Wiki iliyopita katika sehemu ya 8 hadithi hii iliishia katika aya inayosema: “Shahidi wa pili alikuwa Bibi Judith mwenyewe. Aliieleza mahakama jinsi siku moja walivyokuja jamaa watatu. Mmoja alikuwa Mzungu, mwingine Mwarabu na wa mwisho alikuwa mtu mweusi Mwafrika. Watu hawa alidai mama huyu kuwa eti walimuomba ajiunge katika shughuli zao za kichawi. Lakini mama huyu eti alikataa kata kata. Hata hivyo watu hawa waliendelea kuja na kumbembeleza kwa siku kadhaa. Maudhi ya watu hawa yalipozidi aliamua kukubali. Akajiunga!” Endelea…
Kwa vile alikuwa mshiriki wa dini, ilibidi aendelee navyo vyote. Akawa anasali na huku anahudhuria vikao vya wachawi. Baadaye alichaguliwa awe mwenyekiti wa waovu hawa. Baadaye shughuli ilipopea alikuwa amefikia uwezo wa kuwatoa nyongo mamba wakiwa wazima.
Vilevile akawa mpikaji wa vitoto vya fisi na akawa mkaangaji wa vitovu vya watoto. Hata hivyo kwenye dini mama huyu alionekana safi kwa vile shughuli zake zilifanyika usiku na zilionekana kwa wajuaji tu.
Shahidi wa tatu alikuwa mchungaji wa ng’ombe na alikuwa jirani tu na Mama Judith. Yeye aliiambia mahakama kuwa siku moja alipokuwa anakamua ng’ombe wake, Bibi Judith alipita karibu na zizi lake la ng’ombe. Alishangaa kuwaona ng’ombe wote wamemkazia macho mama huyu alipokuwa anapita. Kwa kweli wale ng’ombe walionyesha wazi kuwa walikuwa wamemwogopa mama huyu!
Kesho yake asubuhi alikuta ng’ombe watano wamekufa. Wale waliobaki zizini walionekana kuwa wana wasiwasi kwelikweli na huku manyoya ya miili yao yamesimama na masikio yao yalidhihirisha kuwa kuna dosari fulani. Mnamo saa 7:00 mchana, wakafa ng’ombe watatu na jioni hiyo wakafa tena ng’ombe wanne. Kulipokucha asubuhi yake, kundi zima likawa limeteketea.
Hali hii ilimfanya shahidi aachane na mambo ya dini akaenda kwa fundi mmoja mahiri kwa lengo la kujua asili ya ng’ombe wake kuteketea ghafla. Aliambiwa kuwa dawa ni kwenda kuyakata masikio ya ng’ombe wawili wakubwa waliokufa kisha unayakojolea mkojo na kuyaweka kwenye moto ulioandaliwa. Aliyetenda jambo hili atakuja mwenyewe kuomba msamaha.
Mfugaji huyu alifanya kama alivyoelekezwa na fundi. Alishangaa kumwona Bibi Judith, huyu mama wa Kizungu akija mbio mbio huku akilalamikia maumivu ya kichwa na kuomba msamaha.
Baadaye yule mfugaji aliyatoa masikio hayo motoni na Bibi Judith akaacha kulalamika. Shahidi aliendelea kudai kuwa eti aliogopa kuchukua hatua zaidi akichelea uchawi wa bibi huyu usije ukamwangamiza yeye mwenyewe.
Shahidi wa nne alikuwa ni jirani mfanyakazi kwenye mji fulani. Yeye alidai kuwa siku moja huyu mama alikuja nyumbani kwao kuomba chumvi. Kwa bahati mbaya kukawa na kutoelewana baina yao. Kwa ghadhabu yule mama aliondoka na kusema eti kiburi cha shahidi kitamgharimu na atakiona cha mtemakuni.
Usiku ule, ulipokuwa usiku wa manane, bibi huyu alikuja akiwa na babu mwingine wa Kizungu, Kiarabu na babu mwingine Mwafrika kama sisi. Walimwamuru awafuate, akakataa. Wote wanne walitaka kumchukua kwa nguvu, lakini yeye alipiga kelele na watu wa nyumbani hapo wote wakaamka na kutaka kushuhudia kulikoni!
Bahati mbaya hawakuona kitu chochote kisicho cha kawaida. Ila tu walimwona binti huyu akijaribu kujinasua kutoka kitu fulani ambacho wao hawakuwa wanakiona. Hatimaye Bibi Judith na wenzake waliondoka na ndipo yule msichana akaelezea kisa chote. Alikuwa anatokwa jasho kutokana na harakati za kujiokoa kutoka kwa wale wachawi.
Siku ya pili msichana huyu aliendelea kuielezea mahakama kuwa kwa kuhofia kuwa mama huyu na genge lake wangerudi tena, alichukua kisu kikali akakikojolea mkojo na kisha akakifutika chini ya mto wake. Na kweli lile genge walirudi tena. Katika kujitetea msichana huyu alidai kuwa alifanikiwa kumchoma kisu bibi huyu kwenye paja lake la kulia.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu aliamuru Bibi Judith akaguliwe kama kweli maelezo ya yule dada yalikuwa ni ya kweli au ni kumpakazia tu huyu mama wa Kizungu! Ni kweli yule mama alikuwa na jeraha jipya na yumkini lilimtokea usiku huo.
Kutokana na maelezo hayo, hakimu alitoa amri kuwa huyu mama arudi kwao mara moja kwa vile alikuwa hafai katika jamii yetu. Na baada ya hukumu hiyo yule mama wa Kizungu alitolewa kizimbani akapelekwa kwingine ambako mimi sikujua ni wapi.
Bulongo, ndugu yangu! Ninapenda niendelee kukusimulia mambo haya yasiyo ya kawaida, lakini kwa sasa ninadhani utagundua kwa nini nilianza kwa kukutahadharisha kuwa utakachosoma usimwambie mtu yeyote mambo haya.
Nyamaza kama maji kwenye mtungi. Mimi niliamua kuendelea na safari yangu ya kurudi nyumbani. Kwa hakika nilikuwa sijui ninakoelekea; basi ni kusafiri tu, tena kwa mguu wala kwa hakika sikumbuki kama nilikuwa ninafika mahala fulani ninachoka kwa maana ya kuchoka kikweli kweli, bila shaka yalikuwa mazingira ya huko Gamboshi.
Rafiki yangu Bulongo, maadamu nimeamua kukuelezea mambo haya ni afadhali niendelee tu kukuelezea kuliko nikiishia hapa. Waswahili husema: “Maji ukiyavulia nguo sharti uyaoge”. Sasa kama unavyofahamu mimi sikuwako nyumbani kwa miaka takriban mitatu. Sasa nilikuwa wapi?
Hapa nitajaribu kukuelezea baadhi ya mambo yaliyonifika katika kufa/kuzimia kwangu. Mengine yataonekana kama hadithi za abunuwasi, lakini mpendwa wangu ni ukweli mtupu. Niliyaona kwa hakika!
Siku moja yalinitokea mambo ya ajabu sana. Katika matembezi yangu nikitafuta njia ya kurudi nyumbani. Nilipokuwa ninatembea, ghafla nilianguka chini. Nikaamka haraka haraka na nikawa ninatetemeka huku macho yamenitoka pima. Nikaanza kukimbia kuelekea kusikojulikana.
Baadaye nilianza kukutana na watu na nikawa ninawaogopa sana. Niliendelea kukimbia hadi kwenye mbuyu mmoja. Lo! Jamani ule mbuyu ulikuwa unatoa upepo mwanana na hapo nikatulia kidogo. Nilibaki kuushangaa ule mti hadi nikapitiwa usingizi.
Ghafla nilisikia mtu akiita kwa ukali “wewe! Amka”. Dooh! Kufumbua macho nikamwona bibi kizee. Alinifanyia ishara fulani nami nikaanza kumfuata bila ya utashi wangu. Moyo ulikuwa na hofu, lakini sikuweza kusema lolote mbele yake. Baada ya muda wa kama dakika kumi hivi, yule bibi alitoweka na kuniacha nikishangaa mitaani humo.
Muda huo ulikuwa jioni na kuelekea usiku! Nilitafuta mahali pa kulala na kwa bahati nzuri nilimpata baba mmoja akanichukua hadi kwake. Alinionyesha sehemu ya kulala, lakini nilipoingia chumbani sikuamini macho yangu!
Kitandani nilikoelekezwa nitalala kulikuwa na joka kubwa limejizungusha na godoro lilikuwa ni mamba. Pembeni mwa kitanda kulikuwa na fisi wengi wakiniangalia kwa hamu na baadhi yao wakitabasamu.
Maskini weee! Nilitaka niondoke haraka, kujaribu kufungua mlango haukufunguka, nikajisogeza pembeni mbali kidogo na kile kitanda. Ghafla nikasikia sauti nyororo masikioni mwangu, ilikuwa sauti ya mrembo na hata wewe rafiki yangu Bulongo ungeisikia bila shaka ungeitamani uisikilize. Moyo wangu ukajaa shauku ya kutaka kumuona mtoa sauti hiyo. Ile sauti ikaendelea: “Mmh! Leo kuna mgeni chumbani kwangu”.
Je, unafahamu nini kiliendelea chumbani baada ya sauti hiyo? Usikose sehemu ya 10 yenye kusimulia mambo mazito kuhusu Gamboshi. Mtunzi wa hadithi hii ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI na anapatikana kwa simu Na. 0755629650.