Kwanza nimpongeze CAG pamoja na watu wa ofisi yake. Niwapongeze wenyeviti wote watatu kwa taarifa nzuri walizotusomea leo asubuhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naona suala hili ni kubwa na ni zito. Nadhani ni zito hata zaidi ya kupitisha bajeti. Kwa sababu bajeti tunapopitisha, ni fedha ambazo tunakisia tunadhani kwamba zitakusanywa. Hizi tunazozizungumzia leo ni fedha zimekusanywa zikaliwa – zimeliwa kwa njia nyingi.

Kinachonisikitisha ni taarifa za kila mwaka wenyeviti wanatoa taarifa, CAG analeta taarifa – ni upotevu wa fedha, ni malipo hewa, ni manunuzi yasiyokuwako, ni wizi kila… na Serikali inakaa kimya. Kama mnaona taarifa hizi ni za uongo, kwanini msilete taarifa yenu ya kukanusha kwamba hakuna mishahara hewa?

Hakuna mambo ya ununuzi. Serikali inakaa kimya na fedha za wananchi zinaliwa kila siku, hakuna miradi inayoendelea kijijini, hakuna fedha zinazokwenda halmashauri, halafu tunakaa kila siku kuwaimbia Serikali wanakuwa kama wameweka nta kwenye masikio – hawasikii.

Leo mimi ningetegemea kwamba Waziri wa Fedha angekuwapo hapa kwa sababu hizi fedha tunazozungumzia zimetoka ofisini kwake. Lakini anaona kwamba ni kitu cha kawaida, tumezoea. Hivi wabunge tunakuja hapa kufanya nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kama shughuli yetu ni kuisimamia Serikali, na wameboronga, wamekula fedha za wananchi, tunafanya nini?

Kama ni kukataa kupitisha bajeti ndiyo kazi yetu, kama tunaweza kukataa kupitisha bajeti ya fedha ambazo tunakadiriwa kwamba zitakusanywa na hizi zote zilizoliwa tunakaa kuwaambia Serikali hawasikii, mimi ningeomba wabunge wenzangu, hizi taarifa tungekataa hadi utekelezaji wake ufanyike. Tuambiwe fedha zote za malipo hewa zinakwenda wapi?

Hivi malipo hewa si kuna mtu anayetoa? Kwa nini wananyamaza? Miradi ambayo iko chini ya kiwango inajulikana. Mali za Serikali zinauzwa.

Halmashauri ya Longido gari imeuzwa ambayo afisa amepeleka  gereji imetengenezwa kwa Sh milioni 11. Ameweka tairi mpya kabla halmashauri haijalipa hizo fedha, barua ikaja kwamba huyu afisa amenunua hiyo gari kwa Sh 1,490,000 halafu halmashauri inadaiwa Sh milioni 11 kwa gari hilo.

Eti kibali kimetoka Wizara ya Fedha kwamba huyo afisa ameuziwa hiyo gari. Halafu bado halmashauri ilipe gari ambayo yeye ndiyo amejitengenezea na kujiuzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, wizi kama huo na Serikali wanajua, nimewaeleza, halmashauri tumeisimamisha hiyo gari na tumeichukua, ni mali ya halmashauri aende kutushitaki.

Ndugu zangu, hapa tunacheza. Kuna wabunge wenzangu ambao wapya sidhani fedha zimewahi kwenda halmashaurini kwao tangu waingie hapa bungeni. Hakuna kazi za miradi ya maendeleo inayoendelea.

Kwa hiyo, mimi naona Serikali sijui niseme nini. Sijui Serikali wamechoka au wanafanya makusudi kwa sababu naumia miradi ya maendeleo isipoenda na fedha zinakusanywa.

Tunaona majumba yanaendelea kujengwa na hao maafisa na ninyi mnaona. Kwa hiyo, fedha za wananchi zinavyokwenda tunaziona, mnaona katika halmashauri zenu majengo yanaendelea, nyumba za watumishi… zinajengwa zao wenyewe, wananunua magari, ni matajiri, lakini Serikali inakaa kimya… Kwa hiyo nasema hapa sijui wabunge wenzangu mtaongea nini kwa sababu kila mbunge akisimama hapa ni kilio.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nazungumza kwa uchungu kwa fedha za wananchi ambazo zinaliwa na si kwamba hazionekani, inajulikana kabisa.

Nakumbuka Halmashauri ya Longido tulipangiwa au tuliomba bajeti Sh bilioni 11; ni Sh bilioni 4 tu pamoja na mishahara… hakuna fedha za maendeleo… Tunazungumza kila siku, tunaondoka hapa hakuna kinachofanyika. Leo watuambie kwa hili wasinyamaze kama miaka mingine watujibu. Kwanini mnalipa mishahara hewa hadi leo?