Serikali imejenga vituo vya kutoa huduma kwa pamoja mipakani (OSBPs) vinavyolenga kurahisisha taratibu za Forodha, Uhamiaji, usimamizi wa ubora wa bidhaa na huduma, ulinzi na usalama kwa watoa huduma hizo upande mmoja wa mpaka kwa nchi mbili husika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Joseph Nyamhanga, ameieleza JAMHURI kwamba ujenzi wa vituo hivyo utarahisisha biashara na usafirishaji kati ya Tanzania na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Soko la pamoja kwa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA).
Mhandisi Nyamhanga anasema ujenzi wa vituo hivyo ni juhudi za Serikali za kupunguza vikwazo visivyo vya kiforodha (NTBs), ili kurahisisha biashara na usafirishaji wa magari makubwa yanayosafiri kwenda nje ya nchi, kwa taratibu za kujenga vituo vya ukaguzi wa pamoja katika Ukanda wa Kati maeneo ya Vigwaza mkoani Pwani, Manyoni mkoani Singida, na Nyakanazi mkoani Kagera.
Anasema Vituo vya Ukaguzi wa Pamoja (OSIS) katika Ukanda wa Dar es Salaam ukihusisha barabara kuu za Dar es Salaam hadi Tunduma (mpaka wa Tanzania na Zambia), na Uyole hadi Kasumulu (mpakani mwa Tanzania na Malawi), ambako kutakuwa na vituo vinne ambavyo ni Vigwaza mkoani Pwani, Mikumi mkoani Morogoro, Makambako mkoani Njombe na Mpemba mkoani Songwe.
Hata hivyo, anasema vituo hivyo vya ukaguzi wa pamoja vitakuwa na mizani, vituo vya polisi, vituo vya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na maeneo ya kupumzika kwa madereva wa magari makubwa yanayosafiri kwenda nje ya nchi.
“Wakati wa ufunguzi wa daraja la Rusumo na kituo cha kutoa huduma kwa pamoja mipakani katika eneo la Rusumo mpakani mwa Tanzania na Rwanda, Aprili 6, mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, aliagiza kwamba magari makubwa yanayosafiri kwenda nje ya nchi yapimwe uzito katika vituo vya mizani vya Vigwaza mkoani Pwani, Njuki mkoani Singida na Nyakahura mkoani Kagera,” anasema Nyamhanga.
Anasema vituo ni kwa magari yanayotumia barabara kuu ya Ukanda wa Kati (Central Corridor) kuelekea nchini Rwanda na Burundi. Kwa magari yaendayo nchini Uganda kupitia Ukanda wa Kati yatapimwa uzito katika vituo vya mizani vya Vigwaza, Njuki na Kyamyorwa mkoani Kagera.
Kutofautisha magari makubwa na mabasi yanayosafiri kwenda nje ya nchi na yale yanayofanya safari zake nchini anasema Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imeandaa ‘stickers’ maalumu ambazo zitatumika kutambulisha magari yaendayo nje ya nchi katika vituo vya vya mizani.
Anasema ‘stickers’ hizo zitaoneshwa hivi karibuni baada ya kuzichapisha. Hata hivyo, Serikali inakusudia kuweka mfumo wa kielektroniki wa kuyatambua magari hayo katika vituo vya mizani badala ya ‘stickers’. Takwimu za wizara hiyo zinaonesha kwamba zaidi ya asilimia 62 ya magari makubwa yanayopita kwenye mizani yakiwa kwenye mwendo eneo la Vigwaza, yanaruhusiwa kupita bila kupima kwenye mizani kubwa hivyo uwepo wa mizani ya aina hiyo katika vituo vingine hautakuwa vikwazo kwa magari makubwa yanayosafiri kwenda nje ya nchi.
Pamoja na hayo, kuna idadi ya mizani mbili tu, moja ikiwa eneo la Vigwaza mkoani Pwani, na nyingine eneo la Mikese mkoani Morogoro, zinazopima uzito magari yakiwa katika mwendo (weigh-in-motion).
Nyamhanga anasema iwapo gari lililobeba mzigo unaosafirishwa nje ya nchi litapima kwenye mizani inayopima magari yakiwa kwenye mwendo na kuonekana limezidi uzito, na kuelekezwa na taa za barabarani kwenda kwenye mizani kubwa inayopima magari yakiwa yamesimama, dereva anatakiwa kutii maelekezo hayo.
Jitihada zinazofanywa na Serikali za kujenga vituo vya kutoa huduma kwa pamoja mipakani, utarahisisha huduma kuwafikia wananchi kwa haraka na kuinua uchumi kwa nchi husika.