DAR ES SALAAM

NA JOVINA BUJULU, MAELEZO


Hivi karibuni Rais John Magufuli aliwakaribisha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi mbalimbali za umma katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma kwa ajili ya kutoa mchango wao kifedha kwa serikali.
Michango iliyotolewa ilikuwa ya aina mbili. Kwanza, ilikuwa ni mchango wa asilimia 15 ya mapato ya taasisi hizo. Mchango huu unatolewa kwa mujibu wa sheria ya fedha ambayo inataka taasisi ambazo shughuli zake zinahusisha kukusanya maduhuli, kutoa asilimia 15 ya makusanyo hayo kwa mwaka kama mchango wake kwa mfuko mkuu wa serikali.
Pili, mashirika ambayo hufanya biashara na yana hisa za serikali ndani yake, yanapaswa kutoa gawio kwa serikali kama mbia katika biashara hiyo.
Gawio na michango hii ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya mapato ya serikali kusaidia kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu kwa jamii ikiwemo afya, maji, elimu, nishati, kuboresha miundombinu pamoja na mahitaji yote muhimu katika jamii.
Gawio la michango hii ni muhimu sana kwa sababu huiwezesha serikali kujiendesha kwa kujitegemea na kupunguza utegemezi wa fedha za wafadhili au mikopo kutoka katika nchi wahisani na  mashirika ya kimataifa.
Kimsingi gawio ni faida ya moja kwa moja ambayo mwekezaji anaipata kutokana na uwekezaji wake.
Wakati akipokea gawio na michango kutoka katika mashirika ya umma na kampuni mwaka jana, Rais Dk. John Magufuli alibainisha umuhimu wa kodi kwa kusema: “Serikali  inategemea vyanzo vya aina mbili kupata fedha, ikiwemo visivyo vya kodi ambavyo ni pamoja na kupata gawio kutoka taasisi ambazo serikali ina hisa au inamiliki kwa  asilimia 100 na vyanzo vya kodi”.
Kwa maana hiyo, mashirika ya umma, wakala, waasisi na kampuni kutoa gawio na mchango kwa serikali ni muhimu na ni suala ambalo halipaswi kuwa na mjadala, kwani gawio na michango hiyo inatolewa kisheria.
Serikali pia  ni muhimu ipate gawio kutokana na uwekezaji wake kupitia mashirika hayo. Kwa kuwa gawio linatokana na faida, ina maana kuwa ili serikali ipate gawio, ni lazima mashirika hayo yapate faida katika shughuli zake.
Hivi karibuni Rais Magufuli amepokea gawio la Sh trilioni 1.05 kutoka katika mashirika ya umma, taasisi na kampuni 79 kati ya taasisi 266 zinazopaswa kutoa mchango na gawio kwa serikali.
Rais alionyesha kushangazwa na uchache wa taasisi na mashirika yanayotoa gawio na michango na kusema kuwa ni heri kuwa na mashirika machache yanayoifaidisha serikali kuliko kuwa na mengi ambayo ni mzigo kwa serikali.
Kutokana na hilo, Rais Magufuli alitoa siku 60 kwa wakuu wa taasisi na mashirika hayo kuhakikisha wanatoa gawio na michango kwa serikali, la sivyo wajiondoe wenyewe.
“Hatuwezi kuendelea kukaa na mashirika ya namna hii. Hatuwezi kuendelea kukaa na viongozi wa namna hii. Hatuwezi kuendelea kukaa na bodi za namna hii ambazo tunazungumza hawataki kuelewa,” alisisitiza Rais Magufuli.
Kauli hiyo haikuwa imetolewa na rais kwa mara ya kwanza, kwani wakati akipokea gawio la Sh bilioni 736.36  kutoka kwa taasisi, mashirika ya umma na makampuni 43 mwaka jana, alisema kwamba Tanzania ina mashirika zaidi ya 90, yenye kustahili kutoa gawio na mchango wa kifedha kwa serikali, lakini licha ya idadi hiyo kubwa, pamoja na uwekezaji uliofanywa na serikali katika mashirika hayo, nchi haijanufaika kwa kuwa gawio linalopatikana ni dogo sana na mashirika mengi hayatoi gawio, suala ambalo linatakiwa kupatiwa ufumbuzi.
“Japokuwa mwaka huu wamejitokeza wengi kuliko miaka iliyopita bado mapato ni madogo ikilinganishwa na kile ambacho serikali ilistahili kukipata kutokana na uwekezaji wake kwenye maeneo yote yanayoguswa,” alisema Rais Magufuli.
Alionyesha kufurahishwa na baadhi ya mashirika na kampuni ambazo zilitoa gawio kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake alisema: “Kilichonifurahisha katika utoaji wa gawio kwa mwaka huu (2018) ni kuona Shirika la TAZAMA Pipeline wametoa Sh milioni 681.818, maana tangu kuanzishwa kwake enzi za Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1968, hawajawahi kutoa hata senti tano, walikuwa wanatazama tu.”
Pamoja na Shirika la TAZAMA kutoa gawio kwa mara ya kwanza, baadhi ya  mashirika na kampuni nyingine ambazo zilitoa gawio kwa mara ya kwanza ni pamoja na Mamlaka ya Uendelezaji wa Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KADCO), Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na UTT Asset Management and Investment iliyo chini ya Wizara ya Fedha.
Takwimu zinaonyesha kwamba, mwaka 2014/15  serikali ilipata gawio la Sh bilioni 130.686 kutoka katika mashirika na kampuni 24 na mwaka 2015/16 gawio lilikuwa Sh bilioni 246.3 kutoka katika taasisi za umma 25.
Hali hiyo haikuridhisha, hivyo serikali ilianza kuchukua hatua ambazo zilizaa matunda, ambapo idadi ya mashirika na kampuni zilizotoa gawio na mchango kwa serikali ziliongezeka hali kadhalika kiasi cha fedha kilichotolewa.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema kuwa mapato ambayo yanatokana na gawio na michango ya kampuni, taasisi, wakala na mashirika yameongezeka kutoka Sh bilioni 162.04 mwaka 2014/15  hadi kufikia Sh trilioni 1.05 kwa mwaka 2018/19.
Pamoja na ongezeko hilo la gawio, rais alisema kuwa serikali imewekeza mtaji wa Sh trilioni 56 katika mashirika 266, na kuonyesha kushangazwa na mashirika 187 ambayo hayakutoa gawio kwa mwaka 2018/19.
Rais Magufuli alitoa agizo kwa Msajili wa Hazina, Athuman Mbuttuka, kuangalia utaratibu wa kisheria ili kuyawajibisha mashirika na taasisi zisizotekeleza wajibu wao.
“Agizo langu kwa Msajili wa Hazina ni kuhakikisha kuwa mashirika na taasisi zote zenye kustahili kutoa gawio kwa serikali zinafanya hivyo. Yatakayoshindwa uongozi wake ubadilishwe au mashirika hayo yafutwe kabisa. Hatulipendi shirika, tunapenda pesa,” alisisitiza Rais Magufuli.
Alitaja mambo kadhaa ambayo yanafanya mashirika, kampuni na taasisi kushindwa kutoa gawio kuwa ni pamoja na uongozi mbovu, kukosekana kwa ufuatiliaji madhubuti, udanganyifu, ubadhirifu na rushwa.
Kwa upande wake, Waziri Mpango anasema kuwa ongezeko la gawio mwaka huu limetokana na sera na usimamizi bora wa rasilimali za serikali ikijumuisha kuongezeka kwa mashirika yanayotoa gawio na michango, kuimarisha ufuatiliaji na uchambuzi wa mashirika hayo ili kuhakikisha kuwa yanaongeza ufanisi.
Kwa upande wake, Mbuttuka anasema kuwa ofisi yake imefanya juhudi kubwa kuhakikisha inarudisha hisa za serikali ambazo awali ilikuwa inadhulumiwa katika kampuni mbalimbali.
Kutokana na agizo la rais la kuyataka mashirika ya umma, kampuni na wakala kutoa gawio kwa serikali ndani ya siku 60, wakuu wa taasisi hizo ni lazima wajitathmini.
Kwa kuwa hili lipo kisheria, wakuu hawa hawana sehemu ya kukwepa kutekeleza. Kama watashindwa kwa kigezo cha kutokuwa na fedha, basi wanapaswa pia kuwajibika kwa sababu watakuwa wanadhihirisha kuwa wanaendesha taasisi hizo kwa hasara, jambo ambalo halitarajiwi.
Hatua hii itaunga mkono juhudi za serikali ambayo imeweka msisitizo katika kukusanya mapato ambayo ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo na ujenzi wa nchi.

MWISHO