Serikali ya Tanzania imesema deni la jumla la taifa liliongezeka kwa Sh trilioni 3 katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Desemba hadi Machi mwaka huu.
Serikali hiyo imepuuzilia mbali taarifa zilizochapishwa na gazeti moja nchini humo zilizodai kwamba deni la taifa hilo la Afrika Mashariki liliongezeka Sh trilioni 12 katika kipindi hicho.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi amelitaka gazeti la mwananchi “kuomba radhi kwa umma kwa siku mbili mfululizo kuanzia kesho Jumapili” kupitia ukurasa wa mbele wa gazeti hilo na kwenye mitandao ya kijamii.
Dkt Abbas amesema baada ya gazeti hilo kusisitiza “kuwa hawana nia mbaya, serikali imezingatia utetezi huo na inawapa nafasi ya kujirekebisha zaidi”.
Taarifa iliyotolewa na idara ya mawasiliano ya Benki Kuu ya Tanzania inasema katika kipindi hicho, deni la serikali liliongezeka kutoka shilingi trilioni 47 hadi shilingi trilioni 49 pesa za Tanzania.
“Deni hilo linajumuisha mikopo kutoka kwa nchi wahisani, mashirika ya fedha ya kimataifa pamoja na mabenki ya kibiashara ya kimataifa,” taarifa hiyo inasema.
“Deni la ndani la serikali linajumuisha dhamana za serikali za muda mfupi na hati fungani za serikali pamoja na madeni mengineyo.”
Serikali inasema deni la nje la sekta ya kibinafsi katika kipindi hicho cha kuanzia Desemba 2017 hadi machi 2018 lilipanda kwa shilingi tilioni moja kutoka Sh trilioni 9 hadi Sh trilioni 10.
“Kwa hivyo, deni la taifa ambalo linajumuisha deni la serikali la ndani na nje la sekta ya binafsi liliongezeka kwa Sh trilioni 3 kutoka Sh trilioni 56 mwezi Desemba 2017 hadi Sh trilioni 59 mwezi Machi 2018,” taarifa hiyo ya BoT inasema.
Benki hiyo imesema ongezeko hilo lilitokana na mikopo mipya kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kadhalika, kutokana na malimbikizo ya riba, hasa kutoka kwa nchi za kundi lisilo la wanachama wa wa Paris ambazo hazijatoa msamaha wa madeni kulingana na makubaliano.
Benki hiyo imesema kuwa licha ya hayo, “deni la taifa bado ni himilivu”.
“Kuongezeka kwa deni la taifa kunatokana na jitihada za kujenga mazingira bora zaidi ya kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi ili kufikia azma ya Tanzania ya viwanda yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.”
Tamko la benki hiyo linaonekana kukariri msimamo wa Rais wa Tanzania John Magufuli ambaye majuzi alitoa wito kwa wananchi kuwapuuza wanaodai kwamba Tanzania “inakopa sana”.
Kiongozi huyo alisema mikopo inayochukuliwa na taifa hilo ina manufaa na itachochea ukuaji wa uchumi.
Wakati wa kuadhimisha miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika sherehe zilizofanyika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, kiongozi huyo alieleza matumaini kwamba uchumi wa Tanzania utatengemaa.
“Taifa letu linakwenda vizuri, uchumi wetu unakua vizuri, mwaka jana umekuwa kwa wastani wa asilimia 7 na mwaka huu tunatarajia utakua kwa wastani wa asilimia 7.1, mfumuko wa bei umeendelea kuwa chini kwa wastani wa asilimia 4,” alisema.