DAR ES SALAAM

NA MWALIMU SAMSON SOMBI

Machi 19, mwaka jana Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania baada ya kifo cha mtangulizi wake, Rais Dk. John Magufuli, kilichotokea Machi 17, mwaka jana.

Akizungumza katika hotuba yake fupi baada ya kula kiapo cha kuongoza nchi, Rais Samia aliwaomba Watanzania kuzika tofauti zao na kuwa wamoja kama taifa.

“Huu si wakati wa kutazama mbele kwa shaka bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini makubwa na kujiamini, si wakati wa kutazama yaliyopita bali ni wakati wa kutazama yajayo. Si wakati wa kunyosheana  vidole bali ni wakati wa kushikamana mikono na kusonga mbele,” amesema Rais Samia.

Katika hatua nyingine, Rais Samia aliahidi kuendelea kudumisha ujirani mwema na nchi jirani na kuimarisha uhusiano wa kimataifa huku akiwahakikishia wananchi uongozi unaozingatia haki na usawa.

Aprili, mwaka jana Rais Samia amelihutubia Bunge kwa mara ya kwanza na kueleza dira na mikakati ya serikali yake katika harakati za kuwaletea wananchi maendeleo na kuweka wazi suala la kuendelea kudumisha muungano ambao Aprili 26, mwaka huu utatimiza miaka 58 ya kuzaliwa kwake.

Kwa nyakati tofauti, Rais Samia, amekutana na makundi mbalimbali ya kijamii wakiwamo wazee, viongozi wa dini, wanawake na vijana.

Nia na madhumuni ikiwa ni kupata maoni na kuhimiza uongozi shirikishi katika maendeleo ya taifa.

Katika hatua ya kudumisha na kuendeleza ujirani mwema na kuimarisha uhusiano wa kimataifa, Rais Samia ameendelea kufanya ziara za kikazi katika nchi jirani za Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi.

Huku akitembelewa na viongozi wa kitaifa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na duniani pia amefanya ziara nje ya Afrika na Septemba, mwaka jana alihudhuria na kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) huko Marekani na baadaye kufanya ziara ya kikazi huko  Scotland alikohutubia na kueleza juu ya athari ya mabadiliko ya tabianchi.

Akibeba pia ajenda ya uwekezaji, Rais Samia amefanya ziara nchini Misri, ziara inayoelezwa kuwa na matokeo mazuri katika sekta ya uwekezaji hapa nchini.

Akitimiza miezi tisa ya uongozi wake Desemba, mwaka jana, Rais Samia ametoa hotuba katika matukio mbalimbali zinazoelezwa kuwa ni funga mwaka wa 2021. Mwaka unaotajwa kuwa na mabonde na milima.

Jumatano ya Desemba 8, mwaka jana Rais Samia alihutubia taifa kwa njia ya televisheni akieleza mafanikio na changamoto katika miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania kwa sasa).

Katika hotuba hiyo ya saa tatu usiku, alisema Watanzania wana mambo mengi sana ya kujivunia wakati wakiadhimisha miaka 60 ya uhuru pamoja na changamoto za hapa na pale.

Amesema mafanikio hayo ni pamoja na kulinda uhuru na mipaka ya nchi, kujenga umoja wa kitaifa na mshikamano uliozaa na kulea amani na utulivu uliopo nchini, kuimarisha uchumi na kupunguza umaskini.

Amesema katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika safari ndefu ilikuwa ni kutoka katika kundi la nchi maskini na kufikia nchi ya uchumi wa kati wa chini, jambo ambalo limefanikiwa.

Jambo jingine ni kuongezeka kwa upatikanaji na uboreshaji wa huduma za jamii kwa wananchi. Mafanikio mengine ni kujenga heshima ya nchi na ushawishi wa kikanda na kimataifa.

Kwamba katika miaka 60 ya uhuru tumefanikiwa kushawishi Kiswahili kuwa lugha mojawapo inayotumika katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

“Tumefanikiwa kushawishi Kiswahili kuwa mojawapo ya lugha za SADC. Umoja wa Afrika (AU) na siku chache zilizopita UNESCO imepitisha azimio la kutenga siku ya  Julai 7 ya kila mwaka kuwa siku ya lugha ya Kiswahili duniani,” amesema Rais Samia.

Kuhusu ukuaji wa sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi kwa maendeleo ya viwanda, amesema kuna hitajika nguvu kubwa kuinua sekta hizo.

‘Wito wangu kwenu ni kuendelea kudumisha amani, umoja, mshikamano na muungano wetu kuendelea kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wetu na kufanya mageuzi makubwa kila inapolazimu kuinua sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuendana na kasi ya uchumi wa dunia.

“Tunapoangalia mbele tunakwenda kuandaa dira ya miaka 25 ijayo itakayotutoa mwaka 2025 hadi mwaka 2050. Itaelekeza kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kwa kutoa kipaumbele kwa sekta zinazogusa wananchi moja kwa kwa moja,” amesema Rais Samia.

Tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini Julai, 1992 na kufanyika kwa uchaguzi mkuu  wa kwanza chini ya mfumo huo mwaka 1995, kumekuwa na mijadala juu ya ukuaji wa demokrasia na uendeshaji wa siasa.

Katika hatua ya kujenga mazingira bora ya uendeshaji wa siasa nchini, Desemba 15, mwaka jana Rais Samia alizindua mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa jijini Dodoma na kuwaomba wadau hao wa siasa nchini kujadili na kutafuta njia bora ya kufanya siasa zenye tija kwa ustawi wa taifa letu.

“Niwaombe wenyeviti wenzangu wa vyama vya siasa tusitazame yaliyopita, tutazame mbele kwa matumaini. Tuweke nguvu katika kujenga Tanzania mpya yenye kusameheana na kuheshimiana.

‘Kama mlezi wa amani, natakiwa kuwa mvumilivu, msikivu na mwenye kustahimili na niko tayari kufanya hivyo,” amesema Rais Samia.

Katika hatua nyingine, Desemba 24 Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imeunda kikosi kazi cha watu 23 cha kupitia hoja 80 zilizojitokeza katika mkutano wa wadau wa siasa na demokrasia na kuandaa mapendekezo.

Mapendekezo yatakayowasilishwa katika Baraza la Vyama vya Siasa yatapitiwa na kuwasilishwa serikalini kwa hatua zingine.

Kikosi hicho kimeundwa kwa wito wa wadau wa demokrasia ya vyama vya siasa waliohudhuria mkutano huo uliofanyika kwa siku tatu mfululizo wakitaka kijumuishe wawakilishi wa makundi yote wadau waliohudhuria.

Katika funga mwaka nyingine, Desemba 28 akiwa Dar es Salaam, Rais Samia ameeleza umuhimu wa mikopo kwa maendeleo ya taifa na kuwakosoa baadhi ya watu wanaopinga mikopo hiyo.

Akisisitiza umuhimu wa mikopo, Rais Samia anasema uwekezaji katika ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza unaogharimu Sh trilioni 14.7 unaendelea vizuri, hivyo serikali itahakikisha inakopa kukamilisha mradi huo ili fedha ilizowekeza zisipotee. 

“Kwa njia yoyote, kwa vyovyote tutakopa, tutaangalia njia rahisi zitakazotufaa kukopa na fedha hizi hatutazitoa kwenye tozo wala hatutazitoa kwenye kodi tunazokusanya ndani, ni lazima tutakopa,” amesema Rais Samia.

Katika hotuba ya kuuaga mwaka 2021 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2022, Rais Samia ameeleza changamoto na mafanikio ya mwaka 2021 na kutoa dira kwa mwaka 2022.

Akihutubia taifa kupitia vyombo vya habari, ameahidi kukabiliana na changamoto zinazowakumba wananchi kila siku, kupambana na Uviko-19, sensa ya watu na makazi na kuongeza ubora katika utoaji wa huduma.

“Kama ilivyotamkwa katika mpango wa serikali wa miaka mitano kuanzia 2021/2026 kwamba lengo kuu ni kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi wa taifa kwa ujumla,” amesema Rais Samia.

Kiongozi huyo wa nchi alibainisha kwamba dunia bado inakabiliana na Uviko-19 na kwa sasa lipo wimbi  la nne la ugonjwa huo.

Amesema kirusi kipya cha omicron kinaenea kwa kasi na tayari kipo na kimeshaingia nchini.

“Niwakumbushe kuchukua tahadhari kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya, nitumie fursa hii kuwahimiza kupata chanjo dhidi ya Uviko-19.

“Natambua kuwa chanjo haizuii mtu kupata maambukizi ila inapunguza makali ya ugonjwa huo, hivyo niwahimize wananchi kwenda kuchanja, chanjo zipo na zinapatikana bila malipo,” amesema Rais Samia.

Kuhusu uwajibikaji kwa sekta za umma na binafsi, amezitaka kuanza mwaka mpya kwa kasi na kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

“Kwa watumishi wote wa umma na sekta binafsi, nitoe rai kuwa ni vema tukauanza mwaka mpya 2022 na lengo la kuongeza ufanisi katika uzalishaji na ubora katika utoaji wa huduma,” amesema.

Mfuatiliaji wa masuala ya siasa na jamii, Hashim Yahya wa Morogoro, anasema pamoja na changamoto za kimaisha wananchi wameanza kuelewa dira ya Serikali ya Rais Samia.

“Kila uongozi huwa na malengo yake katika harakati za kuwaletea wananchi maendeleo. Kadri siku zinavyosonga mbele wananchi wameanza kuelewa dira ya maendeleo ya serikali ya Rais Samia,” anasema Yahya. 0755985966