Tunahitaji rais dikteta mwenye uzalendo
Jumamosi iliyopita wakati jua likielekea kuchwea, nilihisi faraja kuandaa makala hii kutoa changamoto kwamba nchi yetu sasa inahitaji kuwa na rais dikteta lakini aliye mzalendo. Dikteta ni mtu anayetawala nchi kwa amri zake bila kushauriwa, au anayetaka analosema litekelezwe bila kupingwa, na mzalendo ni mtu anayependa nchi yake kiasi cha kuwa tayari kuifia.
Fikra ya Hekima inaamini kuwa rais wa aina hiyo anaifaa nchi hii kwani ataiwezesha kupiga hatua kubwa ya maendeleo kutokana na utajiri wa rasilimali lukuki tulizojaliwa na Mwenyezi Mungu.
Tunahitaji rais mwenye ujasiri wa kufanya uamuzi mgumu dhidi ya watendaji wabovu ili kuimarisha matumizi sahihi ya rasilimali zilizopo ziweze kuwanufaisha wananchi wote badala ya kuendelea kuwaneemesha ‘wajanja’ wachache.
Kwamba ifike mahali dhahabu, almasi, Tanzanite, vivutio vya utalii kwenye hifadhi za wanyamapori, ndege, mimea, maziwa, mito, milima na misitu vitumike kuinua uchumi wa Watanzania kuanzia ngazi ya kaya.
Kiongozi wa nchi ambaye ni dikteta mwenye uzalendo siku zote hahitaji ushauri wa watu wengine katika kuwaadhibu watendaji wa serikali wanaotumia madaraka vibaya ikiwa ni pamoja na kuhujumu mali za umma.
Ukielezwa kwamba umaskini wa Watanzania ni wa kujitakia usipoteze muda kupingana na hilo. Viongozi wasio waadilifu ndio chanzo kikuu cha umaskini unaowatafuta wananchi wengi. Dawa thabiti ya viongozi wa aina hiyo ni rais dikteta mwenye uzalendo.
Nchi ya watu wastaarabu haihitaji rais dikteta lakini Tanzania inahitaji rais wa aina hiyo awadhibiti watendaji wa serikali ambao ni miunguwatu na wanaokwaza juhudi za kuboresha maisha ya wananchi kwa kujihusisha na ufisadi.
Leo wananchi maskini hawana chao Tanzania. Maisha mazuri yameendelea kujikita kwa viongozi wa ngazi za juu serikalini na matajiri wachache. Hayo ndiyo matabaka ya watu wachache wanaoendelea kufaidi rasilimali za nchi hii. Wananufaika na hudumza bora za elimu, afya, maji, usafiri, makazi, miongoni mwa huduma nyingine za kijamii.
Tajiri na shangingi lake, maskini na mkokoteni wake; ndio taswira inayoendelea kujidhihirisha Tanzania. Ni aibu kubwa taswira ya aina hii kuwakabili Watanzania wanaozungukwa na rasilimali nyingi.
Rais Mwai Kibaki wa Kenya aliwahi kusema “Uongozi ni fursa ya kuboresha maisha ya wengine, siyo nafasi ya kujinufaisha binafsi.” Watanzania tunahitaji rais atakayesimamia dhana hiyo kwa vitendo na dhati ya moyo.
Tunahitaji rais dikteta na mzalendo awe fagio la chuma dhidi ya wala rushwa na wahujumu uchumi wa nchi. Lakini pia asafishe uozo katika wizara za Maliasili na Utalii, Nishati na Madini, Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Viwanda na Biashara, Afya na Ustawi wa Jamii, Mambo ya Ndani ya Nchi, Uchukuzi, Kilimo, Chakula na Ushirika. Rais Jakaya Kikwete amejijengea umaarufu wa uvumilivu katika masuala ya utawala na siasa nchini. Ameruhusu uhuru mkubwa wa kila mtu kukosoa na kutoa mawazo yake kwa namna awezavyo. Dhana hii ni nzuri kwa taifa lenye watu wastaarabu, si vinginevyo.
Watendaji wa serikali wabadhirifu, wanasiasa na matajiri wanafiki wasio na uzalendo ndiyo chanzo kikuu cha Watanzania wengi kuweka kando dhana ya ustaarabu.
Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015 ni fursa nzuri ya Watanzania kufanya mageuzi ya kihistoria nchini kwa kuchagua rais dikteta aliye mzalendo. Hiyo ndiyo mbinu sahihi itakayoirejesha nchi yetu katika misingi ya uzalendo na mshikamano wa kweli.
Watanzania tuungane kutafuta rais dikteta mwenye uzalendo awe kiboko cha viongozi wabovu, wala rushwa na wahujumu uchumi, la sivyo umaskini utaendelea kuongezeka miongoni mwetu kwa kiwango cha kutisha. Tuamke.