Wiki iliyopita makala hii iliishia katika aya iliyosema: “Yule kizee aliyeniweka mlangoni alikuja akataka kunichukua tena anipeleke kusikojulikana. Nilikataa na akawa ananilazimisha nikubaliane naye. Hapana jamani, dunia ya Gamboshi ndiyo hasa ninayopenda kuishi, maisha ya maajabu ndiyo kipenzi cha roho yangu. Si unajua tena wahenga walisema kipenda roho kula nyama mbichi. Sasa huyu bibi ananipeleka wapi tena? Mimi ni Gamboshi tu!” Je, unafahamu nini kiliendelea? Soma sehemu ya pili…

Siku ya pili katika kuzimia/kufa kwangu huko Gamboshi mashindano yaliendelea tena. Siku hiyo kijana mmoja alikuja akiwa na upinde na mshale mmoja. Alikwenda kuwinda kwenye pori la Serengeti. Mara aliliona kundi la swala ishirini wametawanyika huku na huko kwenye eneo lipatalo ukubwa wa kiwanja cha mpira.

Kijana aliwanyemelea polepole na alipofika umbali wa mita mia moja hivi; akalenga shabaha swala dume aliyekuwa pembeni na mkubwa kupita wote akaachia mshale wake, chwaaa! Hakukosea!

Ulimdunga yule swala dume akaanza kupiga kelele na kulalama.

Kijana akakimbia mbio haraka akauchomoa ule mshale kwa yule swala dume akamwacha akipiga kelele kisha akaanguka, kijana akalenga tena na tena mpaka wote ishirini akawaua kwa huo mshale mmoja kabla hawajatokomea porini.

Aliwafunga wote kwenye mlindi akawabeba na kuwapeleka kijijini. Mimi nilitaka kumsaidia, lakini akanikataza akidai kuwa mimi nilikuwa bado ninanuka ubinadamu! Sikumwelewa! Eti ninanuka ubinadamu!

Baadaye mchana huyo kijana na dada yake mdogo walikwenda tena kwenye pori la Serengeti. Walimuona nyati mkubwa ajabu akiwa peke yake. Walimnyemelea polepole kisha yule kijana akalenga mshale wake na kuachia, chwaaa! Kwa wakati huo huo, dada mtu naye akafyatuka mbio! Akaenda akamkamata yule nyati akamuua; akamchuna ngozi na kuikata ile nyama mpaka akamaliza!!

Kisha alinyoosha mkono akaudaka ule mshale uliokuwa unakuja kwa kasi kwa ujasiri akatabasamu kidogo akasema: “Unataka kudanganya watu kuwa wewe ndiye uliyemuua huyu nyati?” Akautupa chini kisha akatuangalia.

Baadaye jioni hiyo alipita kijana mmoja akiwa amebeba kuku wake kwenye matenga mawili. Walikuwa kuku hamsini, kwa hiyo kila tenga lilikuwa na kuku ishirini na tano. Kuku hawa walizoeana sana katika matenga yao na kama ungekosea ukamweka kuku mmoja kwenye tenga lisilo lake angedonolewa hadi kufa.

Alifika kwenye uwanja ambao jana yake kulifanyika gulio la vyakula na kulikuwa na nafaka za aina aina zimemwagika na kutapakaa sehemu zote, akawafungulia kuku kutoka kwenye matenga yao ili wachakue chakue nafaka zile pale uwanjani.

Karibu na eneo hili kulikuwa na mkwaju mkubwa ambao kipanga alikuwa amepumzika na hajala muda mrefu. Mara akawaona wale kuku kiwanjani akafurahi sana. Akaanza kuruka kwa kasi na huku kucha zake ndefu amezitoa tayari kumnyakua mmoja wa kuku wa yule kijana. Bahati nzuri yule kijana naye aliwahi kumuona yule kipanga na kubaini hila yake chafu.

 Alianza mara moja kuwafukuza na kuwakamata wale kuku mmoja mmoja na kuwarudisha kwenye matenga yao. Alifanya hivyo mpaka akawamaliza wote na kisha ndipo yule kipanga akafika kasi kutaka kumnyakua kuku mmoja wao. Loo! Yule kijana alichupa akamdaka yule ndege na kumuuliza: “Unataka kuiba kuku wangu eti?”

Bulongo, ninayokueleza ni maneno ya kweli! Tena ni kweli tupu ila ni siri nzito. Nimeamua kukueleza wewe tu kwa vile ninakupenda sana. Na tafadhali usimwambie mtu yeyote. Tafadhali niahidi hautamwambia mtu yeyote mambo haya. Siku ya tatu nikiwa katika kufa/kuzimia, mashindano yaliendelea, siku hiyo msichana mmoja alikwenda kuvuna mtama mbali kidogo kutoka Gamboshi.

Bahati mbaya, wingu lilianza kutanda na dalili zikaonyesha mvua zinaweza kuanza kunyesha wakati wowote. Binti huyu kuona hivyo akaanza kukimbia ili mtama wake usije ukalowana. Njia ya kurudi kwao ilikuwa inapitia kwenye kichuguu na ilikuwa inateleza sana kwa vile watoto walikuwa wamemwaga maji sehemu hiyo. Alipokanyaga sehemu hiyo, mara akaanza kuserereka ili aanguke na kumwaga mtama wake! La haula.

Kuona hivyo yule dada alilirusha juu lile kapu la mtama! Akakimbia mpaka nyumbani kwao kijijini; akachukua kotama, akaenda kwenye konde la karibu na akang’oa ndogo haraka haraka! Akasuka kirago upesi upesi na kisha akaanza kukimbia kwenye kapu lake lililokuwa linakaribia kudondoka! Kidogo achelewe!

Alikitupa kile kirago chini ya kapu lililokuwa linadondoka na mtama wake ukamwagika juu ya kirago hicho, alitabasamu akasema: Nisingepata maarifa ya kusuka kirago hiki bila shaka mtama wangu wote ungemwagika na kulowana kabisa. Baba ningemwambiaje? Binti alifika nyumbani akauweka ule mtama wake salama salimini na akaendelea na shughuli zake.

Bulongo, baadaye akili yangu ya ufu ilianza kunitoka kidogo kidogo na nikaona ni afadhali nianze kurudi nyumbani ambako mambo yetu yanatofautiana sana na ya huku Gamboshi. Kwa vile sikuwa ninatoa sauti na nilikuwa peku, nilifika sehemu inayotenganisha dunia yetu na Gamboshi, hatua chache mbele, nikaona miguu ya mtu ameinyosha nikapiga hodi; sasa kwa vile nilikuwa na haraka ya kurudi nyumbani, sikuwa na muda wa kungojea jibu la kukaribishwa.

Nilizunguka ili niende mbele ya mtu huyo, kwa mshangao nikamwona yule mtu amepakata kichwa chake mapajani na anakisuka nywele. Alikichomoa upesi upesi mapajani pake na kukipachika shingoni, akitingishatingisha, akaniangalia na kisha akatabasamu kidogo na akasema: “Karibu kaka!  Nikusaidie nini?”

Mpendwa, jambo hili ni kama ndoto, lakini ni la kweli kabisa na nililishuhudia kwa macho yangu haya mawili.  Bwana, wahenga walisema kua uone. Niliamua nitoke sehemu hiyo kwani nilianza kuhisi kuwa karibu nitachanganyikiwa kwa kukaa eneo hili la ajabu!  Niliamua kwenda kwenye baa moja ya pombe, lakini kama unavyofahamu mimi huwa sinywi pombe, nilipofika nilichagua meza moja iliyo kuwa tupu pembeni mwa baa, muda mfupi nikawa ninakunywa soda yangu.

Baadaye kidogo alikuja dada mmoja amevaa baibui jeusi, refu la kuficha miguu yake.  Alikuja moja kwa moja hadi kwenye meza niliyokuwa nimekaa, akachagua kiti kimojawapo kisha akakaa. Alinisalimu kwa heshima kisha akatulia. Kama ilivyo kawaida kwa wanaume ukikutana na viumbe hawa, nilijikakamua nisionekane kana kwamba sipo.

Nikamuuliza: “Dada unataka kinywaji gani?” Yule dada aliniangalia akatabasamu akasema: “Naomba Mirinda nyeusi kama ipo.” Nilitoa ishara kwa mhudumu ili aje nimwagize. Alipofika nilimweleza oda yangu akaenda kumfuatia soda hiyo huyu dada. Punde si punde soda ikaletwa ikawekwa mezani kisha yule mhudumu akaenda zake na kutuacha sisi wawili.

Katika mazungumzo nilikuja kubaini kuwa yule dada alikuwa mgeni pia hapa Gamboshi na ndiyo alikuwa amefika kutoka sehemu za mbali. Nilijaribu kumdadisi ametoka kijiji gani, lakini kwa hili hakuwa radhi kuniambia. Tukaendelea kunywa soda zetu kimyakimya.

Bahati mbaya katika kujigeuzageuza kwake kwenye kiti nikaona kuwa dada huyu alikuwa na nyayo za kwato za farasi. Niliogopa sana, sikutaka ajue kuwa nimeona miguu yake ya kwato. Nilijifanya kana kwamba hakuna jambo geni, nikaamua kuhamia baa nyingine.

Nilipofika baa ya pili niliagiza nyama choma ya mbuzi na nikaagiza maji wakati ninangojea nyama kutayarishwa. Hapa pia nilikaa meza moja pembeni kabisa mwa baa kulikuwa na utulivu mkubwa. Punde si punde akaja tena dada mwingine amejaa jaa hivi. Akanisalimia na kuketi karibu na mimi kwenye meza yangu.

Huyu alionekana ni mpole kwelikweli na ikabidi nimwelezee kile kisanga cha mtu mwenye miguu ya farasi kule kwenye baa ya kwanza. Alinisikiliza kwa makini sana na nilipomaliza kusimulia akaniuliza: “Ana miguu kama hii?” Alipandisha baibui lake na kuonyesha miguu ambayo ilikuwa na kwato kama za yule mtu wa kwanza!

Mama  wee!  Nilitaka kuzimia rafiki yangu. Nikasimama na kuanza kutoka haraka sehemu hiyo ya ajabu! Mara yule dada alitoweka! Nilipotembea kwa muda mfupi, nikamwona dada mwingine. Yeye alikuwa anakuja upande wangu. Alikuwa amevaa mavazi meusi na baibui.

Mwanzoni nilimwona akiwa na urefu wa kawaida, lakini kadiri tulivyokaribiana alizidi kurefuka. Alikuwa anaongezeka mita moja kila hatua aliyopiga. Na baadaye nyayo za miguu yake zikawa zimeziba barabara kwa ukubwa wake, nikaogopa asije akanikanyaga! Huwi! Huwi! Huwi!

Je, unafahamu nini kiliendelea baada ya hapo? Usikose sehemu ya tatu yenye kusimulia mambo mazito kuhusu Gamboshi. Mtunzi wa hadithi hii ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI na anapatikana kwa simu Na. 0755629650.