Wiki iliyopita katika sehemu ya nne hadithi hii iliishia katika aya inayosema: “Akina mwewe pia walikuwepo wananyakua matambara kwa fujo kisha wanalia Zwi! Zululu! Ndege wengine wadogo walikuwa wanaruka juu juu na baadhi yao walikuwa wanaruka chini chini. Bata mzinga nao pia walikuwa wanahimiza wakisema mrudisheni mtoto wetu jamani, mrudisheni kwani amepotea na tunamtafuta.” Je, unafahamu nini kinafuata? Endelea…
Bulongo, ndoto hii ilikuwa nzuri mno. Kwani nilijiona kuwa kumbe na mimi ni mtu mbele ya watu. Kwani hata ndege walichangia katika kurudi kwangu. Katika dunia hii, uhalisia wa ndoto yangu ni kuwa kulikuwa na jitihada za kila aina za kutaka nirudishwe katika dunia hii na ni watu wachache sana ambao wanatambua kwa yakini baada ya kifo ni nini!
Kwa hiyo yule Bibi Kifimbo alikuwa amewahi kunichukua, lakini wale wenzake walikuwa hawataki. Ila ndiyo nikawa naonyeshwa maraha ya peponi, kule hakuna kula kama hapa duniani.
“Je, ungependa na wewe uende huko? Ni pazuri sana, masharti yake ya kwenda huko mpaka ufe kwanza. Je, unaogopa kufa? Basi ukiogopa kufa jua kuwa utachelewa kwenda Gamboshi kwenye maraha. Je, uko tayari kufa sasa ili ukaonje maraha ya Gamboshi? Ambako hata watoto wadogo si wa kubeza! Ni wazito na wanaweza kukufanyia maajabu hadi ukabloo! Kuna akina bibi wanaotembelea makalio.” Akamaliza kufafanua yule mama kisha akaendelea:
“Ndiyo ninajua kuwa akili yako ya dunia hii inapata ukakasi kuamini maneno haya. Lakini maneno haya ni kweli kabisa na mimi asilani sijawahi kusema uongo popote. Niseme uongo ili nipate nini?” akamalizia. Aliniangalia kana kwamba anataka kuendelea na simulizi zake za ajabu. “Mathalani, hata kwenye dunia yenu hadi leo kuna miti na vitu kadha wa kadha huwa vinazungumza.”
Akanikazia macho kisha akaendelea: “Unakumbuka wakati wa ujenzi wa barabara ya kwenda Pwani kupitia Hinyanga ule mkuyu ulioko karibu na soko, karibu na kale kamto uligoma kukatwa ukidai kuwa wakazi wake wangeenda wapi kwani wamekuwepo hapo kwa maelfu ya miaka, kwa hiyo ulikataa kukatwa na upo hadi leo au huujui?
“Je, ule mkuyu wa kule Bupandansi ambao pia uliwagomea wahandisi kwa sababu wenyewe ni maskani ya watu?” Akatabasamu kidogo kisha akaniangalia tena na kuendelea na simulizi zake hizi za maajabu ya Gamboshi.
“Je, unakafahamu kale kabibi kizee kale kanaitwa Bibi Fisi. Kalikokuwa kanakaa karibu na hospitali kuu? Eti wale mipango miji wakawa wamepanga kupitisha barabara ya mtaa nyumba yake! Kaliwanyamazia tu na vituko vikaanza pale walipokuja na greda lao eti kuchonga barabara.
“Kwa mshtuko greda lilipofika kwenye viwanja vya kale kazee likazimika. Walimwita fundi mkuu wa greda kuangalia hitilafu ya greda hakuona chochote. Walipoliwasha kwa lengo la kurudi nyumbani liliwaka, lakini walipotaka kuendelea mbele na mradi wao wa uchongaji, greda liligoma mara moja likazimika. Kumbe!” Yule bibi aliendelea kueleza.
“Nguvu za yule bibi zilifanya lile greda ligome kwenda mbele. Dereva alipoulizwa sababu ya kushindwa kuliendesha alidai eti wakati mwingine alikuwa anaona majabali mbele yake yamening’inia ungedhani yatamdondokea. Kwa hiyo aliogopa kuendesha greda mbele asije akapondwa na mawe.
“Hivi ndivyo nyumba ya Bibi Fisi ilivyoendelea kuwapo hadi alipofariki dunia ndipo watu wa mipango miji wakaja kupitisha barabara ya mtaa sehemu hiyo. Lakini inadaiwa eti hadi leo watu wanaokaa maeneo hayo huwa hawaishi kuona maluweluwe kwa sababu ya nguvu za yule Bibi Fisi.”
Baadaye nilimwacha bibi kizee huyu na kuendelea na safari yangu ya kurudi nyumbani. Nilivuka mbuga, milima na baadaye nikajikuta ninatembea juu ya maji. Kwa hakika jambo hili la kutembea juu ya maji lilinirusha roho na nikawa na hofu kuwa labda nitazama nife maji, lakini jamani, nilivuka salama salimini nikajikuta niko kisiwani. Nilitembea juu ya maji mpaka ng’ambo ya pili kisiwani!
Mazingira ya kisiwani yalikuwa ya kawaida mpaka nilipofika sehemu ambayo ilikuwa na jiwe la ajabu. Jiwe hilo lilikuwa limekaa juu ya jabali na limekaa kama pia, ingawa halikuchongoka sana kama zilivyo pia; bali lilikuwa bapa hivi. Kule chini! Kwa kuliangalia kwa haraka haraka mwonekano wake uliashiria kuwa unaweza kulisukuma na likadondoka kwa urahisi!
Oh! Jamani, kwa mshangao lile jiwe lilianza kutingishika huku na huko. Niliogopa nikadhani labda tetemeko la ardhi limelikumba jiwe hili. Lakini kwa mshangao jiwe halikudondoka na likabakia hivyo hivyo linachezacheza kwa kufuata mapigo ya muziki. Akili iligoma kufanya kazi kwa kuona jiwe linacheza kama binadamu achezavyo muziki, mzuka ulikaa kichwani!
Nilichanganyikiwa na kujaa fadhaa. Sikuelewa kama nilichoona ni ndoto au uhalisia. Jamani nina uhakika nilichoona ni cha kweli kabisa. Nikiwa katika harakati za kutafuta njia ya kurudi nyumbani huku nimejaa mawazo makuu, nilianza kusikia kwa mbali sauti ya ndege.
Jamani ilikuwa sauti nzuri mno. Hamu ya kutaka kujua ndege huyu ni ndege gani ikanikolea, nikawa ninaangalia huku na huko. Mara nikamwona mwimbaji wangu umbali wa mita kama ishirini na tano hivi. Niliyafikicha macho yangu ili nimwone vizuri malenga wangu.
Alikuwa ameganda hewani, katulia kama helikopta. Nilikodoa macho kwa makini zaidi. Yule ndege rafiki yangu alikuwa amekaa hewani na anaimba kwa furaha huku akichezacheza, lakini ameelea angani! Wimbo wake niliusikiliza kwa makini nikabaini kuwa huenda ndege huyu alikuwa na matatizo, kwa hiyo alikuwa anajifariji kwa wimbo wake.
Alipobaini ya kuwa kuna mtu anamwangalia; kilitokea kitu kama mwanga mkali na mara yule ndege akatoweka. Nilishikwa butwaa nisijue la kufanya. Uchovu ulikuwa umenishika sehemu zote za mwili nikajikuta niko usingizini.
Sijui nililala muda gani, lakini nilipozinduka, nikajikuta nimo mikononi mwa jitu. Jitu hili lilikuwa ni litoto na lilifanana sana na viungo vyetu ila tu vya lenyewe vilikuwa vikubwa sana. Ni viungo vikubwa mno! Hakuna maelezo jitu hili lilionekana ni lipole sana, bali ukubwa wa mwili wake ulitisha ajabu. Kwa ujumla jitu hili lilikuwa na urefu kama kilometa mbili kwenda juu. Lakini ni litoto.
Lilinishika katika vidole vyake vya chanda na dole gumba likawa linaniangalia. Lilinisogeza karibu na macho yake na mara huko juu nikawa ninahisi baridi kweli kweli. Baadaye lilinitumbukiza kwenye mfuko wake wa shati na sikujua tena kilichokuwa kinaendelea. Nikiwa mfukoni mwa lile litoto niliweza kuona mawingu yakiwa chini yangu. Kumbe kwa juu huwa yanaonekana meupe kama pamba ya Wasukuma.
Baadaye lile litoto jamani, likanitoa mfukoni mwa shati lake likatandaza kiganja chake ambacho kilipata ukubwa wa viwanja vitatu vya mpira. Nikawa ninatembea kiganjani huku na huko angani juu! Wakati fulani litoto hili lilihema kwa nguvu na pumzi yake ikanipeperusha likawa linatabasamu likinionea huruma jinsi nilivyokuwa ninahangaika na kuonekana waziwazi nimeogopa.
Baadaye litoto hili lilinipeleka kwa mama yake. Huyu alikuwa mkubwa ajabu na urefu wake ulikosa maelezo, kwani ukitaka kuwaambia watu wa hapa kwetu kuwa alikuwa na urefu wa kufikia kilomita mia saba na ushei hivi, wasingekuelewa, ninaomba nisisitize tena kuwa yule mama alikuwa mkubwa mno! Mkubwa sana!
Lile limama lilinichukua likaniangalia kwa makini, likawa linasema: “Kanafanana nasi, umekapata wapi?” Lile litoto likasema: “Nimekaokota huko porini karibu na mpaka wa himaya yetu.” “Sasa unasemaje?” Lile limama likauliza tena, litoto nalo likajibu: “Kaache tu mama kaende. Nenda ukakaweke kule kwenye mpaka wanakoishi watu wadogo kama yeye.” Haya niliyaelewa kutokana na ule mtambo niliofungiwa na wale rafiki zangu, watu wadogo Msemakweli! Unawakumbuka?
Je, unafahamu nini kiliendelea baada ya hapo? Usikose sehemu ya sita yenye kusimulia mambo mazito kuhusu Gamboshi. Mtunzi wa hadithi hii ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI na anapatikana kwa Na. 0755629650.