Gamboshi ni Kijiji kilichopo katika Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu. Kijiji hiki kinasifika kwa uchawi kila kona ya Tanzania. Mtunzi wa hadithi hii, Bugulugulu Duu, ameamua kuvaa uhusika wa hadithi hii. Anaelezea kuhusu mazingira na mazingara ya uchawi katika Kijiji cha Gamboshi yanavyotesa watu. Hadithi hii ina maneno magumu katika baadhi ya maeneo, lakini inaakisi uhalisia. Endelea…
Kwako Bulongo Gwike,
Salamu sana, ama baada ya salamu, mimi ni mzima wa afya njema. Hofu na mashaka ni juu yako tu wewe rafiki yangu uliye mbali nami. Vipi masomo ya darasa la saba! Mimi ninaendelea vizuri sana. Safari iliyopita nilikuwa wa kwanza katika mtihani wa kumaliza mwaka. Tumeletewa mwalimu mpya, mzee mzee hivi, lakini matata kweli kweli! Ni mwalimu mzuri sana wa somo la Kiswahili.
Madhumuni ya kukuandikia barua hii ni kutaka kukujulisha kuwa mwalimu huyu ametutaka tuandike barua kuhusu maisha tunayotaka kuishi. Nimetumia muda mwingi sana kuwaza nikuelezee kuhusu nini? Hatimaye nimeona nikumegee siri yangu ya moyoni. Ndugu yangu hii ni siri kubwa! Ninachokuomba tu rafiki yangu, tafadhali sana usimwambie mtu yeyote mambo haya. Ni mambo mazito ambayo ni siri kubwa. Ni mambo ambayo mimi nimeyashuhudia kwa macho yangu. Nimeamua nikueleze wewe kwa vile tunashibana. Kwa utangulizi wa maonyo hayo hapo juu, ukiona kuwa huwezi kutunza siri hii, basi usiendelee kusoma barua hii. La sivyo yatakayokupata usinilaumu mimi!
Mambo ninayotaka kukusimulia si ya kawaida! Nilionyeshwa na kuyaona mwenyewe katika mihangaiko yangu ya maisha. Kwa kweli kutokana na utofauti wake ninadhani ingefaa kabisa maisha kuwa hivyo. Tena yangetufaa sana sisi masela tunaopenda kuchokonoa mambo na kuonja upya upya kila mara! Ni mambo ya huko Gamboshi. Bwana Bulongo, Gamboshi ni kama dunia nyingine! Kule kuna watu wa kila aina kutoka duniani kote; kuna Waafrika na makabila yote; Wazungu, Waarabu, Wahindi, Wachina na wengine wengi! Kumekaa kiajabu ajabu tu!
Mpendwa rafiki yangu, unakumbuka mwaka juzi nilipougua ghafla na baadaye sijui tuseme nilikufa au nilizimia! Ukweli kuhusu siku hiyo ni kuwa, alikuja bibi kizee mmoja ambaye sikumtambua. Akanichapa kwa kifimbo chake, nikaanza kumfuata bila ya mimi kujua alikuwa ananipeleka wapi. Nilimfuata pole pole. Akanichukua mpaka nyumbani kwetu! Eti nilikuwa nimekufa.
Kila mtu alikuwa ana huzuni na wengine walidiriki hata kulia. Maskini mama yangu ndiye alikuwa amechanganyikiwa kupita wote. Alikuwa ananililia kweli kweli na nikamwonea huruma. Nilitaka kwenda kumtuliza, lakini kwa bahati mbaya sikuwa na uwezo wa kuongea kutokana na juju nilizopewa na yule bibi kizee. Nilitaka kusimama ili nimtulize mama yangu kipenzi, lakini sikujimudu.
Basi nikatulia hapo mlangoni aliponiketisha yule bibi kizee. Waombolezaji wapya walipokuja kelele zilianza upya. Hata wewe rafiki yangu Bulongo nilikuona nikataka kukusalimia; lakini kama nilivyosema hapo awali, sikuweza kujimudu, hivyo nilibaki nakuangalia tu!
Maskini baba yangu, alikuwa amekazana na wazee wenzake kuosha shina la mgomba. Wakiamini wanaosha mwili wa mtoto wao. Wakaliosha na kulipulizia marashi baada ya kulipaka mafuta ya thamani. Kwa hakika nilitaka kuwasihi wasipoteze muda wao kwani mimi nilikuwa mzima!
Yule bibi kizee alinipeleka hadi panapoitwa Gamboshi. Kama nilivyosema hapo kulikuwa na watu wa kila aina na siku hiyo ilikuwa siku ya kuonyesha ushujaa wa watu wa huko, ilikuwa siku ya mashindano ya kuonyeshana teknolojia mpya. Kwa kweli mambo niliyoyaona yalikuwa ya ajabu sana! Nilipapenda, laiti kama ningepata fursa ya kuishi huko daima nafsi yangu ingeridhika sana.
Pale Gamboshi kuna mibuyu mikubwa ajabu na tulienda na mwenyeji wangu yule bibi kizee ili tushuhudie maajabu ya teknolojia mpya. Kijana mmoja alijitokeza akiwa amepanda farasi. Kwenye mkono wake wa kuume alikuwa ameshika mkuki mkubwa.
Alisogea na farasi wake umbali wa mita zipatazo 300 kutoka ule mbuyu. Kisha akaanza kukimbia na farasi wake, kasi ya farasi iliongezeka sekunde kwa sekunde, vumbi likatimka. Farasi akapiga shoti. Alipoukaribia ule mbuyu umbali wa mita 20 hivi, yule kijana aliutupa ule mkuki wake kwenye lile shina la mbuyu; tundu kubwa likatokea ambamo yule kijana na farasi wake walipita kasi hadi upande wa pili wa shina!
Jamani! Sikuyaamini macho yangu! Niliyapepesa mara mbilimbili nione kama nilichokiona kina uhalisia! Ndivyo! Ni kweli kabisa huo ndio ulikuwa uhakika! Yule kijana alielekea pole pole kwenye meza kuu. Alipofika alishuka kwenye farasi wake akaja taratibu, akasimama kidogo; akajishika kifuani na kuinama kisha akaenda zake.
Mshindani aliyefuata kutuonyesha manjonjo yake alikuwa pia mpanda farasi. Naye alikwenda umbali wa mita 300 kama za yule wa kwanza. Akaanza kukimbia, mwendo ukakolea kila sekunde. Baadaye yule kijana alimbetua yule farasi wake, mara yule farasi na bwana wake wakaruka juu ya ule mbuyu na kutua upande wa pili.
Niliuangalia kwa makini ule mbuyu na urefu wake ulikuwa wapata mita 45! Alikuwa ameruka juu na kutua upande wa pili! Jamani nilichanganyikiwa. Kijana alikuja kutoka upande wa pili wa mbuyu na alipofika meza kuu aliinama kidogo kuashiria amemaliza kazi.
Zamu iliyofuata ya mshiriki wa tatu ilikuwa ya msichana. Yeye alikuwa mrefu, maji ya kunde na aliumbika vizuri. Alimchukua farasi wake akaenda umbali wa mita 300 kama walivyofanya wale wenzake. Alianza kukimbia mbio kuelekea kwenye mbuyu. Farasi alianza kukimbia mbio; mwendo ulikuwa mkali sana. Na kwa kweli mimi nilidhani mwendo huo ulikuwa unaongezeka kila sekunde.
Alipokaribia ule mbuyu tulimwona anafanya kama kuukwepa, mara akanyoosha mkono wake wa kulia. Loo! Aliunyakua ule mbuyu mzima mzima akaupepea hewani. Baadaye aliutupa angani ukaenda kuangukia ziwani! Jamani! Nilimtazama tena yule binti na sikummaliza. Na baadaye alikuja pole pole na farasi wake hadi meza kuu. Akainama kuashiria na yeye amefunga kazi.
Bulongo, si unafahamu ilivyo dhaifu kwa viumbe hawa hasa wanapokuwa wazuri; nilitaka niende kumwambia kuwa roho yangu ilikuwa imemdondokea. Lakini bahati mbaya sikuwa na uwezo wa kusimama au kujimudu. Nilibaki kumeza mate tu!
Sasa rafiki yangu; unaonaje dunia ya hawa vijana watatu? Unafikiri ni nani anawazidi wenzake? Yule wa kupita kwenye tundu la mkuki? Au ni yule aliyeruka na farasi mbuyu wa mita 45, au ni huyu kisura aliyeng’oa mbuyu na kuutupa ziwani?
Basi bwana, kwenye kuzimia au kufa kwangu niliendelea kumwona mama yangu ameshikiliwa na kina mama wengine wakimfariji na kumtia moyo. Alikuwa ametulia kidogo, lakini macho yake yalikuwa mekundu kwa kulia kwa muda mrefu. Niliendelea kumwonea huruma na kwa kweli moyo wangu ukazidi kumpenda kwa jinsi alivyokuwa ananililia mimi kitoto chake.
Yule kizee aliyeniweka mlangoni alikuja akataka kunichukua tena anipeleke kusikojulikana. Nilikataa na akawa ananilazimisha nikubaliane naye. Hapana jamani, dunia ya Gamboshi ndiyo hasa ninayopenda kuishi, maisha ya maajabu ndiyo kipenzi cha roho yangu. Si unajua tena wahenga walisema kipenda roho kula nyama mbichi. Sasa huyu bibi ananipeleka wapi tena? Mimi ni Gamboshi tu!
Je, unafahamu nini kiliendelea siku ya pili katika kifo cha Bwana Duu? Usikose sehemu ya pili yenye kusimulia mambo mazito kuhusu Gamboshi. Mtunzi wa hadithi hii ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI na anapatikana kwa simu namba: 0755629650.