Friedikin Conservation Fund (FCF) ni Kampuni tanzu ya kampuni za uwindaji wa kitalii zinazomilikiwa na tajiri Mmarekani, Friedkin. Kampuni hizi zimekuwa mstari wa mbele kuvuruga tasnia ya uwindaji wa kitalii nchini Tanzania.

Zimekuwa zikikiuka sheria za nchi kwa makusudi huku zikionekana dhahiri kuwa ziliiweka Serikali iliyopita mfukoni, hasa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, na wakubwa wengine. 

Zimekuwa zikijivisha joho la kusaidia juhudi za uhifadhi ingawa zimekuwa zikitajwa kujihusisha na ujangili na uhalifu mwingine kama usafirishaji na uuzaji bangi. Zimekuwa zikifanya haya kwa kutumia vibaraka wao ambao ni viongozi wa Serikali iliyopita na baadhi ya wabunge.

Kampuni hizi zimekuwa na ujasiri wa kudai hadharani kuwa zina uwezo wa kuamua nani awe Waziri wa Maliasili, nani awe Mwenyekiti wa Bunge wa Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Mazingira na Maliasili na nani awe Mkurugenzi wa Wanyamapori! 

Kwa kutumia nafasi yake ya uwaziri, Nyalandu alinyang’anya vitalu kutoka kwa kampuni zilizokuwa zimemilikishwa kihalali na kuvigawa kwa rafiki zake hao Wamarekani. Hapa ni vema ikajulikana kuwa Nyalandu alishasema Wamarekani walikuwa wametaka awe rais wa Tanzania kwenye Uchaguzi wa mwaka 2015!

Sheria inaweka ukomo wa idadi ya vitalu kwa kampuni – inataka mchakato wa kugawa vitalu ufanywe na Kamati ya Ushauri ya Ugawaji Vitalu; inataka mchakato huo uanze kwa kutangazwa kwanza kwenye vyombo vya habari na waombaji washindanishwe kwa kuzingatia vigezo; inataka kampuni inayoomba kitalu iwe imeandikishwa kama kampuni ya uwindaji wa kitalii.

Kampuni hizi zilimpa Nyalandu ndege ya kutumia wakati wa kampeni zake za ubunge na hata kwenye urais. Katika Awamu hii ya Tano kampuni hizi zilihaha kuhakikisha kuwa Nyalandu anapata uwaziri wa Maliasili na Utalii na alipokosa zikaelekeza nguvu awe Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili.

Nyalandu alizawadia kampuni hizi Leseni ya Rais ya kuua wanyamapori 704 bure wakati kisheria zilikuwa hazistahili. Aidha, Nyalandu aliamua kukiuka kwa makusudi Sheria za Ugawaji Vitalu na kuzipa vitalu zaidi ya idadi inayoelekezwa na sheria, achilia mbali kwamba vitalu hivi alinyang’anya kutoka kwa kampuni nyingine zilizogawiwa kihalali na moja ya alichokiita kitalu (Mwiba Ranchi) hakikuwa kimekidhi sifa ya kuitwa kitalu kutokana na kuwa chini ya kilometa 200 za mraba. 

Katika Leseni ya Rais iliyotolewa kwa watu ambao hawana hadhi ya kupewa leseni hiyo, Nyalandu aliruhusu watoto wadogo chini ya miaka 15 kuwinda, kinyume cha sheria za nchi. Hili alilifanya siku chache tu baada ya kuifungia kampuni ya mzawa kwa madai ya kutenda kosa hilo hilo. 

Uanzishwaji wa Ranchi ya Mwiba ni moja ya vitendo vya dhahiri vya ufisadi na uchafu ambavyo vilitekelezwa kibabe na Nyalandu akiwa na washirika wake.

 

Wajitwalia kitalu kibabe  

Juni 24, 2013 Rais Barack Obama, alipelekewa barua ikimtaka aingilie suala la kampuni ya Kimarekani ili iendelee kumiliki kitalu isichostahili. Barua iliyosainiwa na wabunge 18 wa Bunge la Marekani, ilieleza kuwa FCF hawatendewi haki na Idara ya Wanyamapori ya Tanzania na kutaka kuingilia kati suala hili ili kulinda maslahi ya wawekezaji kutoka Marekani. 

Friedkin Group inamiliki kampuni mbili za uwindaji nchini Tanzania –  Tanzania Game Trackers Safaris (TGTS) Ltd na Wengert Windrose Safaris (WWS) Ltd. Kampuni zote ziliomba vitalu vya uwindaji kwa msimu wa mwaka 2013-2018 ambako TGTS ilipata vitalu vitano (5) vya uwindaji wa kitalii na WWS walipata viwili (2). Kabla ya hapo, msimu uliotangulia, kampuni hizi mbili zilipata vitalu 14 vya uwindaji wa kitalii.

Kutokana na mgawo mpya, TGTS na WWS hawakufurahishwa na hivyo wakaomba rufaa ya mapitio kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Januari, 2012. Rufani yao iliwasilishwa kwa Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii kwa maoni na mapendekezo. Kimsingi, kampuni hizi zilitaka kujua kwanini hazikupewa vitalu zilivyoomba kikiwamo cha Lake Natron Game Controlled Area (North) ambacho sasa kinajulikana kama Lake Natron Game Controlled Area (East). 

Ijulikane kuwa tayari TGTS walikuwa wameshafikisha idadi ya vitalu ambavyo kampuni moja inaruhusiwa kuvimiliki kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na.5 ya mwaka 2009 chini ya kifungu 38(7)1. Kwa upande mwingine, WWS ilipewa vitalu vitatu kati ya vitano ilivyoomba; na hiyo ilisababishwa na ushindani mkali uliokuwapo. Ushindani ulikuwa mkali kutokana na matakwa ya Sheria, Kifungu 39(3)(b), ambacho kinasema asilimia 15 pekee ya vitalu vya uwindaji wa kitalii ndiyo inayopaswa iwe kwa kampuni za kigeni. 

Kampuni zote mbili zikaandika rufani zikiomba mapitio ya waziri, ambaye naye kwa mara nyingine akawasilisha kwa Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu vya Uwindaji.

Kwa mara nyingine ikaonekana hakuna sababu ya kisheria ya kuzinyang’anya kampuni nyingine vitalu na kuipatia WWS.

Kwa mujibu wa sheria, WWS walitakiwa waondoke katika kitalu cha Lake Natron GCA (East) kuanzia Machi 31, 2013; muda ambao ulikuwa wa mwisho kwa uwindaji. Hata hivyo, hawakutaka kuheshimu matakwa hayo ya kisheria. Badala yake wakaamua kwenda mahakamani, ikiwa ni kuonesha kwamba hawakuridhishwa na uamuzi wa mara mbili uliofanywa kupitia mapitio ya Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo, Balozi Khamis Kagasheki.

Mahakama ikatoa uamuzi uliowabwaga WWS. WWS wakarejea tena kwa Waziri wa Maliasili na Utalii wakimtaka awape kitalu ambacho Kampuni ya Green Miles imepewa kisheria.

Waziri wa Maliasili na Utalii akamwagiza Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kuitisha mkutano wa wadau wote kujadili suala hilo. Nyaraka zote, ikiwa ni pamoja na ripoti ya Chuo cha Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), barua za ugawaji vitalu zikawasilishwa na kubainika kuwa madai ya WWS si halali. WWS wakawasilisha ramani iliyoghushiwa ambayo walidai kuwa wameipata kutoka TAWIRI. Nyaraka zilihusu uthaminishaji vitalu uliofanywa na TAWIRI kwenda kwa Mkurugnzi wa Idara ya Wanyamapori, matangazo kwa umma ya kukaribisha maombi ya vitalu vya uwindaji, barua za mgawo wa vitalu na ramani za vitalu vyote. 

Ripoti ya TAWIRI ya Februari 2011 ilikuwa na saini ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kila ukurasa. Ripoti hiyo ilikuwa na ramani kuonesha vitalu upande wa kaskazini iliyosomeka “Lake Natron GCA (North-South)” ilhali upande wa mashariki ulisomeka Lake Natron GCA (North). Ikasisitizwa kuwa huo ndiyo uliokuwa msingi wa mapendekezo ya mabadiliko ya majina ili kuonesha uhalisia wa kijiografia wa mahali kilipo kitalu badala ya majina ambayo yalikuwa yakisababisha mkanganyiko.

Licha ya ufafanuzi wote huo, WWS waliendelea kusisitiza kuwa wao ndiyo wenye haki ya kitalu walichohodhi.

Mkurugenzi Mtendaji wake akawasilisha ramani aliyodai ameipata TAWIRI. Alipoulizwa hatua alizotumia kuipata kutoka TAWIRI, wakati TAWIRI wakiwa hawana mamlaka ya kutoa ramani kwa kampuni za uwindaji wa kitalii, akasema alifanya hivyo kwa vile Idara ya Wanyamapori haikumpa ramani. 

Hata hivyo, ukweli ni kuwa WWS na kampuni yake dada ya TGTS walipewa ramani zote za vitalu vya uwindaji kutoka Idara ya Wanyamapori. WWS wakaonywa kwa tabia yao ya kujitwalia nyaraka kutoka mamlaka zisizoruhusiwa kisheria, na kuambiwa kuwa kitendo hicho si tu kuwa ni ukiukwaji wa maadili, bali pia ni uvunjaji wa sheria.

Baada ya majadiliano marefu, mwafaka haukufikiwa kwa vile WWS walisisitiza lazima wapewe kitalu ambacho kinamilikiwa kihalali na Green Miles.

WWS wakaamua kwenda mahakamani tena. Wakafungua kesi mbili mpya (Misc. Commercial Case No. 26 ya 2013 na Misc. Land Application Na. 44 ya 2013). Pamoja na hatua hiyo, wakawa wanahamasisha jamii iliyo kando ya Lake Natron GCA kupinga uwepo wa Green Miles. WWS wakashiriki kuhatarisha maisha ya watalii kwa kuchimba mashimo kwenye kiwanja cha ndege, kuziba barabara kwa mawe na miti na kuwafukuza watalii kwa kutumia magari kwa nia ya kuwagonga. 

Green Miles Safaris Ltd ni kampuni ya Tanzania, na si ya Falme za Kiarabu kama inavyopotoshwa na FCF.

Kutokana na madai yao ya upotoshaji, inaonekana kuwa Lake Natron GCA (North-South) ni kitalu pekee katika eneo hilo la uwindaji. Ukweli ni kuwa Pori Tengefu la Lake Natron kuna vitalu vinne vya uwindaji wa kitalii vilivyogawiwa kwa kampuni nne tofauti zikiwamo WWS na Green Miles Safaris. WWS wanapenda wao ndiyo wawe katika eneo hilo lote, likiwamo la Green Miles Safaris.

Kwa mujibu wa Sheria, Kifungu cha 38(7), kwa vyovyote vile, kampuni (mtu) moja haitapewa vitalu vya uwindaji wa kitalii zaidi ya vitano.

Waziri wa Maliasili na Utalii ana mamlaka kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 na Kanuni za Uwindaji za mwaka 2010 kugawa vitalu (siyo ardhi) kwa kampuni ya uwindaji kwa muda wa miaka mitano. Vitalu vyote vya uwindaji ni mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na ndiyo maana mwekezaji haruhusiwi kuwa na majengo ya kudumu katika kitalu. Kwa hiyo, ni kosa kwa kampuni yoyote kudai kuwa ina umiliki wa kitalu cha uwindaji baada ya muda wa miaka mitano kumalizika. 

Aidha, hakuna dhamana ya kwamba mtu au kampuni iliyopewa kitalu cha uwindaji msimu huu, itapewa kitalu hicho hicho msimu ujao. Ndiyo maana kampuni zote, zikiwamo zile zilizokuwa katika vitalu hivyo hutakiwa kuomba upya kwa msimu unaofuata.

Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu vya Uwindaji na Mahakama ni vyombo huru na kwa maana hiyo havipo chini ya maofisa wanyamapori au Idara ya Wanyamapori Tanzania.

Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii ilipitia mara mbili suala hili na kujiridhisha kuwa ugawaji ulifanyika kihalali. Mahakama pia ililiona hilo na ndiyo maana ikatoa hukumu dhidi ya WWS. Mara zote WWS, kwa makusudi, imekuwa haitaki kueleza uamuzi huu wa vyombo hivi viwili, badala yake imekuwa ikiwasingizia maofisa wadogo wa wanyamapori kwamba wameipatia kinyemela kampuni ya Green Miles Safaris hivyo vitalu. 

Waziri alishatoa uamuzi wake kulingana na ushauri wa Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii. Ni wazi kuwa WWS hawakufurahishwa na uamuzi wa Waziri Kagasheki na ndiyo maana wakaamua kwenda mahakamani ambako nako walishindwa mara tatu, na juzi wameshindwa kwa mara ya nne. 

 

Kwanini wanang’ang’ania kitalu hiki?

WWS wameshawahi kutoa ofa kwa Green Miles ili wakinunue kitalu hicho kwa dola 600,000 za Marekani (shilingi zaidi ya bilioni 1 kwa wakati huo). Green Miles wakakataa, lakini wakawa tayari kuwauzia safari WWS. WWS wakasisitiza kuwa wanachotaka ni kitalu na si kitu kingine. Baada ya kuona wamefeli kukipata kitalu, ndipo walipoanza kufanya hujuma za kila aina, lengo likiwa kuhakikisha wanakipata.

Uadui wa kampuni hizi mbili ukafika hadi Reno-Nevada, Marekani mnamo Januari 2013 ambako WWS kwa kutumia ushawishi wao kama Wamarekani, wakamfukuza Mkurugenzi Mtendaji wa Green Miles kutoka kwenye maonesho. GMS wakapeleka malalamiko kwa waandaaji wa maonesho hayo ya Safari Club International-SCI’ ambao walifanikiwa kuingilia kati na kutuliza mambo.

Baada ya juhudi zote zilizolenga kuwafanya watwae kitalu cha Lake Natron Game Controlled Area (East), WWS wakaibuka na tuhuma dhidi ya maofisa wa Idara ya Wanyamapori wakisema wanacheza ‘mchezo mchafu’ kwamba wamebadili majina ya vitalu ili wapewe Green Miles. Idara ya Wanyamapori ikatoa taarifa kuonesha kuwa mabadiliko yaliyofanywa hayakulenga Lake Natron pekee, bali vitalu vingi vikiwamo vilivyoko kwenye Pori la Akiba la Selous. 

Kubadilishwa kwa majina ya vitalu kulitoka na ukweli kuwa majina ya awali hayakuwasilisha uhalisia wa mahali vilipo kijiografia. Pia ilielezwa kuwa mabadiliko hayo kwa namna yoyote yasingeweza kuathiri mahali kilipo kitalu na ukubwa wake. 

Awali, WWS walipewa barua ya kitalu na ramani – Lake Natron GCA (North-South) ambacho kilikuwa kimependekezwa kiitwe Lake Natron GCA (North) kutokana na kuwa kaskazini.

Hata hivyo, kwa kuwa lengo lao ni kupata Lake Natron GCA (North) –   iliyopendekezwa iitwe East – kwa namna yoyote ile, WWS hawakuwa tayari kuukubali uhalisia na ukweli, hivyo wakaamua kudanganya kuwa hawakupewa ramani yoyote kutoka mamlaka husika.

Kwa mujibu wa sheria, WWS walitakiwa waondoke katika kitalu cha uwindaji cha Lake Natron GCA (East) Machi 31, 2013 ambayo ni tarehe ya mwisho ya msimu wa uwindaji, na mwisho wa leseni yao katika eneo hilo. 

Baada ya uamuzi wa Mahakama kupuuzwa, wamiliki halali wa kitalu – kampuni ya Green Miles – walilalamika kwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wakisema walishindwa kujenga kambi kwa vile WWS walikuwa bado wamekalia kwa mabavu kitalu hicho.

Mei 20, 2013 Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori aliwaandikia WWS barua akiwapa notisi ya kuondoka katika kitalu hicho ndani ya siku tatu. WWS wakapuuza amri hiyo.

Badala yake, Mei 23, 2013 ujumbe wa WWS ukarejea kwa Waziri Kagasheki ukisisitiza kukichukua kitalu hicho cha Lake Natron (East) (ambacho awali kiliitwa Lake Natron North). Aidha, wakamtaka Waziri afute amri ya siku tatu waliyopewa na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori.

Kimsingi, kwa miaka mingi WWS na TGTS wamekuwa wakaidi na wenye kiburi, si tu kwa maofisa wa Serikali, bali hata kwa wawekezaji wengine katika tasnia ya uwindaji wa kitalii. Tabia hizi zimeoneshwa katika maeneo tofauti ambako wamekuwa wakiendesha shughuli za uwindaji kama vile kwenye Mapori ya Akiba ya Selous, Rungwa, Ugalla na Pori Tengefu la Lake Natron na Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Makao.

Mbali ya mgogoro unaoendelea Lake Natron, kampuni dada ya WWS, yaani TGTS ilikuwa kwenye mgogoro mkubwa na kampuni ya Fereck Safaris katika eneo la Makao WMA. TGTS, kupitia Mwiba Holdings, iliingia kinyume cha sheria na kujenga kambi katika eneo la kitalu cha uwindaji la Fereck Safaris Ltd. Kampuni ya Fereck ilishalipa ada zote za kitalu na kuanza kutekeleza ahadi zake kwa wanajijiji kwa mujibu wa mkataba. 

TGTS iliondolewa kwenye mchakato wa maombi ya kumpata mwekezaji kwa kitalu cha Makao WMA. Kampuni hiyo ya Wamarekani ilipata alama 50; wakati washindani wake, yaani Fereck Safaris walipata 86. TGTS, ambao hawakuwa na mkataba na WMA, hawakuwa na kibali cha kuwawezesha kufanya shughuli eneo hilo; hata hivyo walianza kufanya utalii wa picha na mara kadhaa wafanyakazi wake walikamatwa wakiwa wameua wanyama kinyume cha sheria. Kibaya zaidi, shughuli hizo walikuwa wakizifanya kwa uangalizi wa polisi; jambo lililozidi kutia shaka. Baada ya kuandamwa, Fereck Safaris walisalimu amri.

Rekodi za Wizara ya Maliasili na Utalii zinaonesha kuwa Julai 16, 2013 aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa, alimwandikia barua nyingine Mkuu wa Kanda, Kikosi Dhidi ya Ujangili Kanda ya Kaskazini, akimtaka aiondoe mara moja kampuni ya WWS kwenye Kitalu cha Lake Natron East kinachomilikiwa kihalali na Green Miles.

“Wizara imepokea malalamiko kutoka kwa Afisa Wanyamapori Wilaya ya Longido pamoja na mwekezaji aliyegawiwa kitalu cha Lake Natron Game Controlled Area East kwamba kampuni ya Wengert Windrose Safaris Limited inafanya fujo na kuvuruga shughuli za uwindaji wa kitalii zinazoendelea katika kitalu hicho.

“Suala hili si tu kwamba linakosesha Serikali mapato, bali pia linaleta hasara kwa mwekezaji halali wa eneo hilo na kuvuruga tasnia ya uwindaji nchini. Kuna hatari tukafikishwa mahakamani na tuliyemgawia kitalu kutudai fidia.

“Kwa kuwa Kampuni ya Wengert Windrose Safaris Limited hadi sasa imeshindwa kulipia ada za kitalu ilichogawiwa cha Lake Natron Game Controlled Area North, na pia imekaidi kutii maagizo ya Idara ya kuitaka kuondoka katika kitalu cha Lake Natron Game Controlled Area East yaliyotolewa kupitia barua Kumb. Na. HD 27/519/01/116 ya tarehe 16 Mei, 2013 unaagizwa kuhakikisha kwamba Kampuni ya Wengert Windrose Safaris Limited inaondoka mara moja katika kitalu tajwa hapo juu na utoe taarifa ya utekelezaji wa agizo hili. Ikibidi shirikisha polisi,” ilisema barua hiyo iliyosainiwa na Profesa Songorwa.

Je, uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Tano utakubali kuburuzwa na Warekani hawa?