Wiki iliyopita katika sehemu ya 9 hadithi hii iliishia katika aya inayosema: “Maskini weee! Nilitaka niondoke haraka, kujaribu kufungua mlango haukufunguka, nikajisogeza pembeni mbali kidogo na kile kitanda. Ghafla nikasikia sauti nyororo masikioni mwangu, ilikuwa sauti ya mrembo na hata wewe rafiki yangu Bulongo ungeisikia bila shaka ungeitamani uisikilize. Moyo wangu ukajaa shauku ya kutaka kumuona mtoa sauti hiyo. Ile sauti ikaendelea: “Mmh! Leo kuna mgeni chumbani kwangu.” Endelea…
Sikuweza kujibu lolote kwa sababu nilikuwa na woga wa mazingira nilikokuwa. Pembeni naona fisi! Kitandani kuna nyoka mkubwa na mamba ndiyo godoro! Na sasa kuna sauti nyororo ya mrembo ambaye haonekani. Bado mlango haufunguki. Ile sauti ikaendelea kutoka:
“Karibu sana Bugulugulu Duu. Nimefurahi sana kupata mgeni mtanashati kama wewe. Karibu sana.” Nilimshukuru msemaji kwa hofu na shauku kubwa na kulazimika kutoa tabasamu la kinafiki. Mara akaonekana machoni pangu msichana mrembo. Jamani yule kimwana alikuwa mrembo sana. Alijaa raha! Aliumbika vizuri! Alipendeza machoni pa mtu yeyote. Hakika alikuwa mrembo sana.
Alinisogelea pale nilipokuwa nimesimama akaniomba nikalale kitandani pale kwani ndipo nilipoandaliwa. Nilimweleza kuwa siwezi kulalia nyoka na mamba kwa vile mambo haya huko kwetu hayako.
Akacheka! Akacheka tena kwa sauti kubwa mpaka nikahisi ardhi inatetemeka kwa kicheko chake. Tukiwa katika maongezi mara macho yangu yaliangalia kwenye miguu yake. Mama weee! Nakufa! Nikapiga kelele kujaribu kuomba msaada kwani yule dada alikuwa na kwato kama za yule wa zamani niliyekutana naye kule kwenye baa.
Nikafungua mlango kwa nguvu na kuanza kukimbia haraka kutoka eneo hilo. Baadaye kidogo nikaona kwa mbele fisi wengi sana wamesimama na wananiangalia. Nilipowakaribia sana mara wale fisi wakageuka na kuwa binadamu kama sisi! Nilichanganyikiwa.
Baadaye niliendelea kukimbia. Sasa sielewi vizuri nilichokuwa ninaona njiani; fisi au binadamu! Niliogopa sana na kwa kweli wakati huo maisha ndiyo niliyoyathamini na kutaka kuyatetea kwa kila hali. Nilikimbia! Nikakimbia. Baada ya muda mrefu sana, nikamkuta babu mmoja akilima shambani kwake usiku huo!
Alishtuka akaniangalia na akaniuliza kwa hofu: “Kijana unatoka wapi na unakwenda wapi?” Nikamjibu: “Babu sijui ninakotoka na sijui ninakokwenda.” Akacheka kidogo, akaniuliza tena: “Wewe ni mgeni huku?” Nikamjibu kwa kujiamini: “Ndiyo babu. Mimi ni mgeni kabisa sehemu hizi”.
Akaniuliza tena kwa upole: “Kwa hiyo unataka kurudi nyumbani?” Nikamjibu tena: “Ndiyo babu.” Akaendelea kuniambia kuwa ni wazo zuri kurudi duniani, lakini tatizo ni njia ya kurudia niliyoipitia ni ngumu sana. Njia hiyo huyu babu alidai kuwa ina mitihani mingi kabla ya kuvuka mpaka wa dunia hii na huko!
Nikauliza hiyo mitihani ikoje? Babu akasema: “Mitihani yenyewe iko baharini”. Alinielekeza niende baharini na niwe ninafuata maelekezo nitakayokuwa ninapewa.
Niliondoka haraka nikamwacha yule babu shambani kwake. Muda mfupi nilipokuwa ninaikaribia ile bahari nikasikia sauti ya yule mrembo mwenye kwato za farasi na nilikuja kubaini baadaye kuwa kumbe yule babu hakuwa yeye bali alikuwa ni yule mrembo mwenye kwato. Akanisisitiza kuwa nisirudi nyuma ila niendelee mbele kwani huko ndiko njia ya kurudi nyumbani iliko.
Nilipofika baharini, nilianza kuingia polepole na moyo umejaa woga kweli kweli. Lakini tamaa ya kurudi kwetu iliushinda woga wangu wote. Nikaendelea kuingia baharini mpaka nikaona maji yamefika kwenye kidevu, hatua mbili, tatu ningeanza kuyanywa. Nikiwa katika kutafakari hivyo; mara nikavutwa mguu kwa mbele na kitu ambacho sikukifahamu. Nilipelekwa hadi chini kabisa baharini.
Jamani; kumbe sakafu ya bahari ni kama vile tu mabara yalivyo. Kuna sehemu za tambarare, zilizoinuka na kuna mabonde ya ufa. Kunapendeza kwelikweli. Haya ndiyo maisha ninayoyapenda kuyaishi! Ya maajabu.
Baada ya kutembea muda mfupi, niliwakuta papa wakubwa wakinywa pombe na pembeni kulikuwa na mamba wakicheza karata. Nilipoangalia kwa makini zaidi kwa mbali kidogo jamani nilisikia muziki mwororo na nikawaona samaki wakicheza muziki huo. Ilikuwa raha na hata na mimi nikawa ninachezacheza polepole.
Nilikuwa ninaona aibu samaki hawa wasije wakaniona ninacheza muziki wao na sipatii vizuri kama walivyokuwa wanacheza wao kwa umahiri. Mara ghafla nikasikia sauti ikiuliza:“Unataka nini huku ewe mwanadamu?”
Nikajibu kwa ujasiri: “Ninataka kurudi nyumbani.” Viumbe wote waliokuwa eneo hilo wakaangua kicheko na baadaye samaki aina ya changu akaja karibu yangu akasema: “Hii ndiyo njia yenyewe ila usirudi nyuma, ama sivyo usitulaumu ukiogopa na ukaamua kurudi nyuma.”
Jamani kulikuwa na kadagaa kadogo karibu nami, kakasema: “Mimi nitakunyofoa macho yako huwa wanasema nyie binadamu mna nyama nzuri sana. Ila nyama yenu ina mafuta mengi mno. Mimi sipendi sana mafuta….” Kakacheka.
Niliendelea na safari yangu humo baharini. Mara ghafla nikakuta moto mkubwa njiani na mishale mingi ilikuwa inakuja kasi. Ajabu hakuna hata mmoja ulionichoma. Nikafumba macho na kumwachia maisha yangu Mola. Niliendelea kutembea huku nimefumba macho, kwa kitambo nilipoyafumbua, loooo! Maajabu mengine.
Nilimuona kuku anapigana na tembo na hatimaye yule tembo akamezwa na yule kuku! Isitoshe muujiza mwingine ni pale ati kunguni alipommeza mbwa mzima mzima. Looo! Nilichanganyikiwa kabisa na nikaamua niendelee mbele nitoke eneo hilo. Kitambo kidogo, nilishangaa kuona mawe yakiporomoka kutoka mlimani. Mengine yalikuwa yananijia.
Nilikata tamaa ya kuishi na hapo nikakumbuka tena ile kauli ya yule dada kwamba hakuna kurudi nyuma. Baadhi ya mawe yalinipiga kichwani ila kwa mshangao nikawa siumii. Mengine yalinikwepa na mengine ndiyo hivyo tena yakanipiga. Nilihangaika sana katika hali hiyo na baadaye likaja jiwe moja kubwa lilivingirika polepole na liliponikaribia likasimama.
Nilipochungulia sehemu yake moja nikaona kuna pango, nikaingia humo kwa usalama wangu. Baadaye kwa sababu ya kipigo cha yale mawe nikauona mwili wote unauma. Mara usingizi ukanishika na sijui kilichoendelea hapo baadaye.
Nilikuja kufahamu kuwa nilikaa usingizini sehemu hiyo kwa miezi miwili kwa sababu katika usingizi wangu, hata miguu yangu ilikuwa imeanza kuliwa na mchwa ambao bila shaka walidhani nimekufa.
Niliamka kutoka usingizini kwangu nikaendelea na safari yangu ya kurudi nyumbani. Bulongo, ingawa maneno ninayokuhadithia ni ya kweli kwa vile niliyaona kwa macho yangu, lakini inabidi pia nitubu kuwa akili yangu huenda ilikuwa imeruka. Kwa sababu ukiyaangalia na kuyachunguza maneno yenyewe kibinadamu hayaeleweki.
Lakini kwa vile mimi niliyaona, siwezi kuendelea kuyaficha moyoni mwangu. Ninakuelezea wewe kipenzi changu. Amini ninachokuambia kuwa ni ukweli! Na ni ukweli mtupu. Niliyaona kwa macho yangu haya mawili. Na nina uhakika akili yangu ilikuwa timamu. Isitoshe ya nini niseme uongo kwa mtu ambaye ni rafiki yangu! Ili iweje! Maudhui ya barua hii ni kuelezea mambo ambayo yamefichama ndani ya mauti.
Rafiki, sielewi kama nilikuwa bado baharini au nilishatoka. Niliendelea na safari yangu ya kurudi nyumbani na eneo nililofika kila kitu kilihuishwa; yaani nilishangaa sana kuona hata wanyama kama mbuzi walikuwa wanaongea kama sisi watu. Nakumbuka siku moja mnamo saa 11:00 asubuhi wakati jogoo walipowika niliamka na kuendelea na safari yangu ya kurudi nyumbani.
Nilipokaribia kwenye msitu hivi, ghafla nikaona moto unawaka barabarani. Mapigo ya moyo yalianza kwenda haraka haraka. Punde nikasikia sauti ya beberu la mbuzi. Nilipoisikiliza kwa makini ile sauti nikaitafsiri eti inasema: “Shuka chini leo nimekupata. Nyie binadamu wakorofi sana. Mnatunyanyasa sana na kutudhulumu kila wakati.” Nilitembea kidogo kisha nikajikuta nimo kwenye himaya ya watu wa ajabu. Sielewi sawa sawa kama hawa walikuwa ni watu au la.
Nilipelekwa kwenye ghorofa moja na huko nikakuta nimeandaliwa chakula. Kilikuwa eti damu ya kichwa cha mtu. Sikula na waliponibembeleza ikashindikana hatimaye waliondoka. Nikaachwa peke yangu.
Je, unafahamu nini kiliendelea chumbani baada ya kuachwa peke yake? Usikose sehemu ya 11 yenye kusimulia mambo mazito kuhusu Gamboshi. Mtunzi wa hadithi hii ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI na anapatikana kwa simu namba 0755629650.