Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya amedai kuwa, Ruto hakuwa na nia ya kufanya kazi nami na alitaka tu kunitumia kupata watu kushinda uchaguzi”, ameambia wanahabari.
Gachagua amezungumza hayo akiwa anatoka katika Hospitali ya Karen alipokuwa anatibiwa.
Rigathi Gachagua ameendelea kudai kuwa kuna baadhi ya watu ambao wamejaribu kumuua kwa kumuwekea sumu kwenye chakula mara mbili.
“Kwa mara ya kwanza, niseme ilikuwa mnamo Agosti 30, huko Kisumu, walinzi wa siri waliingia chumbani kwangu Kisumu na kuingia kwa nguvu na mmoja wao akajaribu kunitilia sumu kwenye chakula changu, lakini tuligundua na tukaweza kuepuka mpango huo” amesema Gachagua.
“Nilitakiwa kuuawa kwa kuwekewa sumu, na mnamo Septemba huko Nyeri, timu nyingine ilikuja na kujaribu kunitilia sumu kwenye chakula ambacho kilichokusudiwa kuwa changu na Baraza la Wazee wa Kikuyu.”
Rigathi Gachagua ameendelea kumshutumu Rais William Ruto na kudai kuwa amesaliti makubaliano waliokuwa nayo kabla ya kuingia madarakani mwaka 2022.
Gachagua aliongeza kuwa alilazimika kuwatimua baadhi ya maafisa wa ujasusi katika ofisi yake kwa sababu hakujihisi salama.
Kulingana na Gachagua, aliyemwamini amemfanya akapitia kipindi kigumu mwaka mmoja uliopita.
“Kwa mwaka mmoja uliopita, imekuwa changamoto sana kwangu. Lakini mimi ni mtu mvumilivu sana, mvumilivu kweli. Kilichotokea Alhamisi kilikuwa kilele cha mateso na mfadhaiko ulioendelea kwa mwaka mmoja.”
Gachagua aliendelea kudai kuwa tangu kulazwa katika hospitali ya Karen siku ya Alhamisi, watu walio karibu na rais ambao hawakutajwa wamekuwa wakipiga simu kubaini iwapo afya yake inazidi kuzorota.
“Ninasikia watu wake wengi walikuwa wakipiga simu hapa (hospitalini) wakiuliza ikiwa nimekufa, nimenusurika, kama nitapona, walikuwa wakisherehekea,” Gachagua amewaambia wanahabari wakati anatoka hospitalini.
”Ruto atawajibika kwa lolote litakalonitokea”, Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema.
Alilinganisha ‘mateso’ ya mkuu wake wa zamani na yale aliyokumbana nayo Kenneth Matiba wakati wa utawala wa marehemu Rais Daniel Moi.
“Nikiitazama, pengine ni historia inayojirudia. Rais William Ruto alitaka kunipitisha njia ambayo Rais Moi alimpitishia Matiba. Alimsukuma Matiba hadi akapata kiharusi na kufa. Ninapoangalia kile rais anachonifanyia, hasa sasa nikiwa hospitalini, akinididimiza, na kunitendea kama mnyama… nafkiri alitaka kunipeleka kwenye njia ya Matiba,” alisema.
Haya yanajiri siku chache baada ya Bunge la Kitaifa kupiga kura ya kumuondoa madarakani na hoja hiyo ikapitishwa na Bunge la Seneti.
Maseneta walipiga kura kuunga mkono angalau mashtaka matano kati ya kumi na moja yaliyowasilishwa dhidi ya Gachagua.
Hoja ya kuondolewa kwa madarakani iliwasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse katika Bunge la Kitaifa.
Jumla ya wabunge 281 walipiga kura kuunga mkono kuondolewa kwake madarakani dhidi ya 44 waliopinga hoja hiyo.