Brigedia Jenerali (mstaafu) wa JWTZ anayetimiza umri wa miaka 83
* Atoboa siri ya mafanikio yake
Kesho ni siku muhimu kwa Brigedia Jenerali (mstaafu) Francis Xavier Mbenna, anayetimiza umri wa miaka 83 ya kuzaliwa. Mwanajeshi mstaafu huyu, mkazi wa jijini Dar es Salaam, alizaliwa Julai 31, 1930 huko Likese Masasi, mkoani Mtwara.
Alisoma katika shule za msingi Nandembo, Tunduru mwaka 1942-1943, Ndanda 1944-1945, Peramiho 1946-1947. Januari 1948 alijiunga na Shule ya Sekondari ya St. Mary’s W.F ya Tabora na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1951. Alifaulu mtihani uliomwezesha kwenda kusoma katika Chuo cha Cambridge.
Alipata mafunzo katika Chuo cha Ualimu Ihungo, Bukoba kati ya mwaka 1952 na 1953 na baadaye katika Chuo Kikuu Hull, Yorkshire nchini Uingereza mwaka 1960 hadi 1961. Alifundisha katika Shule ya Abbey School Ndanda mwaka 1954 hadi 1960, Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Songea mwaka 1960 hadi 1964 akiwa mkuu wa shule hiyo.
Pia alipata nafasi ya kufanya kazi katika kambi mbalimbali za Jeshi la Kujenga Taifa za Mgulani, Mafinga, Oljoro, Buhemba, Ruvu na Makao Makuu ya JKT. Alikuwa Kamanda wa JKU Zanzibar (1978-1980) na ametumikia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) (1982-1988) akiwa Kamisaa na Brigedi Kamanda na Mkuu wa Idara ya Elimu Ngome.
Alishika vyeo mbalimbali na hatimaye kupandishwa kuwa Brigedia Jenerali kabla ya kustaafu kwa umri Juni 30, 1988. Amepata kuwa mwenyekiti wa Kamati ya JWTZ ya uteuzi wa maofisa kadeti kati ya mwaka 1996 na 2003, Mjumbe wa Bodi ya Korosho (1999-2002), Mjumbe wa Mfuko wa Pembejeo (2002-2005).
Brigedia Jenerali mstaafu Mbenna pia ni mjumbe katika bodi ya shule za Milenia tangu mwaka 2002 hadi sasa. Pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Saidia Wazee Tanzania (SAWATA) Taifa. Pia ni Mwenyekiti wa Tanzania Age Care Organization (TANACO) Taifa.
Brigedia Jenerali huyu kwa sasa ni mwandishi katika moja ya Safu za gazeti hili (JAMHURI). Lakini pia hivi karibuni aliadhimisha miaka 58 ya ndoa yake. Kutokana na historia ndefu na yenye mafanikio, gazeti hili lilimfuata na kutaka kujua siri ya mafanikio na changamoto alizokumbana nazo katika maisha.
JAMHURI: Hongera sana. Nini siri ya mafanikio hadi umetimiza miaka 83 ya kuzaliwa ukiwa bado na mwonekano kama wa kijana?
BRIGEDIA JENERALI (MSTAAFU): Kuna vitu vingi ambavyo vinachangia mpaka unaona ninaonekana kama hivi nilivyo. Kwanza kibailojia binadamu ana matezi hapa shingoni ambayo yanatoa vichocheo kwa ajili ya ukuaji. Akiwa na vichocheo vingi basi utaona mtu anafumuka na kuwa na mwili mkubwa. Lakini vichocheo vikiwa kidogo basi pia utaona binadanu anakuwa katika hali ya kawaida.
Mbali na hizo sababu za kisayansi lakini pia kuna namna ya kujitunza. Kwa mfano, mimi sinywi [pombe] wala sivuti [sigara/tumbaku]. Unajua ukinywa unakosa hamu ya kula, na kama huli huwezi kuwa na mwili mzuri kwa sababu kazi ya chakula ni kujenga mwili.
Jambo la tatu niseme kwamba mimi najishughulisha na kazi mbalimbali za kijamii. Kwa mfano, mimi ni Mratibu wa Vicoba katika eneo hili la Uwanja wa Taifa na nimetoa eneo langu kwa ajili ya kufanyia mikutano yetu ya mara kwa mara. Tuna vikundi vinne na kila kikundi kina watu 30.
Sizeeki ‘I am very active’ sina muda wa kukaa na kunung’unika au kulalamika lalamika na kukumbuka yaliyopita. Hali ya kunung’unika na kukumbuka yaliyopita ni mojawapo ya mambo ambayo yanaweza kumfanya mtu kuzeeka haraka.
JAMHURI: Una watoto wangapi?
BRIGEDIA JENERALI (MSTAAFU): Nilibahatika kupata watoto saba, wanne wametangulia mbele ya haki. Kwa sasa nina watoto watatu, wawili wa kike na mmoja wa kiume. Mke wangu anaitwa Maura, ana umri wa miaka 78, kama unavyomuona pale na yeye anaonekana bado kijana kama mimi. Nina wajukuu tisa na vitukuu wanne.
JAMHURI: Unaona tofauti gani kati ya maisha ya sasa na yale ya kwenu mkiwa bado vijana?
BRIGEDIA JENERALI (MSTAAFU): Zamani tulikuwa na maisha ya kujitegemea zaidi kwa sababu fedha hazikuwapo tofauti na ilivyo sasa. Mimi nakumbuka wakati nasoma sekondari mwaka 1943 niliwahi kutembea kwa miguu kutoka Tunduru hadi Masasi nikielekea shule, mwendo wa maili 125, Songea hadi Njombe mwaka 1947.
Maisha ya sasa yamekuwa ya kuiga, vijana nao wamekosa maadili, wanapenda Uzungu na ubinafsi, matokeo yake hakuna uchungu na nchi. Nakumbuka mimi nikiwa mwalimu tulikuwa tunafundisha ili watoto wetu wafaulu vizuri na hatimaye shule yetu ipate sifa. Siku hizi ni twisheni tu. Watoto wa sasa wanapenda kuwatawala wazee na hasa pale anapokuwa na uwezo wa kifedha. Hii inatufanya wazee tuone uchungu.
Tunaishi maisha ya kutokuwa na msimamo, tukiwa na msimamo ndipo tutakapokuwa na maadili ya kitaifa. Hivi kwa mfano, liko wapi vazi la kitaifa? Je, kuna haja ya kuunda kamati ya kutafuta vazi la kitaifa? Ukienda Unguja na Pemba utakuta vazi la koti na kanzu kwa mwanaume na baibui kwa wanawake. Hii ni ‘style’ ya mavazi ya Unguja na Pemba na hata kama wameiga kwa Waarabu lakini bado wana vazi linaloweza kuwatambulisha kama watu wa eneo fulani.
Sioni haja ya sisi kung’ang’ania mavazi yenye maandishi ambayo mengine hatujui maana yake, mengine yanatudhalilisha na tunadhalilika bila kujua.
JAMHURI: Nini kifanyike ili kurudisha hali hii ya uzalendo?
BRIGEDIA JENERALI (MSTAAFU): Kwanza Watanzania tunatakiwa kuwa na ile hali ya uzalendo. Lakini pia mahali pengine pa vijana kupatia uzalendo ni kupitia JKT. Hii ni sehemu ambayo kwa kiasi kikubwa inaweza kutoa vijana wenye uchungu na nchi yao na hivyo, kurejesha hali ya uzalendo.
JAMHURI: Unaonekana mtu wa kujishughulisha na uandishi, hili nalo likoje?
BRIGEDIA JENERALI (MSTAAFU): Ni kweli, uandishi ni kitu ambacho nakipenda na hasa pale ninapokuwa nimekaa na kutulia sehemu fulani.
JAMHURI: Unapendelea burudani gani katika maisha yako?
BRIGEDIA JENERALI (MSTAAFU): Napendelea mpira wa miguu. Nakumbuka wakati nilipokuwa shule nilikuwa mchezaji mzuri wa nafasi ya mlinzi wa kulia na niliwahi kuwa kocha wa timu ya shule kule Ndanda na Songea Boys.
Timu yangu katika Ligi ya Uingereza ni Manchester United, na hapa nyumbani [Tanzania] timu yangu ni Majimaji ya Songea. Nakumbuka kuna wakati fulani nikiwa Arusha, Majimaji walikuja Arusha kucheza nikawakaribisha vizuri sana.
Najua utanishangaa kidogo kwa hili, mimi ushabiki wangu ni wa kizalendo zaidi “I am very conservative”. Kama nilivyosema awali Watanzania wengi hatuna uzalendo na vitu vyetu, na kwenye soka hali ni ile ile hakuna ushabiki wa kizalendo.
Mbali ya soka napendelea muziki na nilikuwa kiongozi wa Bendi ya JKT Kimbunga. Ilikuwa ni mwaka 1965 ambapo nawakumbuka wanamuziki wa bendi hiyo kama John Simon (mwimbaji) na mpiga gitaa la solo, Saidi Vinyama. Wengine nilishawasahau.
JAMHURI: Mpaka kufikia umri huu umepata kutembelea nchi gani?
BRIGEDIA JENERALI (MSTAAFU): Nimewahi kutembelea nchi kama India, Bulgalia, Uigereza, Amerika ya Kusini, Zambia, Zimbabwe na Vatican ambapo nilikutana na Papa John Paul. Kwa sasa nikipata hela nina mpango wa kwenda kuhiji huko Lourdes nchini Ufaransa.