Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Mwanza
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Ummy Mohammed Wayayu amesema matumizi ya Mfumo wa kuwezesha uratibu wa shughuli za uandaaji wa vikao mbalimbali vya bodi na menejimenti katika Halmashauri na Taasisi za Umma(e-Board) umerahisisha uendeshaji wa vikao na kupunguza gharama za maandalizi .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ndiyo halmashauri ya kwanza kuanza kutumia mfumo huu wa e-board kati ya halmashauri 184 nchini, mfumo huu umesanifiwa na kutengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).
Amesema kuwa kabla ya halmashauri hiyo kuanza kutumia mfumo wa e-Board mwaka 2023, fedha nyingi zilikuwa zinatengwa katika ununuzi wa shajara,wino na vifaa vingine kwa ajili ya vikao vya madiwani na menejimenti katika halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza amesefafanua kuwa, “Kabla ya mfumo huu, kila mwaka tulikuwa tunatumia takribani shilingi milioni 200 hadi 300 katika maandalizi ya uendeshaji wa vikao, kwa sasa gharama ni nzuri,kwa kuwa tunatumia e-Board, ambao umetusaidie kupeleka fedha katika mambo mengine ya halmashauri,” amesema.
Ameongeza kuwa, mfumo wa e-Board umesaidia kupunguza gharama za kudurufu taarifa mbalimbali na badala yake zinapakiwa kwenye mfumo na madiwani wanapakuwa na kuendelea kuzifanyia kazi.
Ameeleza kuwa licha ya mfumo huo kusaidia katika kupunga gharama, Mkurugenzi huyo amesema kwamba mfumo wa e-Board umesaidia katika upigaji wa kura za siri katika uchaguzi wa Wenyeviti wa Kamati pamoja na uchaguzi wa Mstahiki Meya.
“Hapo awali usiri katika chaguzi hizo ulikuwa mdogo sana, lakini kwa sasa tunatumia mfumo hivyo kura zinakuwa za siri na kila mtu ndani ya nafsi anajua amemchagua nani,” amefafanua.
Ameongeza kuwa mfumo wa e-Board unawasaidia madiwani kushiriki katika kila kikao hata wanapokuwa nje ya halmashauri hiyo kwa kutumia vishkwambi ambavyo vimewezeshwa matumizi ya mfumo huo na kugawiwa kwa kila diwani.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo Mheshimiwa Renatus Mulunga, amesema kuwa mfumo wa e-Board umewasaidia madiwani kuendesha vikao vyao kwa ufanisi ili kuboresha huduma za wananchi wa Ilemela.
“Nina miaka 25 kwenye udiwani, huko nyuma ilikuwa lazima ujaze gari mafuta kwa ajili ya kusambaza makarabrasha, lakini kupitia mfumo wa e-Board kila diwani anapata taarifa na makabrasha yake popote alipo kupitia mfumo na kuanza kuyafanyia kazi,” amesema Bw. Mulunga.
Mulunga ametoa rai kwa halmashauri nyingine ambazo bado hazijaanza kutumia mfumo wa e-Board, kufanya ziara halmashauri ya Manispaa ya ilemela ili zikajifunze au kuwasiliana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ili zipate uelewa kuhusu mfumo huo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Halmashauri ya Ilemela Isaack Tanguye, amesema kwamba halmashauri hiyo ilianza kutumia mfumo wa e-Board baada ya kupata malalamiko kuhusu gharama kubwa za uandaaji wa vikao.
Ameongeza kwamba baada ya malalamiko hayo kuwa mengi, kitengo chake kiliamua kuwasiliana na e-GA kuomba mfumo wa e-Board, na baadaye walianza kuwajengea uwezo Madiwani pamoja na Menejimenti ya halmashauri hiyo ili kuanza kufanya vikao vyao kidijiti.