Kwa hili, Lema amempiku Zitto
shabiki wa soka kuliko michezo mingine kwa muda mrefu. Kama Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, wangekuwa timu mbili za soka zinazopepetana, safari hii ningemshangilia Lema.
Ningempigia Lema makofi ya nguvu alipopepetana na Zitto kwa maneno au hoja, wiki iliyopita. Vijana hawa ni miongoni mwa wabunge maarufu, na wote ni wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kauli iliyotolewa na Lema katika kikao cha wabunge mjini Dodoma, Jumanne iliyopita, ndiyo chanzo cha vita hii ya maneno. Zitto ametoa taarifa akilalamika kwamba mbunge huyo wa Arusha Mjini alimshambulia kuhusu uamuzi wake wa kukataa posho za vikao vya Bunge.
“Mimi sipokei kabisa posho za vikao na ndiye mbunge pekee ambaye hapokei posho ya vikao tangu mwaka 2011. Hatuwezi sisi kama wabunge kuanza kulilia posho, wakati wananchi wetu hawana maji… Mbunge anayetaka posho zaidi akafanye kazi nyingine na awaachie wanaoweza kuwakilisha watu waendelee.” Hii ndiyo kauli ya Zitto iliyompatia Lema mashiko.
Mbunge huyu wa Kigoma Kaskazini anasisitiza kuwa malipo ya wabunge ni makubwa yasiyoendana na hali halisi ya maisha duni yanayowakabili wananchi wengi, huku Serikali ikishindwa kuwalipa vizuri walimu na wauguzi. Kimsingi kauli hii ina sura ya kutetea maslahi ya wananchi wanyonge.
Hata hivyo, tafakari ya Lema kuhusu kauli hii ya Zitto inakwenda mbali zaidi. Anamtafsiri Zitto kama mtu anayejifananisha na maskini.
Lema anatukumbusha kuwa umaskini si uzalendo. Anatetea hoja ya kuboresha maslahi ya wabunge akisema kufanya hivyo hakuwaondolei wawakilishi hao wa wananchi wajibu wa kutetea maslahi bora kwa watumishi wengine wa umma wakiwamo wa idara za Elimu, Afya, Polisi na Mahakama.
“Nilisema huwezi kuzuia taasisi moja kupewa maslahi bora eti tu kwa sababu watumishi wengine hawalipwi vizuri, ni haki wabunge kulipwa vizuri na wakati huo wapiganie maslahi ya watumishi wengine,” anasema Lema na kuongeza:
“Kwa hiyo, nikasisitiza kwamba nawashangaa wale ambao wanakataa posho ya shilingi 80,000 na ukienda kuchunguza wanakatwa fedha zote kutokana na mikopo waliyochukua, lakini bado wakija sehemu kama Arusha wanalala kwenye hoteli ya gharama kubwa kati ya dola za Marekani 150 na 600.
“Kwa hiyo, ikiwa unakataa posho ya shilingi 80,000 halafu unalala chumba cha dola 600 hustahili kupata credibility (sifa) stahili… ni unafiki tu na kutafuta sifa za kipuuzi.
“Kuna hatari ya kuona kwamba shilingi 80,000 au shilingi 200,000 ni fedha nyingi, ni kwamba kama sisi wabunge tutalipwa shilingi 50,000 basi maana yake ni kwamba walimu au polisi tutaridhika wakilipwa hata shilingi 10,000.”
Mbunge huyu wa Arusha Mjini anasema mazingira ya aina hiyo yanaibua maswali lukuki juu ya maisha ya mbunge kama Zitto. Anamtafsiri kama mtu mwenye ukwasi unaostahili kuhojiwa.
Kwa upande wake, Zitto anaona msimamo wa Lema unapingana na wabunge wengine wanachama wa Chadema, ambao wamepata kuunga mkono hoja ya kufuta posho za wabunge.
Zitto, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, wamepata kuunga mkono pendekezo la kufuta posho za wawakilishi hao wa wananchi bungeni.
Hivi karibuni imethibitika kwamba wakati wabunge wengi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakitaka kuboreshewa maslahi, kila mbunge hulipwa mshahara wa Sh milioni 11 kwa mwezi.
Kiasi hiki hakijumuishi posho ya Sh 330,000 anayolipwa mbunge kwa kuhudhuria kikao kimoja kwa siku. Kati ya fedha hizo, Sh 80,000 za kujikimu akiwa nje ya jimbo lake, posho ya vikao Sh 200,000 kwa siku na mafuta ya gari Sh 50,000. Pia mbunge hulipwa kiinua mgongo au bahashishi (gratuity) ya Sh milioni 72 baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka mitano cha ubunge.
Kadhalika, kila mbunge hupewa Sh milioni 50 za Mfuko wa Jimbo kila mwaka kwa ajili ya kuchangia gharama za shughuli za maendeleo ya wananchi jimboni.
Kwa ukweli usiopingika, kiwango cha mshahara na marupurupu ya wabunge wetu ni kikubwa. Ukweli mwingine usiopingika ni kuwa wabunge wanakabiliwa na mahitaji mengi likiwamo la kuwapatia wananchi wenye matatizo mbalimbali msaada wa fedha. Wanaotembelea ofisi na miji ya wabunge wataniunga mkono katika hili.
Zitto na wabunge wengine wanaposimamia hoja ya kufuta posho za wabunge lazima wana mbadala wa posho hizo. Lema amekwishaling’amua hilo, ndiyo maana anasema huo ni unafiki tu.
Zitto angepata umaarufu mkubwa mbele ya umma kama angetueleza kwamba anapokea posho zake za vikao vya Bunge na kuwagawia wananchi wenye matatizo mbalimbali jimboni kwake.
Halafu aseme ni wapi anapata fedha za kuziba pengo la mahitaji yake yaliyokuwa yanategemea posho hizo. Kisha atuambie iwapo amethibitisha kuwa na wabunge wengine wana chanzo kingine cha kujipatia fedha za ziada kama ambavyo yeye amebahatika.
Inatosha kusema tu kwamba angalau Lema amepata ujasiri wa kumjibu Zitto kwa nguvu ya hoja kuhusu msimamo wa kupinga posho za wabunge. Ni wabunge wachache ndani ya Chadema wenye ujasiri wa aina hiyo. Wengi ni wanafiki tu, ni waoga wa kusimamia ukweli, ni mithili ya bendera ambayo daima hufuata upepo.