Gari la Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linadaiwa kuua dereva wa pikipiki, Cosmas Swai (42), kwa kumkanyaga kichwani akiwa amembeba mkewe, Anna Swai (39) pamoja na mwanawe, David Swai (11).

Ajali hiyo imetokea Machi 12, mwaka huu, eneo la Segerea Mbuyuni, baada ya mashuhuda wa ajali hiyo kudai kuwa gari hilo la Polisi ‘lilitanua’ njia (kupita kando ya barabara) na kwenda kuvaana na pikipiki hiyo ‘uso kwa uso’.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Zuberi Chambela, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa masuala hayo hutolewa taarifa na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, lakini pia, suala hilo lipo chini ya uchunguzi wa Jeshi la Polisi.

 

“Siwezi kuzungumzia hilo kwa kuwa Jeshi la Polisi tumekuwa na utaratibu wetu wa kutoa taarifa, mamlaka ya kutoa taarifa kuhusu masuala ya aina hiyo yako chini ya Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Afande Mambosasa. Mtafute yeye, ama anaweza kulizungumzia ama atoe maelekezo kwangu nizungumze, lakini pia Polisi tumejiwekea utaratibu wa kuzungumza kuhusu masuala ambayo upelelezi wake unaendelea,” amesema Kamanda Chambela.

Katika mazungumzo yake na Gazeti la JAMHURI, Mambosasa alisema: “Bado taarifa hizo hazijanifikia hadi sasa (Jumamosi iliyopita jioni – Machi 16, 2019). Lakini nitamuagiza RPC Ilala anipatie taarifa hizo.”

 

Akizungumzia tukio hilo nyumbani kwake Kinyerezi – Kituo Kipya ambako ndiko shughuli za msiba wa mumewe zilifanyika, mjane wa marehemu Cosmas, Anna, aliyekuwa abiria kwenye pikipiki hiyo amesema siku ya Jumanne, Machi 12, 2019 majira ya jioni mwanawe, David, aliugua ghafla na alilazimika kumuwahisha Hospitali ya Segerea kwa ajili ya matibabu na baada ya matibabu ya awali, alimtaarifu mumewe awafuate hospitalini hapo kwa ajili ya kuwarudisha nyumbani.

“Mume wangu alifika akiwa na pikipiki na kutuchukua kwa ajili ya kurudi nyumbani. Wakati tunapandisha kilima cha Segerea Mbuyuni, mbele yetu niliona Defender (gari la Polisi) likiwa linakuja upande wetu kwa kasi. Nikamwambia mumwe wangu umeona hilo gari…mara baada ya kutamka hayo nilisikia tu nimetupwa mbali, nilipoinuka nilimwona mume wangu chini ya gari katikati ya tairi la mbele ya gari na lile la nyuma, tairi la mbele likiwa limekwishamkanyaga kichwa, alikuwa amevaa kofia ngumu kwa hiyo kichwa hakikuharibika isipokuwa ile kofia ilipasuka, mwanangu naye alitupwa mbali,” alidai mama huyo wa watoto wawili, akifafanua kuwa ‘Defender’ hiyo ya Polisi ilikuwa ya rangi ya maziwa (cream).

 

Gazeti hili likiwa limeshuhudia majeraha ya mama huyo maeneo ya uso wakati akielezea tukio hilo, anasema alikimbizwa hospitalini pamoja na mwanawe kwa ajili ya matibabu, na baada ya kutibiwa aliruhusiwa kurejea nyumbani lakini mtoto wake alikimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI) kwa ajili ya huduma zaidi za matibabu.

Alisema usiku wa tukio hilo, alipigiwa simu na kuelezwa kuwa fedha zinahitajika kwa ajili ya matibabu ya mwanawe, kiasi cha shilingi 150,000 ili afanyiwe vipimo vya uchunguzi wa kichwa (CT – Scan), na kisha alipe shilingi nyingine 200,000 kwa ajili ya mwanawe huyo kufanyiwa upasuaji.

 

“Kwanza mume wangu ndiyo amefariki dunia, mwili uko mochwari, mwanangu yuko Muhimbili hali yake mbaya, natakiwa kulipa fedha ambazo sikuwa nazo, lakini maisha ya mtoto wangu ni muhimu. Nililazimika kukopa fedha shilingi 200,000 kutoka kikundi chetu cha kupeana mikopo (VICOBA),” ameeleza.

Anasema tangu kutokea kwa tukio hilo, Jeshi la Polisi lilimfanyia mahojiano mara mbili, lakini akilalamika kuwa mahojiano hayo yamekuwa yakifanywa kwa ukali katika tafsiri inayoweza kuonekana kuwa yeye ni mtuhumiwa, badala ya shuhuda wa tukio hilo anayehitaji msaada wa Jeshi la Polisi.

 

“Wamekuwa wakiniita Kituo cha Stakishari bila kujali hali yangu ya maumivu mwilini kutokana na majeraha lakini pia kufiwa na mume wangu, pamoja na kumuuguza mwanangu,” analalamika.

Siku tano baada ya kutokea kwa ajali hiyo mama huyo amekuwa akiishi katika wakati mgumu kwa kukabiliwa na msiba wa mumewe nyumbani lakini mwanawe kuwamo katika hali ya kupigania maisha yake, huku gazeti hili likiwa limeshuhudia mtoto huyo akiwa na jeraha kubwa kuanzia katikati ya paji la uso kuelekea nyuma katikati ya kichwa, kisha hadi upande wa sikio la kulia, ikielezwa kuwa amepasuka fuvu la kichwa.

“Katika ajali ile mimi sikupoteza fahamu, nilishuhudia yote. Polisi wamenihoji mara mbili, nimewaeleza niliyoona. Sijui hali ya mwanangu ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kinyerezi, nimeshindwa kwenda kumwona kwa kuwa hapa nipo msibani, nimefiwa, nashindwa kumuuguza, kulala naye hospitalini,” amesema.

 

Taarifa za awali za uchunguzi wa mwili wa marehemu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili zimeeleza kuwa sababu za Cosmas kufariki dunia ni kutokana na kuumia sana kichwa (Severe Traumatic Brain Injury – TBI).

Marehemu huyo alisafirishwa Machi 15, 2019 kwenda kwao Masama, Moshi – Kilimanjaro kwa ajili ya maziko, mkewe akilazimika kusafiri kwenda kumzika mumewe na mwanawe anayeendelea na matibabu MOI akihudumiwa na mmoja wa mashemeji wa mke huyo wa marehemu.

 

Mdogo wa marehemu Cosmas, aliyejitambulisha kwa jina la Vincent Swai, alisema asubuhi ya siku ya tukio alikutana na kaka yake huyo ambaye alimwagiza jioni (siku ya tukio) wakutane kwa ajili ya mazungumzo ambaye alimsisitiza kuwa ni muhimu lakini kinyume chake, jioni hiyo alipokea taarifa za msiba wa kaka yake huyo.

Naye alilalamikia ushirikiano mdogo kutoka kwa Jeshi la Polisi Kituo cha Stakishari ambako ndiko tukio hilo linaendelea kufanyiwa upelelezi.

 

“Jeshi la Polisi limeshindwa kutambua hali yetu ya majonzi, walituahidi kutupatia rambirambi lakini hadi tunaanza safari ya kusafirisha mwili wa ndugu yetu hawajatupatia chochote hata jeneza, hili si kitu sana, kinachouma zaidi ni hali ya kutuchukulia kama watu wasumbufu pale tunapotaka kuhoji zaidi kuhusu hatima ya suala hili,” amesema.

Baadhi ya waendesha ‘bodaboda’ wa kituo cha pikipiki Segerea Mbuyuni, ambao waliusindikiza mwili wa mwenzao huyo kwa msafara mkubwa wa bodadoda kutoka eneo la Jangwani jirani na Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako mwili huo ulikuwa umehifadhiwa hadi Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Segerea Mbuyuni, waliomba haki itendeke kwa mwenzao huyo.