Mhadhiri wa Utalii na Mambo Kale katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Noel Lwoga; na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Profesa Audax Mabulla, wanazungumzia ugunduzi wa Zinj miaka 60 iliyopita na faida zake kwa Tanzania, Afrika na ulimwengu. Endelea…
Dk. Lwoga: Zinj ni kama tanzanite
Zinj ana faida katika makundi matatu ya kiuchumi, kijamii na kimazingira. Zinj ni kama tanzanite au hata zaidi kwa sababu tanzanite unaweza ukachimba ikaisha, lakini ukihifadhi vema Zinj ambaye hapatikani sehemu nyingine duniani inaweza ikawa ni kichocheo cha kupata mapato endelevu.
Utalii ni sekta ambayo kwa Tanzania inachangia takriban asilimia 25 ya mapato ya kigeni. Tukiweza kutumia hili fuvu vile inavyopasa, tukalitangaza – linaweza likatuletea watalii wengi zaidi. Kuna nchi zinazotegemea urithi kama huu. Sisi bado hatujautumia vizuri. Tukilitangaza sawa sawa hili fuvu linaweza likawa chanzo kizuri sana cha mapato tofauti na sekta kama kilimo unachopaswa ulime, usafirishe mazao – Zinj ni kwamba hela zinakuja zenyewe.
Kwa upande wa kijamii: Ni kweli kwamba jamii ya Kiafrika imekuwa na kutojiamini kutokana na historia tulivyopita katika mambo ya utumwa, ukoloni na kadhalika. Tukizungumzia Zinj na kuwaelimisha wananchi inaweza ikamsaidia Mwafrika kujiamini, kujitambua na hata kujivunia asili yao na kujivunia wenyewe kama Waafrika.
Kwa mara nyingine inaweza ikaleta ukombozi kwa kizazi kijacho. Hifadhi ya Zinj ni kama hifadhi ya kujiamini kwa kizazi kijacho. Tukilitangaza hili, hawa watoto wa leo wakatambua hivyo na kujifunza historia ni kwamba tutapata kizazi kinachojiamini na imara kuliko tulikotoka.
Faida za kimazingira: Umuhimu wa kuhifadhi vitu kama hivi, pale ambako jamii inatambua thamani ya urithi, ikatambua mazingira ambayo yaliwezesha kupatikana kwa fuvu hili – kutaifanya jamii kuona umuhimu wa kuhifadhi, tena si kwa kumshurutisha mtu, bali mtu atatamani kile kitu kiendelee kuwapo. Kwa maana hiyo kuna faida kubwa kimazingira. Kuna umuhimu mkubwa wa kutangaza adhimisho hili la miaka 60 ya Zinj kwa sababu watu watajua umuhimu wa Zinj, lakini pia umuhimu wa kuhifadhi mazingira ambamo huyu Zinj amegundulika.
Profesa Mabulla: Fahari ya Tanzania, Afrika
Pale kwenye eneo alikopatikana Zinj walipopima lile tabaka walikuta ni la miaka milioni 1.075. Kwa wakati huo [1959] likawa ndilo fuvu lenye umri mkubwa sana dunia nzima. Kwa sababu hiyo likatangazwa na likaiweka Tanganyika [Tanzania] kwenye picha ya ulimwengu na Bara la Afrika.
Mtazamo wa wanasayansi ukaanza kubadilika. Mwanzo waliamini watu wote wameanzia huko Asia, Ulaya – sasa kwa ugunduzi wa Zinj mtazamo ukageuka. Hii ni muhimu kwa sababu mindset ya watu na wataalamu wakaona tumetoka Afrika hata kama tutakuwa Wazungu au watu wengine, lakini chimbuko letu ni Afrika. Kwa hiyo Zinj akaiinua Tanganyika, akaiinua Afrika. Miaka hiyo ubaguzi, Mzungu hata kukugusa wewe mweusi anaona utabadilika, akiamini sisi bado tunaendelea kubadilika mwishowe tutakuwa kama wao. Walikuwa wanatuona sisi tuko nyuma kumbe hawakujua rangi yetu hii [nyeusi] ilikuwa mahususi kwa mazingira ya kwetu. Kwa hiyo ugunduzi wa Zinj ukaitangaza sana [Tanganyika].
Pia wanasayansi kwa dunia nzima wakaanza kuangalia Tanzania, wakaanza kuangalia Afrika Mashariki kufanya utafiti wao Kenya, Ethiopia na hata Afrika Kusini. Ugunduzi huu ukasaidia kuchochea shughuli za utafiti, ukachochea hata ufadhili. Leaky akaanza kupewa hela, lakini kabla ya hapo utafiti wake haukuwa na udhamini.
Wazungu ndio wameiga nywele zetu. Vitu vingi sisi tume – invent wenzetu wameviboresha tu. Hata Wazungu wanajua ‘we are all Africans’. Rangi zetu hazitupi tofauti – genes ni zilezile, kila kitu ni kilekile – we are all Africans.
Na si mafuvu tu ambayo yamethibitisha, lakini hata mafunzo ya genetics, DNA watu [wanasayansi] wamezichambua. Hata Eva alikuwa mwanamke wa Kiafrika. Kutoka hapa ndiyo wakaenda nchi nyingine wakawa African diaspora. Watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine ni kitu kimekuwapo kwa miaka milioni 1.7 na walikuwa wanaanzia huku Afrika.
Asili ya binadamu
Kama binadamu tumekuwa tunajiuliza maswali kadha wa kadha kuhusu uwepo wetu duniani:
-Sisi ni nani?
-Tumetoka wapi?
-Tupo duniani kwa ajili gani?
-Tunaelekea wapi?
Haya ni baadhi tu ya maswali tunayojiuliza. Wataalamu wamejaribu kujibu maswali haya kutoka tasnia mbalimbali. Pale kazi za wataalamu zinapokosa majibu, wanarejea simulizi na hadithi za wahenga huku wakiendelea kutumia mbinu za kisayansi kupata majibu sahihi yanayokidhi kiu yetu ya kufahamu zaidi. Taaluma za sayansi asili kama vile elimu miamba, elimu viumbe, kemia na fizikia, kwa pamoja zimejaribu kutoa majibu ya maswali yanayoulizwa na wanafalsafa wa leo, hali inayoleta msisimko kwa wengi.
Katikati ya karne ya 19, Mwingereza aliyebobea katika elimu viumbe, Charles Darwin, alianzisha nadharia ya mabadiliko ya viumbe kuendana na nyakati na mazingira, na kuelezea chimbuko la binadamu na mabadiliko yake.
Darwin alielezea uwezekano mkubwa wa Bara la Afrika kuwa kiini cha chimbuko la binadamu kwa kuzingatia wingi wa aina za sokwe wanaopatikana huko hadi leo, hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa sasa nadharia hii inakubalika kwa jamii kubwa ya wanasayansi, lakini mnamo karne ya 19 hii nadharia tete kuhusu Afrika haikutambuliwa wala kukubalika katika mfumo wa imani za Wazungu.
Kwa karibu karne nzima, kila nadharia iliyokuwa inakubalika ilihusu Ulaya, na halafu Java, Indonesia na baadaye tena China. Hata uvumbuzi wa zamadamu aina ya Australopithecus africanus huko Afrika Kusini mwaka 1924 haukuleta hamasa yoyote katika mtazamo huo, hadi miaka ya 1960 pale ugunduzi mpya ulivyotoa majibu ya kuipendelea Afrika.
Mwaka 1959, Dk. Lous na Mary Leakey walipogundua fuvu la Zinjanthropus boisei katika Bonde la Olduvai, kumekuwa na ongezeko kubwa la upatikanaji wa mabaki ya zamadamu na ushahidi wa shughuli na tabia za binadamu. Mbinu zinazotumiwa na wanasayansi kupata taarifa zimeongezeka na juhudi za wataalamu nazo zimeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Mwishoni mwa mwaka jana Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, alizindua Makumbusho ya Olduvai Gorge, ambayo ni chimbuko la historia ya binadamu kwa takriban miaka milioni 3 iliyopita.
Makumbusho haya ni kielelezo cha maisha na ustaarabu wa binadamu ambao unaelezea maisha ya vizazi vilivyopita na kusaidia kujua hasa historia ya binadamu.
Ujenzi wa makumbusho haya umesaidia kuvutia watalii na wanasayansi wa masuala ya mambo kale kutoka pande zote za dunia.
Ujenzi umefanikishwa na Jumuiya ya Ulaya kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha. Gharama halisi za ujenzi ni Sh bilioni 1.7; asilimia 20 kati ya hizo zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Mhifadhi Mambokale wa Kituo cha Kumbukizi ya Dk. Louis na Mary Leakey; Jemima Richard, anasema majengo mapya na miundombinu vimeleta mapinduzi makubwa mno Olduvai Gorge, hasa kwa upande wa ongezeko la wageni.