Nimepata fursa hivi karibuni kushiriki katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa atamizi ya sekta ya ubunifu katika nyanja za muziki, filamu, na mitindo iliyofanyika Dar es Salaam.
Mradi huo, ambao unanuwia kunufaisha wadau wa tasnia ya sanaa waliopo ndani ya nchi za Afrika Mashariki unasimamiwa na shirika lisilo la kiserikali la Culture and Development East Africa (CDEA), ambako mimi nimepewa heshima ya kuwa Mwenyekiti wake na Mjumbe wa Bodi kwa miaka kadhaa sasa. CDEA ni miongoni mwa asasi zisizo za kiserikali 12 ambazo zitatekeleza mradi huo ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kila moja ya asasi hizo 12 zilizopewa jukumu hilo zinapaswa kutekeleza mradi kwenye nchi walau mbili, na CDEA itatekeleza mradi huu Tanzania na Uganda.
Wafadhili wakuu ni Jumuiya ya Afrika Mashariki na kampuni ya GIZ ambalo ni Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Serikali ya Ujerumani.
Malengo ya miradi mingi nchini katika nyakati hizi yanajikita katika kukuza uwezo wa wananchi wa kuinua kipato chao, na mradi huu unayo malengo ya aina hiyo. Inatarajiwa kuwa utekelezaji wa mradi huu utakuza ushirikiano katika kufanya kazi za ubunifu miongoni mwa wabunifu wa Afrika Mashariki kwa maana ya kuwarahisishia wasanii kuhama kutoka eneo moja la Afrika Mashariki na kwenda eneo jingine kwa nia ya kujiongezea zaidi ujuzi, mtaji, na masoko ya kazi zao.
Matarajio makuu ni kuona wabunifu chipukizi wanakua katika ujuzi wa kiufundi ili kuweza kuongeza thamani ya bidhaa wanazozalisha na hatimaye kujiwezesha kupata miliki bunifu (intellectual property rights). Aidha inatarajiwa kuwa wale wabunifu wa mitindo wataweza kupata hataza (patent).
Kwa kufikia hatua hizi muhimu za kumiliki kazi zao kisheria, CDEA inatarajiwa kuwa wabunifu wataweza kuongeza ubora wa bidhaa zao kwa kiwango cha kimataifa na wataweza kuanza kuuza kazi zao nje ya nchi bila kuwa na hofu ya kupokonywa haki hizo. Hatimaye inatarajiwa kuwa vipato vyao vitaongezeka na hali yao ya kuiuchumi kuimarika.
Kwa muda mrefu sekta ya sanaa imeonekana kuendeshwa kwa taratibu ambazo si rasmi, na inatarajiwa kuwa, polepole na kupitia mradi huu, washiriki watajiongezea uwezo wao na kuibadilisha sekta hii iwe rasmi.
Hiyo ni nia, lakini matokeo siyo siku zote hufuata malengo. Nimesikiliza hivi karibuni mahojiano ya msanii Diamond Platnumz akizumgumzia thamani ya mmoja wa mikataba yake na kampuni ya kurekodi ya kimataifa. Ni mkataba wenye thamani kubwa sana, siyo tu kwa Tanzania, bali hata kwa nchi nyingi tu ulimwenguni. Walengwa wa mradi huu hawatajijengea uwezo wa kumfikia Diamond, lakini watajiongezea uwezo wa kuimarisha kazi zao, na kujiongezea kipato.
Mradi huu wa atamizi unazungumzia kuwaongezea wabunifu, kupitia mafunzo, uwezo wao kushirikiana na wasanii wenzao wa Afrika Mashariki na kuwapa nyenzo za kulinda haki za kazi zao. Lakini tunatambua kuwa iwapo Diamond ameweza kupata mafanikio makubwa ya kuongeza mapato yake bila ya kupitia kwenye mradi huu wa atamizi ni ukweli kwamba hata wale wasio na msingi huu wanaweza kufikia mafanikio makubwa. Yapo masuala kadhaa yasipotimia, basi hata elimu na ujuzi wa kiasi gani haviwezi kuleta hayo mafanikio yanayokusudiwa kufikiwa.
Wapo wauza mkaa ambao hawakumaliza darasa la saba ambao wana kipato kikubwa kuliko walimu wenye shahada za vyuo vya elimu ya juu.
Wanaokuzwa kwa imani za dini wanaamini kuwa mafanikio yanaletwa na Muumba. Wengine wanaamini kuwa mafanikio yanaletwa kwa vibuyu na tunguli. Wasioamini vyote viwili watakwambia kuna watu wanazaliwa na bahati tu, na kama huna hiyo bahati kamwe hutafanikiwa.
Lakini wote tunaweza kukubaliana kuwa mbumbumbu mwenye elimu na maarifa ni bora kuliko mbumbumbu asiye na elimu na maarifa. Mwenye elimu na maarifa anajijengea nafasi nzuri zaidi ya kufikia mafanikio.
Na ndiyo kwa msingi huo CDEA inaamini kuwa mradi huu ni fursa muhimu kwa wabunifu chipukizi, na ni nafasi yao ya kushiriki na kujiongezea uwezo.