Dar es Salaam. Sekta ya fedha nchini hasa mabenki yametakiwa kubuni namna mpya ya kuwafikia wateja wengi zaidi ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza amana, maana katika kila shilingi 100 inayotolewa na Benki Kuu, ni shilingi 40, ndiyo inaingia kwenye sekta za fedha.
Hayo yamesemwa na Gavana wa Benki Kuu, Prof Benno Ndulu katika mkutano wake na taasisi za kifedha uliofanyika Arusha, mwishoni mwa Novemba, huku lengo likiwa ni kuhakikisha Tanzania inatumia vema nafasi yake kijiografia.
Mkutano huo wa 18, uliandaliwa na Benki Kuu, ulizishirikisha taasisi zote za fedha, mabenki, mifuko ya hifadhi za jamii, mkutano huo ulizinduliwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango. Mkutano huo hufanyika kila baada ya miaka miwili,
“Fursa hizi ni nyingi ukizingatia nchi ya Tanzania ipo katikati ya bara la Afrika imepakana na upande wa Bahari ya Hindi, hivyo inayo nafasi kubwa kibiashara…nchi hii tunaweza kutumia fursa hii kuendeleza fursa ya viwanda ambayo ndiyo dhamira kuu ya serikali ya awamu ya tano.” amesema Dk. Mpango.
Waziri Mpango, alitumia fursa hiyo ya kukutana na wadau wa sekta ya fedha na kuwaachia changamto kadhaa ikiwa ni pamoja na kujiuliza wamejipangaje kuwasaidia taasisi na makampuni madogomadogo ili waweze kupata mtaji, namna ya kuifikia sekta ya kilimo ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi, maana huko ndiko Watanzania wengi walipo.
Katika sekta hiyo ya kilimo ambayo ndiyo imeajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania, kuona namna wanavyoweza kusaidiwa ili kutumia ardhi iliyopo kuzalisha ili kujenga uchumi.
Dk. Mpango amezitaka taasisi za fedha kusogeza huduma zake hadi vijijini na kuwaelezea wananchi fursa zilizopo pamoja na kuwapatia wananchi hao mikopo ya kuendeleza shughuli zao ili waweze kujikwamua kiuchumi, huku wakitakiwa kutoa elimu ili kufahamu namna wananchi wanavyoweza kushirikiana na taasisi za fedha kukuza uchumi.
Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo na wadau mbalimbali katika sekta ya fedha, Gavana wa Benki Kuu, Prof Benno Ndulu, amesema wamejadili changamoto kadhaa ambazo zimejitokeza katika sekta ya fedha.
Prof Ndulu, anasema kwamba, mabenki sasa hivi kwa ujumla yamekuwa katika hali ya kutokuwa na ukwasi mwingi kama zamani, imebidi kujaribu kutafuta njia mbalimbali ambazo zitahakikisha kuwa mabenki wanaendelea kuwa na fedha za kutosha pia kuendelea kutoa mikopo kwa sababu mikopo ndiyo nguzo kuu ya kuweza kusaidia katika kuendesha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongeza mzunguko wa fedha.
“Benki Kuu ambayo ndiyo chanzo kikubwa cha ukwasi tumejipanga, tunaangalia njia mbalimbali za kuhakikisha hata kama wamepungukiwa kwa sababu baadhi ya fedha zilizokuwa kwenye mabenki sasa haziko kule, sisi tunahakikisha wanakuwa nazo.
“Hili imebidi tulizungumze kwa sababu lipo na tumekubaliana na mabenki kwamba na wao wakatafute fedha huko nje, kuna wananchi wengi hawajafikiwa na mfumo wa benki, maana katika kila shilingi 100 tunayotoa, shilingi 40 tu ndiyo inaingia kwenye mfumo wa benki, huku shilingi 60 ikiwa nje ya mfumo.
“Mabenki yaende kuzifuata hizo, wahamasishe amana kwa kutumia njia mbalimbali. Tumedhamiria kuwa, tumekuwa tukiwekeza sana kwenye miundombinu, tunatakiwa kuimarisha uwezo wa logistics, eneo jingine la kulifanyia kazi ni suala la mikopo ya muda mrefu, uwekezaji unahitaji mikopo ya muda mrefu na uendeshaji ni fedha ya muda mfupi.
“Kitu kimoja tumekubaliana haiwezekani fedha yote ya maendeleo na ya kuwekeza ikatoka katika vyanzo vya ndani peke yake, hata China wanapata fedha kutoka nje, tena ndio nchi inaongoza duniani kwa kupata fedha za uwekezaji kutoka nje…lazima tujue ni namna gani tutaendelea kuhamasisha uwekezaji wa kutoka nje, pamoja na mabenki kwenda nje kutafuta vyanzo vya fedha za mikopo ya muda mrefu.
“Imebidi tuhakikishe hili nalo linafanyika, mabenki mengine yameanza kutafuta fedha nje, wapo wanaopata kwenye mabenki ya ulaya, Benki ya Maendeleo ya Afrika, IFC, Benki ya maendeleo ya Ulaya, mikopo kama ile iliyoweza kusaidia Kagera Sugar na kusaidia kuinuka tena,” amesema Profesa Ndulu
Gavana Ndulu amesema, sekta ya fedha imekubaliana katika kutafuta mikopo ya kilimo, pamoja na kuboresha mifumo ya taarifa za wote wanaotaka kukopa katika sekta ya kilimo, tutakuwa na mkakati maalum wa kuwasaidia wakulima.
Hali ya ukwasi imebadilika katika sekta ya mabenki, katika mfumo wetu wa ufuatiliaji wetu wa ukwasi wa ziada ya matumizi kweye benki umefikia shilingi bilioni 530, ili isiwe mbaya inatakiwa iwe kuanzia Shilingi bilioni 300, japo hapo nyuma kweli hali haikuwa nzuri sana.
Gavana afafanua kuhusu akaunti za mashirika
Prof Ndulu, anasema Benki Kuu haijachukua pesa kwenye mabenki, fedha hizo ni zile za serikali, na kwamba Benki Kuu ni benki inayomilikiwa na serikali, na mwenye benki ndiye ameweka fedha zake pale.
Amesema, Benki Kuu haifanyi malipo kwa niaba ya serikali kwa mtu mmoja mmoja au mkandarasi, wale walioweka fedha wanapotaka kulipa fedha hizo hurudishwa kwenye akaunti zao zilizoko katika mabenki, hivyo kuondoa ile dhana kwamba kuondolewa kwa sehemu ya fedha za serikali katika mabenki kumesababisha ukwasi.
Gavana amesema, wale wanaolipwa sio serikali, kuna malipo ya wakandarasi ambao wanazo akaunti kwenye benki za biashara, fedha hizo zinalipwa kupitia akaunti ya mdai, kwa hiyo fedha hizo zinakaa benki kuu kwa muda tu, maana siku kuna fedha wanaingiza na nyingine zinatoka.
“Sema siku hizi fedha zinalala Benki Kuu, zinaamka na kufanya kazi kwenye mzungumko, sasa kama huna fedha zinazolala kwenye mabenki huwezi kuzitumia katika kuwekeza, na hiyo ndiyo changamoto za mabenki.” Amesema Prof Ndulu.
Prof Ndulu amesema, sababu kubwa ya upungufu wa fedha, unatokana na kupungua kwa fedha za misaada kutoka nje, hata upatikanaji wa mikopo kutoka nje imepungua sana. Amesema fedha za mashirika zilizohama mpaka sasa ni shilingi bilioni 234 huku ambazo bado ziko katika mabenki ni zaidi ya shilingi bilioni 700.
Gavana amesema, fedha za serikali ni asilimia 3 tu ya fedha zote ambazo zinawekezwa kwenye mabenki. Prof Ndulu amesema amana zilizoko kwenye mabenki ni shilingi trilioni 15.7.
Naye mwenyekiti wa chama cha mabenki, ambaye pia ni Mkurugenzi wa benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei, amesema kushiriki kwao katika mkutano huo kumeweza kuwasaidia walau kufahamu mipango ya serikali hasa katika maeneo ya uwekezaji.
“Sisi tunaoendesha mabenki tumefaidika baada ya kufahamu mipango ya serikali ya kuboresha biashara ya usafirishaji (transit trade), kuzifikia nchi zilizoko nje ya bahari kama vile Rwanda, Uganda, Burundi, Kongo DRC, Zambia, Malawi,” amesema Dk. Kimei.
Amesema kuna fursa nyingi ambazo zitahitaji fedha za muda mrefu na pia fedha za muda mfupi, lazima mabenki yajipange na hayawezi kutarajia kupata fedha hizo ndani pekee.
“Mimi kama Mkurugenzi Mkuu wa CRDB, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita tumepata mikopo inayozidi shilingi bilioni 500, na kuzikopesha kwenye miradi mikubwa hapa nchini, lazima tuendelee kukusanya amana.
“Tunashuruku Benki Kuu, imeweka mikakati ya kubridge gap inayotokea katika ukwasi, maana umepungua kidogo na wakati huu benki zinaweka sawa mizania yake, ili ziweze kukidhi mahitaji ya mikopo ambayo itaombwa inabidi tupate mahali pa kujihifadhi kutoka Benki Kuu.
“Lakini huko nyuma niliwahi kusema, hili jambo la kutegemea fedha za mashirika ya umma zaidi na serikalini, linavyobanwa ni fursa ya sisi mabenki kwenda kuwafikia wale wadogo wadogo, sasa tunatakiwa kutanua mitandao yetu na kuwafikia Watanzania wengi zaidi ili kukusanya amana zaidi,” amesema Kimei.