KARATU

Na Bryceson Mathias

Mtoto mwenye umri wa miaka minne, Asteria Petro, amejeruhiwa na fisi katika Kata ya Basodawish, Karatu mkoani Manyara, akiwa ni wa 28 kukumbwa na kadhia hiyo, hivyo kuzua hofu miongoni mwa wananchi.

Taarifa zinasema kwamba fisi huyo wa ajabu amekuwa akila watu, hasa watoto, wenye umri kati ya miaka mitatu hadi saba huku tukio la hivi karibuni linalohusisha kujeruhiwa kwa Asteria likitokea Mei 4, 2022 mbele ya mama yake mzazi aliyekuwa akifanya shughuli za nyumbani.

Baba wa mtoto huyo, Petro Sanka, ameliambia JAMHURI kuwa tukio hilo lilitokea wakati Asteria akicheza na pacha wake maeneo ya nyumbani kwao.

“Ghafla mtoto akalia akimwita mama yake kwamba ‘fisi anakuja!’ Mama akadhani kuwa ni mbwa wao. Mara fisi akakamata kichwa cha mtoto na kukimbilia porini.

“Kelele za mama yake ndizo zilizaa msaada baada ya watu kujitokeza na kumkimbiza fisi huyo ambaye alimwacha mtoto na kutokomea porini,” amesema Sanka.

Serikali wilayani Karatu imewahi kuwaahidi wananchi wa Basodawish kuwa ingeunda kikosi kazi maalumu kikihusisha askari wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara, Mamlaka ya Uhifadhi wa Bonde la Ngorongoro na askari wa wanyamapori wa halmashauri kumsaka fisi huyo, lakini ahadi hiyo haijatekelezwa.

Asteria kwa sasa anaendelea na matibabu huku hali yake ikiimarika.

Aprili 24, mwaka huu, Sanka aliahidi kutoa tripu mbili za mawe kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha watoto cha kata kusaidia ulinzi na matunzo ya watoto dhidi ya wanyama wakali.

“Nilitoa kama sadaka na ninaamini nami sadaka hiyo ndiyo imemnusuru mwanangu dhidi ya kifo cha kusikitisha kwa kuliwa na fisi,” amesema.

Sanka amemshukuru Mchungaji wa KKKT Usharika wa Bassadawish, Jimbo la Karatu, Robert Temba, kwa msaada mkubwa wa matibabu ya Asteria alipolazwa Hospitali ya Mount Meru jijini Arusha.

Hili ni tukio la 28 ndani ya miaka mitatu kwa watoto wa eneo hilo kukamatwa na kushambuliwa na fisi; mabaki ya watoto saba kati yao (vichwa au sehemu za miili) yamezikwa huku wananchi wakibaki kujiuliza adha hii ya aibu itakwisha lini.

“Ni hofu tupu. Watu wanashindwa hata kufanya shughuli za maendeleo. Sisi kama kanisa tunajitahidi kukamilisha ujenzi wa kituo cha watoto kiwe sehemu ya ulinzi na eneo zuri la kuwalea ili wazazi wapate nafasi ya kufanya shughuli zao kwa amani,” amesema Mchungaji Temba.

Amesema matukio saba ya aina hiyo yametokea Basodawish peke yake, mawili yakigharimu uhai wa watoto. 

Mengine manne yametokea Kijiji cha Shangt; watoto wawili wakifariki dunia na wawili kujeruhiwa. 

“Pia mtoto mmoja wa Kijiji cha Endamarariek aliuawa na fisi huku mwingine akijeruhiwa, ambapo katika Kijiji cha Gidbaso yametokea matukio kadhaa ingawa hakuna mtoto aliyejeruhiwa,” amesema Mchungaji Temba. 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Basodawish, Meta Bare, amesema kwa namna ya matukio yalivyo, inaonekana kuwa fisi anayehusika ni mmoja tu.

“Huyu fisi anasumbua kata nzima ya Endamarariek. Hivi tunavyozungumza kuna mtoto mwingine yupo Kituo cha Afya cha Fame, Karatu, kwa ajili ya upasuaji baada ya kujeruhiwa na fisi,” amesema Bare.

Diwani wa Endamarariek, John Mahu, ameliambia JAMHURI kuwa siku nzima ya Jumamosi iliyopita amekuwa na vikao mfululizo na viongozi wa kimila wa Karatu kutafuta suluhu ya kadhia hiyo.

“Wazee wameahidi kutoa jibu ndani ya siku mbili hizi. Hata jana tu (Ijumaa iliyopita), fisi huyo ameonekana akimvizia mtoto aliyekuwa akiogeshwa na mama yake. Mambo ya ajabu kabisa,” amesema Mahu.