Wananchi wa Kijiji cha Chiwambo mkoani Mtwara wamemuua fisi wa silaha za jadi baada ya kuvamia nyumbani kwa mkazi mmoja wa kijiji hicho wakati wakiota moto ndani.
Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho, Maimuna Mbaya amesema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa saba usiku baada ya fisi huyo kuvamia kwenye familia marehemu Haika Mangeja (62).
Amesema kuwa wakati marehemu Mangeja na mke wake, Asina Nguriko (49) wakiota moto ghafla fisi huyo aliwavamia na kuanza kumjeruhi mke wa marehemu.
Amesema kuwa kutokana na kitendo hicho marehemu alianza kumuokoa mkewe lakini kwa bahati mbaya fisi aliacha kupambana na mwanamke huyo na kuanza kumshambulia marehemu.
Amesema mwanamke huyo alipiga kelele za kuomba msaada ndipo wananchi walifika na kuanza kumsaka fisi huyo.
Amesema kuwa katika harakati za kumtafuta porini ndipo walipomkuta fisi huyo akiwa anakula mwili wa marehemu eneo la kichwani na kumuua kwa kutumia silaha za jadi.