NA MICHAEL SARUNGI
Hatimaye Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), imeteketeza kilo 1,103.58 za
nyama mbovu, mali ya kampuni ya Frostan Limited ya Dar es Salaam.
Kuteketezwa kwa nyama hiyo kumefanyika Februari 21, mwaka huu, ikiwa ni
baada ya JAMHURI kuwa gazeti pekee lililoibua biashara hiyo haramu kwa mujibu
sheria za nchi, lakini pia ikihatarisha afya na uhai wa watu.
Katika toleo lake la 327, gazeti hili liliripoti kuuzwa kwa nyama ya kampuni hiyo
kutoka Marekani na Afrika Kusini, iliyomalizika muda wake wa matumizi.
Nyama hiyo iliyonunuliwa pia na JAMHURI katika uchunguzi wa habari hiyo,
iliuzwa kwenye maduka ya bidhaa mbalimbali maarufu kama supermarkets, bucha
za kampuni hiyo, hoteli na balozi kadhaa za jijijini humo.
Maduka ya kampuni hiyo yaliyotumika kuuza nyama mbovu ni pamoja na
yaliyobainika kuwa maeneo ya Sinza, Mwananyamala, Mbagala, Kwa Mtogole na
Msasani.
Zikiwa zimepita takribani siku 44 tangu kuchapishwa kwa habari iliyohusu nyama
hiyo, TFDA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Baraza la Taifa la Hifadhi ya
Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeteketeza nyama hiyo katika eneo la Dimani,
Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Awali, nyama hiyo ilipangwa kuchomwa Kibaha, lakini hapakuwa na mawasiliano
mazuri kati ya TFDA na NEMC, hivyo kusababisha kuahirishwa kwa uteketezaji
wa nyama hiyo.
Afisa Mazingira wa Manispaa ya Kinondoni, Ahamed Msangi, amesema NEMC
walifanya ukaguzi katika eneo la awali lililopo Kibaha na kubaini halikukidhi vigezo
vinavyoruhusu uteketezaji wa nyama mbovu kufanyikia hapo.
Msajili wa Bodi ya Nyama nchini (TMB), Suzan Kiango, amesema kuteketezwa
kwa nyama hiyo ni mojawapo ya vielelezo vya namna Serikali ilivyodhamiria
kuwadhibiti wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.
Amesema TMB, kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali, wameunda timu
itakayofanya ukaguzi wa kushtukiza kwa wafanyabiashara ya nyama, ili
watakaobainika kukiuka sheria na kanuni wachukuliwe hatua ikiwa ni pamoja na
kuteketeza bidhaa zao na kunyang’anywa leseni za biashara.

Pia Kiango amesema ili kudhibiti hali hiyo katika hatua za awali, TMB imeanza
kutoa mafunzo kwa watumishi wa mamlaka za Serikali za Mitaa watakaoshiriki
kutoa elimu ya namna ya kusimamia uzalishaji wa nyama kwa umma wakiwamo
wachinjaji wa mifugo na walaji.
Amesema majaribio ya mpango huo yatawahusisha watumishi wanne kutoka
katika kila mamlaka za Serikali za Mitaa za mikoa ya Dar es Salaam, Pwani,
Morogoro na Dodoma.
Mratibu wa Kanda wa NEMC, Jaffar Chimgege, amesema dhamira ya mamlaka
hiyo ni kuhakikisha mazingira yanabaki kuwa salama kwa viumbe na mimea.
Amesema kutokana na hali hiyo, NEMC itaendelea kuwadhibiti watu wenye nia
ovu na wanaoshiriki vitendo vyenye kuathiri maisha ya watu hasa kwa
inayohusiana na uharibifu wa mazingira.
Chimgege amesema NEMC inawataka watu wanaoshiriki shughuli mbalimbali za
kibinadamu kuhakikisha kuwa mazingira yanaendelea kuwa salama kwa kila
kiumbe.
Mkaguzi wa vyakula kutoka TFDA, Deltrunds Simforian, amesema kuteketezwa
kwa nyama ya Frostan Limited kunapaswa kuwa mfano kwa wafanyabiashara
wengine wa bidhaa zinazotumiwa na binadamu, ili waiepuke hasara inayotokana
na uteketezwaji wa bidhaa zao.
Amesema TFDA inaendelea kuimarisha mbinu na mikakati kwa kushirikiana na
TMB ili kukabiliana na wafanyabiashara wenye nia ya kutengeneza faida kubwa
kwa maslahi binafsi bila kujali afya za walaji.
WENYE HOTELI WAASWA
Meneja Ugavi wa Hoteli ya Sea Cliff ya jijini Dar es Salaam, Caleb Mwambe,
ambaye ni mmoja wa washirika wa kibiashara wa Frostan Ltd, amesema vitendo
vya uuzaji nyama mbovu vinapaswa kuchukuliwa hatua na mamlaka husika ili
kulinda afya za walaji kama wanaotumia bidhaa za kampuni hiyo.
Amesema uongozi wa hoteli hiyo inayotoa huduma za kibinadamu, utakutana
kuitafakari hali iliyojitokeza na kuamua hatua za kuchukua ili kukabiliana na hali
iliyojitokeza.
Kwa mujibu wa Mwambe, ni jukumu la hoteli zote nchini kushirikiana na mamlaka
husika kupambana na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu, wanaouza bidhaa
zisizokidhi viwango.
WANANCHI WAKOSOA

Baadhi ya wananchi wamepongeza hatua ya kuteketezwa kwa nyama hiyo,
ingawa kwa kukosoa kwamba umepita muda mrefu tangu bidhaa hiyo kubainika
kuwapo sokoni.
Wamesema nchi inakabiliwa na kasi ya ongezeka la bidhaa zikiwamo za vyakula
visivyo na viwango kwa matumizi ya binadamu, lakini hatua za udhibiti hazioneshi
matumaini ya kuondokana na hali hiyo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Uteketezaji (Incinerator Company), David Gatleii,
amesema uteketezaji wa nyama ya Frostan Limited ni moja ya majukumu yao,
kuhakikisha usalama wa viumbe kwa kuharibu bidhaa zinazobainika kuwa
hatarishi kwa uhai wa viumbe.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, amesema hatua za kuwadhibiti
wafanyabiashara wanaouza bidhaa bandia zinazohatarisha maisha ya watu, kama
ilivyobaini kwa Frostan Limited ni endelevu.
Amesema Serikali imetoa maagizo kwa TMB kuimarisha mifumo itakayowadhibiti
wafanyabiashara wanaoingiza nyama na vyakula vibovu kutoka nje ya nchi.
Hata hivyo, Mpina amekosoa hatua ya uingizaji wa nyama kutoka nje ya nchi
wakati Tanzania ina mifugo mingi, ikishika nafasi ya pili barani Afrika.
Mpina amesema uingizwaji wa nyama hiyo unaopaswa kudhibitiwa, unachangia
kuwanyima fursa wafanyabiashara wa mazao ya mifugo nchini.
Amesema takwimu za wizara hiyo zinaonesha kuwa Tanzania ina ng’ombe milioni
28.4, mbuzi milioni 16.7, kondoo milioni tano, kuku milioni 77, hivyo hakuna
sababu ya kuendelea kutegemea uagizaji wa nyama kutoka nje.
Kwa mujibu wa Mpina, katika kipindi cha mwaka, Tanzania inaagiza nyama tani
2,000 kutoka nchi za nje hasa Kenya, Afrika Kusini, Dubai, Uingereza, Marekani
na Ubelgiji, kiasi kilicho sawa na inayosafirishwa kwenda nje.
Amesema ipo haja ya kuhakikisha mamlaka husika zinapitia upya taratibu za
utoaji wa leseni kwa wafanyabiashara wanaoagiza nyama kutoka nje ya nchi.
ILIVYOKUWA
Kampuni ya Frostan Limited ilibainika kubadilisha tarehe za kumalizika muda wa
matumizi ya nyama iliyoagizwa kutoka Marekani na Afrika Kusini, ili iendelee
kuuzwa nchini licha ya kuwa ni kinyume cha sheria.
JAMHURI lilipata nyaraka na taarifa za kina kuhusu ‘mchezo mchafu’ huo
uliothibitishwa na Mkurugenzi wa kampuni hiyo (mtaje jina lake), akidai kwamba
haikuwa kosa kwa vile taarifa zake zilitolewa TFDA kabla ya kufikia uamuzi huo.

Mwisho