Kagame, Museveni, mkataa wengi ni mchawi

Ndoto za Rais wa Rwanda, Paul Kagame, na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, kutaka kuzitenga nchi za Tanzania na Burundi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeyeyuka.

Sasa ushindi uko mikononi mwa UTATU MWAMINIFU (Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya).

Nchi tatu za Tanzania, Burundi na Kenya zinapokuwa na msimamo unaofanana katika EAC, ni dhahiri kuwa nchi mbili za Rwanda na Uganda hazitaweza kufanikisha chochote kinachoweza ama kuivunja, au kuidhoofisha Jumuiya hiyo. Hii ni sawa na kusema kwamba Kikwete, Nkurunziza na Kenyatta wamepangua mbinu za Kagame na Museveni zisizo na tija katika EAC.

Rais Kenyatta ameonesha mfano mzuri wa kuigwa kutokana na ujasiri wake wa kujitenga na maswahiba wake — Rais Kagame na Rais Museveni — waliokuwa na mtazamo wa kuzimwaga Tanzania na Burundi kutoka EAC. Awali Kenya ilionekana kuungana na Rwanda na Uganda kuzitenga Tanzania na Burundi katika baadhi ya masuala ya kimkataba yanayoihusu Jumuiya hiyo.

Kwa upande mwingine, Rais Kikwete anastahili pongezi nyingi kwa kutangaza msimamo wake kwamba Tanzania haitajitoa EAC, bali itaendelea kuwa mwanachama wake mwaminifu kwani tayari imeshatumia muda mrefu na gharama kubwa kuchangia maendeleo ya Jumuiya hiyo.

Akilihutubia Taifa hivi karibuni kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Kikwete alielezea kushangazwa na hatua ya Rwanda, Uganda na Kenya kuvunja makubaliano ya mkataba wa EAC na kuzitenga Tanzania na Burundi.

Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete alitaja maeneo manane ambayo mataifa hayo yameanza ushirikiano wa walio tayari (Coalition of the willing) na maeneo manne miongoni mwa hayo yanayovunja moja kwa moja makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.

Mambo hayo ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa-Kigali-Bujumbura-Sudan Kusini, ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya-Uganda-Sudan Kusini, ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta, ushuru wa forodha wa pamoja, kuharakisha shirikisho la kisiasa la EAC, viza ya pamoja ya utalii ya Afrika Mashariki, kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria, uzalishaji na usambazaji wa umeme wa pamoja.

Kati ya hayo, Rais Kikwete alitaja mambo manne yasiyogusa makubaliano ya pamoja ya EAC kuwa ni bomba la mafuta, kiwanda cha kusafisha mafuta, umeme na reli ya kisasa. Hata hivyo, Tanzania ina maslahi ya moja kwa moja katika miradi hiyo, lakini haijajua kwanini haikushirikishwa.

Rais Kikwete alisema huenda masuala ya uhamiaji, ardhi, ajira na kuharakisha shirikisho la kisiasa ambayo Tanzania imeyakataa kuwa sehemu ya EAC, ndiyo yaliyozisukuma Rwanda na Uganda kuitenga kwenye ‘ushirikiano wa walio tayari’. Lakini, katika kuonesha dhamira nzuri ya kukataa ubaguzi usiokuwa na tija katika EAC na uaminifu wake kwa Tanzania kama mwanachama halali wa Jumuiya hiyo, Rais Kenyatta alimtuma Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed, kutuliza hali ya mambo kufuatia hotuba hiyo ya Rais Kikwete.

Waziri Mohamed aliwasili hapa nchini hivi karibuni na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe. Alielezea msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Kenya wa kuunga mkono msimamo huo wa Rais Kikwete.

Katika mazungumzo yake na Waziri Membe, kwenye mkutano uliowashirikisha pia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri Mohamed alisema ziara yake hiyo inalenga kuonesha namna Kenya ilivyoguswa na kuridhishwa na kauli ya Rais Kikwete kuhusu EAC.

“Tumeipitia kwa tahadhari kubwa kauli ya Rais Kikwete kuhusiana na suala la shirikisho na tunakubaliana na hoja zake. Kama wanachama wa Jumuiya, tunaiunga mkono Tanzania kuhusiana na Jumuiya na tusingependa kwenda njia tofauti na Tanzania,” alisema Waziri Mohamed.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Kenya, aliihakikishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania kwa jumla kwamba nchi wanachama wa EAC hazitaitenga katika Jumuiya hiyo, kwani Tanzania ni moja ya zana muhimu zinazotegemewa na nchi nyingine ndani ya Jumuiya hiyo kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wote. Kama Waziri Membe alivyosema, Kenya imegutuka na kutambua kwamba ilikuwa imedanganywa kwa kufanya mikutano iliyojadili baadhi ya masuala ya EAC bila kuialika Tanzania. Inaelezwa kwamba Kenya haikujua kama mikutano iliyoifanya pamoja na Rwanda na Uganda ilikuwa kinyume na Itifaki ya shirikisho la Afrika Mashariki.

Hata hivyo, Rwanda na Uganda zinapaswa kung’amua kwamba hatua ya Kenya kujitokeza hadharani kuiunga mkono Tanzania katika masuala ya EAC, ni ishara ya kutetea umoja na upendo wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo, kama si salamu za kukemea kasumba za unafiki na hisia za kutafuta maslahi binafsi zinazoweza kuisambaratisha.

Kwa ukweli ulio wazi, nchi zote wanachama wa EAC zimetoka mbali na bado zina safari ya kufikia mengi ya maana ndani ya Jumuiya hiyo, kwa ajili ya maendeleo ya pamoja na wananchi wake.

Kwa mantiki hiyo, umefika wakati sasa Rais Kagame na Rais Museveni wakiri kwamba kwa namna walivyojaribu kuzitenga Tanzania na Burundi walikuwa wamepotoka na kuelekea ndiko siko ndani ya EAC. Walikuwa wanaelekea kuvuruga amani, umoja na upendo ndani ya Jumuiya hiyo.

Wapenda amani, umoja na upendo tunasubiri kuona na kusikia Rais Kagame na Rais Museveni wakirejea kuungana na Rais Kikwete, Rais Nkurunziza na Rais Kenyatta katika jitihada za kuijenga Jumuiya hiyo, vinginevyo watajihalalishia maneno ya wahenga yanayosema ‘mkataa wengi ni mchawi’.

Binafsi nisingependa kuona na kusikia Rais Kagame na Rais Museveni wanaitwa wachawi wa EAC.