Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mtwara

Watu 23 wamejeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi la Shule ya Msingi Salem baada ya kugongana na gari la Jeshi la Wananchi (JWTZ) katika eneo la Migomigo Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.

Ajali hiyo imetokea Novemba 28, 2024, saa 1 jioni katika eneo hilo la Migomigo barabara ya kutokea wilayani Newala mkoani humo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara ya Ligula, Zawadi Bwanali amethibitisha kuwapokea majeruhi hao ambapo kati ya hao wanafunzi ni 20, walimu wawili na dereva mmoja.

Amesema majeruhi wameanza kupokelewa hospitalini hapo majira ya saa 1, usiku na kuanza kupatiwa matibabu ambapo mmoja kati ya wanafunzi hao alihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini kwa ajili ya matibabu zaidi.

“Niwatoe hofu wananchi a wengi tumeshawafanyia uchunguzi na wengi hawana shinda kwani wengine wamepata michubuko midogo midogo na wale wengine ambao walichanika tumewashona na hali zao zimeendelea kuimarika na wengine tumewaruhusu.’ alisema.

Aidha ajili hiyo imetokea wakati wanafunzi hao alipokuwa wakitokea uwanja wa ndege mkoani humo kwa ajili ya ziara ya kimasomo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara SACP Issa Suleiman amesema ajali hiyo imehusisha basi hilo la shule ya msingi ya Salem na gari la jeshi aina ya lori katika eneo hilo la Migomigo na uchunguzi wa ajali hiyo bado unaendelea ili kubaini chanzo cha ajali.