*Limenunuliwa kwa Sh milioni 180
*Lilipokatiwa bima nyaraka inaonyesha
limenunuliwa kwa Sh milioni 70
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Gari analolitumia Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) Taifa, Rashid Mtima, kwa ajili ya shughuli za ofisi yake lenye namba za usajili T 327 DPP limegubikwa na utata mpya baada ya bima yake iliyokatwa kwa mara ya kwanza kuonyesha limenunuliwa kwa Sh milioni 70 badala ya Sh milioni 180.
Gari hilo ambalo ni mtumba (used) huku mchakato wa ununuzi wake nao ukiwa umegubikwa na utata, limenunuliwa Desemba 24, 2018 baada ya Talgwu kulipa malipo ya awamu ya kwanza (Sh milioni 40) na wakakabidhiwa Januari 2, 2019 na muuzaji ambaye ni Dar es Salaam Motors and Commission Agent Ltd, aliyepo makutano ya Mtaa wa Swahili na Barabara ya Morogoro eneo la Fire jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa nyaraka ya Januari 3, 2019 ambayo ni ankara ya malipo ya fedha baada ya kupatiwa huduma ya bima mseto au bima kubwa (Gazeti la JAMHURI lina nakala ya kivuli chake) kutoka Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) kwenda Talgwu inaonyesha namba za usajili wa gari hilo ambazo ni T 327 DPP, aina yake ambayo ni Toyota na thamani yake ambayo ni Sh milioni 70.
Pia nyaraka hiyo yenye namba ZIC/2018 inaonyesha kiwango cha asilimia 3.5 kinachotakiwa kukatwa kutoka katika thamani ya gari hilo ambayo ni Sh milioni 70, inaonyesha Sh 2,450,000 ya tozo ya bima iliyopatikana kutokana na asilimia hiyo, inaonyesha Sh 2,205,000 iliyopatikana baada ya punguzo la asilimia 10.
Vilevile inaonyesha Sh 396,900 ambayo ni asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na jumla kuu ya fedha zote za tozo ya bima ambayo Talgwu walitakiwa kulipa wakati huo baada ya majumuisho yote ni Sh 2,601,900.
ZIC yaahidi kutoa ufafanuzi
Kutokana na utata mpya wa kununuliwa kwa Sh milioni 180 lakini katika nyaraka za bima kuonyesha lina thamani ya Sh milioni 70, Juni 3, 2022 JAMHURI liliwasiliana na ofisa mmoja wa ZIC kwa njia ya simu (hakutaka jina lake liandikwe gazetini) akasema Talgwu ndio waliofanya kosa kwa kutoa taarifa za uongo za thamani halisi ya gari hilo.
“Wao Talgwu ndio wanaojua kwa nini wametoa taarifa za uongo. Kwa kawaida sisi tunakatia gari bima kutokana na thamani yake kwa wakati huo baada ya kuletewa na mteja,” amesema ofisa huyo.
Pia Juni 3, 2022, JAMHURI liliwasiliana na Meneja wa ZIC Tawi la Lumumba jijini Dar es Salaam ambako bima ya gari hilo ilikatiwa, Majda Ahmed, kwa njia ya simu baada ya kumkosa ofisini kwake na akasema hawezi kuzungumza chochote kuhusu utata wa thamani ya gari hilo hadi aangalie nyaraka zake.
Katika hatua nyingine, Juni 3, 2022, JAMHURI liliwasiliana kwa njia ya simu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa ZIC, Arafat A. Haji, na akaahidi kutoa ufafanuzi wa taarifa ya utata wa thamani ya gari hilo hadi wakalikatia bima.
“Kwa muda huu niko nje ya ofisi nimeshatoka na sasa hivi (Ijumaa) niko katika kikao kingine, naomba nitumie namba ya usajili wa hilo gari halafu kesho (Jumamosi) nitampa ofisa wangu mmoja anitafutie faili lake kisha tuwasiliane saa nne asubuhi nitakupa taarifa zote.
“Kuna wateja wengine wanatoa thamani kubwa ya magari yao ili yanapopata ajali aweze kulipwa kiasi kikubwa cha fedha na kuna wengine wanatoa thamani ndogo ya magari yao ili ile tozo ya bima watoe kiasi kidogo cha fedha lakini tuwasiliane kesho (Jumamosi),” amesema Arafat.
Kesho yake Juni 4, 2022, JAMHURI liliwasiliana na Arafat lakini akasema pia hakuwapo ofisini kwa wakati huo na ofisa wake naye hayupo.
“Unajua mimi niko Zanzibar na faili la hilo gari liko Dar es Salaam. Kwa hiyo nakuomba Jumatatu (jana) tuwasiliane asubuhi mapema ili nikupe ofisa wangu mmoja aliyepo Dar es Salaam ili akusaidie kukupa taarifa ya gari hilo,” amesema Arafat.
TIRA yang’aka
Juni 3, 2022 akizungumza kwa njia ya simu na JAMHURI, Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Oyuke Phostine, amesema ni kosa kisheria kwa mteja kutoa taarifa za uongo kuhusu thamani ya gari au kitu chochote kile pindi anapokwenda kupatiwa huduma ya bima.
Amesema na endapo ikigundulika hivyo, adhabu yake kwa mteja wa gari hilo au kitu hicho ni kufutiwa bima yake kwa kuwa inakuwa si halali kutokana na kushindwa kusema ukweli.
“Kama ikigundulika hivyo, basi hiyo bima si halali kwa sababu katika taratibu za bima wakati wa kulipa inabidi useme ukweli ulio halisi usiokuwa na matendo au chembe ya uongo wowote ndani yake, yaani hapa hakuna kuongopa hata kidogo,” amesema Phostine na kuongeza:
“Na ukweli unakuwa katika pande zote mbili, yaani upande wa kampuni ya bima inapotakiwa kumpatia mteja bima lazima iseme mimi nina hii na nitakupa kwa gharama hii.
“Na itakukinga dhidi ya majanga fulani, vivyo hivyo kwa mteja naye anapokwenda kukata bima ni lazima aseme kila kitu kinachohusika katika jambo lake au kitu chake kwa ukweli wake.”
Kuhusu gari la Talgwu kuwa na thamani ya Sh milioni 180 lakini lilipokatiwa bima linaonekana lina thamani ya Sh milioni 70, amesema maana yake ni kwamba bima hiyo si halali machoni kwa mkataba wa bima.
Pia amesema ikigundulika hivyo mkataba huo wa bima unakufa hapo hapo kwa sababu kampuni za bima zinafanya kazi kwa kuhakikisha kuna ukweli kwa pande zote mbili na ukweli usipokuwapo maana yake sera za bima hazifanyi kazi.
“Kwa hiyo kama gari lina thamani ya Sh milioni 180 halafu wewe ukaweka thamani yake ni Sh milioni 70 na ikigundulika si thamani halisi, maana yake utakuwa haujakingwa pindi janga linapotokea na hata ukigonga gari la mtu mwingine nalo litakuwa halijakingwa,” amesema Phostine.
Katika hatua nyingine, amesema kampuni ya bima ina wajibu wa kuchunguza na kujiridhisha kuhusu thamani ya gari kwa bei ya sokoni kwa wakati huo kabla ya kutoa huduma ya bima kwa wateja wao.
Zabuni kutotangazwa
Licha ya gari hilo kugubikwa na utata mpya wa thamani ya bei yake kutofautiana na ile iliyopo katika nyaraka ya bima kutoka ZIC, lakini pia hivi karibuni JAMHURI limeripoti jinsi mchakato wa ununuzi wake nao ulivyogubikwa na utata baada ya taratibu za zabuni kutofuatwa kama kanuni mbalimbali za Talgwu toleo la mwaka 2018 zinavyoelekeza.
Taarifa ambazo JAMHURI limezipata hivi karibuni kutoka chanzo chake cha kuaminika kilichopo ndani ya Talgwu kimesema kati ya mwaka 2017 na 2018, ofisi ya katibu mkuu ilipeleka maombi kwa Baraza Kuu Taifa la Talgwu ya kununua gari jipya lililoanza kutengenezwa kuanzia mwaka 2015 kwa ajili ya matumizi ya ofisi yake na akaidhinishiwa Sh milioni 100.
Chanzo hicho kimesema baada ya kutafuta gari na kulikosa kutokana na cheo chake, Mtima, anadaiwa kujiongezea fedha nyingine Sh milioni 80 kwa ajili ya kununua gari lenye thamani ya Sh milioni 180, na hatua hiyo ni kinyume cha kanuni zao, kwa sababu hakupeleka maombi mapya kwa Baraza Kuu Taifa la Talgwu kama inavyotakiwa.
Pamoja na kudaiwa kujiongezea fedha hizo kimakosa, chanzo hicho kimesema Ofisa Ugavi na Ununuzi wa Talgwu, Brigither Emmanuel, akamshauri Mtima kuhusu ununuzi wa gari jipya lenye thamani hiyo kupitia barua yake aliyomwandikia Desemba 17, 2019.
Baada ya makubaliano hayo kufanyika, chanzo hicho kimesema Talgwu wakafanya malipo ya gari hilo kwa awamu tano (JAMHURI lina kivuli cha nakala za mkataba wa malipo); Desemba 24, 2018 wamelipa Sh milioni 40, Januari 30, 2019 wamelipa Sh milioni 35, Februari 28, 2019 wamelipa Sh milioni 35, Machi 29, 2019 wamelipa Sh milioni 35 na Aprili 30, 2019 wamelipa Sh milioni 35.
Kasoro za gari zabainika
Baada ya malipo hayo kuanza ndipo utata na kasoro zikaibuka kutokana na gari hilo kuwa na kadi mbili (JAMHURI lina nakala za vivuli vya kadi) kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilizotolewa na ofisa wake mmoja mwenye namba 20000269 ya kitambulisho chake wakati wa mchakato wa usajili wake.
Kadi ya kwanza ya gari hilo iliyotolewa na TRA katika ofisi zake zilizopo Mtaa wa Samora, Dar es Salaam na kuthibitishwa Januari 3, 2019 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive inaonyesha gari hilo lenye namba za usajili T 327 DPP aina ya Toyota Land Cruiser V8 lilitengenezwa mwaka 2015, ikiwa na maana kwamba limeingizwa hapa nchini miaka minne kabla hawajalinunua rasmi mwaka 2018, huku mmiliki wake akiwa ni Talgwu nalo ni kosa kwa sababu gari hilo halikuagizwa nje ya nchi na chama hicho bali liliagizwa na muuzaji na ndiye katika kadi alipaswa awe ndiye mmiliki wa kwanza na aliyenunua alitakiwa aonekane umiliki wake umehamishwa kutoka kwa muuzaji huyo.
Januari 23, 2019, Ofisa Utumishi wa Talgwu, Cassian Mbunda, akamwandikia barua muuzaji baada ya kubaini kasoro za gari hilo.
Mtima ajibu
Mei 14, 2022, JAMHURI lilizungumza na Mtima kwa njia ya simu yake ya mkononi na kumtaka mwandishi wa habari hii kwenda ofisini kwake kwa ajili ya kupata majibu yote.
“Gari limenunuliwa tangu mwaka 2019 hadi leo hayo mambo ya kadi yanatoka wapi? Ionekane lina kadi mbili? Wewe njoo ofisini nitakupa majibu, siwezi kuongea mambo ya kirafiki halafu unanimaliza, sina muda huo,” amesema.
Mei 16, 2022 JAMHURI lilifika ofisi za Talgwu na kuzungumza na Mtima, pamoja na mambo mengine amesema kuhusu gari analolitumia kuwa na kadi mbili na licha ya kumhakikishia mwandishi wa habari hii kwamba akienda ofisini kwake atamuonyesha lakini hakumuonyesha kama alivyoahidi, kisha naye akahoji kuhusu hizo kadi.
“Sasa kadi mbili kivipi? Kwamba kuna kadi ya kwangu halafu kuna kadi ya Talgwu?” amehoji.
Amekiri kwamba gari hilo wamelinunua kwa Sh milioni 180 baada ya kwanza kutenga Sh milioni 100 na haikutosha kutokana na bei za sokoni kisha wakaongeza Sh milioni 80.
“Tulilikosa kwa bei hiyo na tukarudisha katika vikao tukaongezewa fedha kisha tukaenda kununua hilo gari,” amesema.
Pia amesema hakumbuki kuhusu suala la kadi kuwa hivyo, kwa kuwa hata mchakato wote wa ununuzi wa gari hilo hajausimamia yeye bali alisimamia msaidizi wake, kwa sababu wakati huo alikuwa anasafiri mara kwa mara.
“Ninachojua kadi ni moja tu na wamechukua Takukuru. Kwa hiyo kama kuna kadi mbili sikumbuki kabisa na kama ni kweli, basi hata TRA nao wana vitendo vya rushwa,” amesema.
Kuhusu gari hili kuwa la mtumba licha ya ofisi yake kuomba kwa Baraza Kuu Taifa la Talgwu kununua jipya amesema ununuzi wake umefuata taratibu kwa sababu wao si serikali kwamba lazima wanunue magari mapya.
“Sisi si serikali, kwa hiyo si lazima kununua magari mapya, utaratibu huo nimeukuta hivyo na Talgwu haijawahi kununua magari mapya, nimeurithi na kanuni hazitulazimishi kufanya hivyo ndiyo maana naendelea nao,” amesema.
Mjumbe wa Kamati Tendaji Taifa
(KUT) ya Talgwu afunguka
Juni 4, 2022 JAMHURI limefanya mahojiano na mjumbe wa KUT (jina limehifadhiwa) na amedai Mtima ni mbinafsi na muongo na anajisifu kuwa ameinyanyua Talgwu katika kipindi chake lakini ukweli ni kwamba hawezi kujilinganisha na makatibu wakuu wenzake waliopita waliokuwa na uwezo mkubwa wa uongozi.
“Kikao chetu cha hivi karibuni pale Dodoma tulipanga tumsimamishe, hapeleki fedha za kuendesha chama matawini, akipeleka ni nusu au hakuna kabisa, ila katika ununuzi kama wa magari, sare za Mei Mosi na mengineyo huwezi kuona fedha zimekosekana kwa kuwa ndiko kwenye ubadhirifu,” amesema.