Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Katika kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania, vijana wa Generation Samia (Gen S) wameonyesha mfano mzuri wa mshikamano na uzalendo kwa kufanya shughuli ya usafi katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dodoma, huku wakitoa wito kwa jamii kushikamana na kuendelea kujenga taifa lenye maendeleo endelevu.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya usafi, Kiongozi wa vijana Hao(Gen S) Mkoa wa Dodoma, Sonatah Nduka amesema kuwa shughuli hiyo ni sehemu ya kuadhimisha siku hiyo muhimu kwa vitendo ili kuweka alama ya uzalendo kwa jamii na vizazi vijavyo kwa ujumla.

“Leo, tumeungana kama vijana wa Kizazi cha Samia kufanya usafi katika maeneo ya umma, na hii ni sehemu ya kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru,tunataka kuonyesha kwa vitendo kuwa tuna dhamira ya kutunza mazingira yetu na kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuleta maendeleo endelevu, “amesema

Licha ya hayo Nduka ameeleza kuwa kama vijana wanapaswa kujivunia utaifa wao na kutambua mchango wa kila mmoja katika kujenga taifa lenye mafanikio,” amesema

Vijana hao walifanya usafi katika maeneo ya Hospitali, soko kuu, barabara za jiji, na maeneo ya shule,ikiwa ni ishara ya kujitolea kwa hiari na kuwa mfano bora wa uongozi na uzalendo miongoni mwa vijana.

Kwa upande wake Msaidizi mwandamizi wa Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma ,Paul Mageni amewashukuru vijana hao kwa kutenga muda kufanya usafi katika Hospitali hiyo Kwa kuweza kutambua umuhimu wa wagonjwa wanaolazwa hospitali hapo kwani mazingira mazuri pia ni tiba kwa wagonjwa.

“Mmefanya ibada njema, kuwajali watu wasiweza ni ibada, ni wajibu wetu kuhakikisha tunamuunga mkono Mhe.Rais kwenye suala zima la kutunza mazingira ikiwa ni ajenda kama nchi kuhakikisha tunapata hewa safi kwani afya ya mtu huanza kutunzwa kwa kuzingatia mazingira yanayotuzunguka ili kupata hewa safi na kuepukana na magonjwa ya mlipiko”amesema

Aidha amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuleta maendeleo, akisema kuwa hatua ndogo kama hizo zinaweza kuwa na mafanikio makubwa katika kuboresha hali ya maisha na kuendeleza utamaduni wa ushirikiano.

“Usafi ni jambo la msingi, lakini kubwa zaidi ni kuwa na mshikamano kama jamii,tunaweza kufanikisha mambo makubwa zaidi kama tutashirikiana, kila mmoja akichukua jukumu lake kwa dhati,leo, tunadhihirisha kwamba vijana wa Generation Samia wamekuwa somo kwa wanajamii kuwa na utayari wa kuchangia kuleta mabadiliko chanya kwa taifa letu,”amesisitiza.

Mmoja wa vijana hao Neema Julias ameeleza kuwa miaka 63 ya Uhuru imewafunza uzalendo na kueleza kuwa wao kama vijana wametumia nafasi hiyo kufanya uzalendo kwa shughuli za kijamii na kuiasa jamii kuhusu umuhimu wa kushikamana katika kushinda changamoto mbalimbali zinazokikabili taifa, ikiwa ni pamoja na vita dhidi ya maradhi, ujinga, na umasikini.

“Ni vizuri kuona vijana wanapiga hatua kwa kufanya kazi nzuri kama hii, tunaahidi kuendeleza jitihada hizi za kuboresha mazingira yetu na kujenga taifa lenye mafanikio,” amesema