fedha hizo hazifiki kwa wakati na huenda zinaweza kupotea.
Ameyataja mafanikio yaliyopatikana kupitia mfumo wa GePG kwamba ni pamoja na kuokoa fedha za Serikali ambazo zimekuwa zikipotea kabla ya mfumo huo, pia kuiwezesha Serikali kupata na kuona taarifa mbalimbali zinazohusu ukusanyaji wa mapato.
Baadhi ya taasisi ambazo zimenufaika na mfumo huo wa GePG ni pamoja na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Mkoa wa Arusha (AUWASA).
Akizungumza na wahariri waliotembelea makao makuu ya TANAPA kujionea namna mfumo huo wa GePG unavyofanya kazi kwa ufanisi, Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulika na huduma za jamii, Juma Kuji, anasema tangu kuanzishwa kwa mfumo wa makusanyo wa fedha za Serikali, TANAPA imeokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo zilikuwa zikitumika kuwalipa watoa huduma kutoka benki mbalimbali.
Kuji anasema TANAPA ilikuwa ikilipa asilimia moja ya mapato yake yote inayokusanya kwa mabenki hayo, ambazo ni kati ya Sh bilioni 1 hadi Sh bilioni 3 kwa mwaka. Huku akisisitiza kwamba sasa hakuna malipo yoyote yanayofanyika kwa benki hizo kutokana na matumizi ya mfumo wa GePG.
Akizungumzia mafanikio ya TANAPA baada ya kuunganishwa na mfumo wa GePG, Mkuu wa Kitengo cha Tehama, Boniphace Maliki, anasema hapo awali kabla shirika hilo halijaanza kutumia mfumo wa GePG, kila geti la hifadhi lilikuwa na akaunti yake, hivyo kusababisha shirika hilo kuwa na akaunti zinazokaribia 100, jambo ambalo lilikuwa linachelewesha kupata taarifa za makusanyo na ufanyaji wa usuluhishi wa kifedha (Bank reconciliation).
Maliki anasema baada ya kujiunga na GePG, TANAPA imebaki na akaunti 8 tu, ambazo akaunti 4 ni za shilingi na nyingine 4 ni za dola ya Marekani.
Anasema mfumo huo umeliwezesha shirika hilo kutatua changamoto nyingi za makusanyo kwa kuwa makusanyo yote yanasimamiwa na mfumo wa GePG.
Katika ziara ya kujifunza namna mfumo wa GePG unavyofanya kazi, wahariri walitembelea taasisi nyingine inayotoa huduma ya maji, yaani Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka mkoani Arusha (AUWSA), ambapo walipata taarifa jinsi mfumo wa GePG ulivyorahisisha makusanyo na kupunguza usumbufu kwa wateja.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mkuu wa Kitengo cha Tehama wa AUWSA, Ndaki Tito, anasema baada ya kujiunga na mfumo huo katika mwaka wa fedha 2017/18 taasisi hiyo imefanikiwa kuongeza mapato yake kutoka Sh bilioni 1.2 hadi Sh bilioni 1.6 kwa mwezi.
Tito anasema kuwa mbali na shirika kuongeza mapato yake, pia wateja wamefaidika kwa kiasi kikubwa kwa sababu mfumo wa GePG umeruhusu kufanya malipo kupitia njia mbalimbali zikiwamo mitandao ya simu, hivyo kupunguza usumbufu kwa wateja wake.
“Pamoja na mafanikio hayo, kuna changamoto wanazokumbana nazo kupitia mfumo huo wa GePG, ikiwamo changamoto ya mtandao.
“Changamoto ninayoiona kwa upande wa GePG ni utegemezi zaidi kwa upande wa mtandao, maana bila ya mtandao huwezi kuona mapato na changamoto nyingine ni elimu kwa wananchi, ambapo wananchi wengi hawana uelewa kuhusu matumizi ya namba ya malipo (control number) kuwa unaweza kulipia katika benki yoyote,’’ anasema Tito.