Tatu Saad, JAMHURI MEDIA

Klabu ya Geita Gold imetangaza nia ya kushiriki katika michuano ya Kimataifa msimu wa 2023/24 kwa ubora mkubwa zaidi kwa kuweka mikakati mbalimbali itakayowasaidia katika kufikia malengo hayo.

Katibu mtendaji wa Geita Gold, Simon Shija amesema wamedhamiria kuona wakirejea katika michuano hiyo ya Kimataifa baada ya kujifunza mambo mengi kutoka kwa klabu ya Simba na Yanga ambazo zinashiriki michuano hiyo mpaka sasa.

“Kuna mambo mengi tumejifunza na kutambua wapi tulipokosea mwanzoni mwa msimu huu tuliposhiriki Michuano ya Kombe la Shirikisho, tunaamini tukirudi tena tutakuwa imara zaidi.” Amesema Shija.

Amesema kinachowasaidia Yanga na Simba kufanya vizuri katika michuano hiyo ni uzoefu waliokuwa nao katika michuano hiyo na uwekezaji mkubwa unanifanyia na klabu hizo.

Kingine kinachowasaidia Simba na Yanga ni usajili mzuri wa wachezaji na kuwalipa mishahara kwa wakati, bonsai na kuweza kumudu gharama wa apokee mda kuweka kambi popote hali ambayo unaleta hamasa kwa wachezaji kufanya vizuri.

“Klabu za Simba SC na Young Africans zinasajili, kulipa mishahara mizuri kwa wakati, bonasi na kuweka kambi sehemu yoyote, hivyo inaleta motivation kwa wachezaji kufanya vizuri, kwetu klabu ndogo hili linatupa hamasa kubwa,” amesema Shija.

Shija amesema wamejipanga vizuri ili kuhakikisha wanamaliza ligi kuu ya Tanzania wakiwa nafasi nne za juu ili waweze kuwa sehemu ya timu zitakazoshiriki tena michuano ya Kimataifa msimu ujao.

“Sisi kama timu tutapambana tusitoke kwenye nafasi tuliyopo, pili kupambana kwa nguvu zote kupigania nafasi nne za juu japokuwa waliopo juu yetu wanatuzidi alama nyingi.

“Tumejipanga kuhakikisha tunamaliza katika nafasi nne za juu ili tuwe sehemu ya timu zitakazowakilisha nchi kimataifa msimu ujao, kama tutafanikisha hili, itakuwa ni mara yetu ya pili mfululizo.”amesema Shija

Geita Gold FC kwa mara ya kwanza ilishiriki Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2022/23, na kuondolewa katika hatua ya awali kwa faida ya bao la ugenini dhidi ya Hilal Alsahil ya Sudan, ikipoteza ugenini 1-0 na kupata ushindi wa 2-1 nyumbani Tanzania.