TUZO YA MO IBRAHIM KUENDELEA

KUKOSA MSHINDI

Ni wazi sasa hakuna kiongozi bora Afrika

Bara la Afrika limeendelea kuumbuliwa na Wakfu wa Mo Ibrahim, ambapo tuzo hiyo imekosa mshindi kwa mara ya nne mfululizo.

Hilo ni pigo kubwa kama si dalili mbaya katika mustakabali wa uongozi katika Bara la Afrika. Lakini pia ni kipimo kinachothibitisha moja kwa moja kwamba dhana ya uongozi bora haijafanikiwa kuhuishwa katika mataifa mengi barani hapa.

Wakfu wa Mo Ibrahim ambao humzawadia rais mstaafu aliyeonesha uongozi mzuri, umesema hakuna kiongozi wa nchi yoyote ya barani Afrika aliyestahili tuzo hiyo mwaka huu.

Inafafanuliwa pia kwamba rais mstaafu anayestahili kupewa tuzo hiyo aliyeiwezesha nchi yake kuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa utawala wa kidemokrasia, uhuru binafsi, kuheshimu haki za binadamu, uthabiti wa siasa na maendeleo ya kiuchumi.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini London, Uingereza wiki iliyopita, Wakfu wa Mo Ibrahim umesema ulifanya tathmini na kujiridhisha pasi shaka kwamba hakuna rais mstaafu barani Afrika aliyekidhi vigezo vya kutwaa tuzo hiyo yenye thamani kubwa duniani.

Tuzo hiyo ambayo hutolewa na mfanyabiashara bilionea mzaliwa wa Sudan na raia wa Uingereza, Mo Ibrahim, hutoa dola milioni tano za Marekani kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo na dola 200,000 kila mwaka hadi kiongozi husika atakapofariki.

Pia Wakfu huo hutoa dola 200,000 za Marekani kwa mradi wowote unaoungwa mkono na mshindi wa tuzo hiyo kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo.

 

Kwa mujibu wa takwimu za wakfu huo, bado kuna baadhi ya nchi katika Bara la Afrika zinazoendelea kukabiliwa na matatizo ya uongozi usioridhisha likiwamo la kutotii sheria.


Utafiti huo unaangazia masuala mbalimbali vikiwamo vigezo vya utawala bora kama vile ukuaji wa uchumi, sekta za afya na sheria. Nchi iliyopata alama nzuri kuliko nyingine zote ni Mauritius, ikifuatiwa na Botswana na Cape Verde.


Hata hivyo, bado kuna tatizo la pengo kubwa kati ya maskini na matajiri, huku ripoti hiyo ikionya kuwa iwapo tatizo hilo litapuuzwa huenda mizozo zaidi ikaibuka.

Hali hiyo ni ishara tosha kwamba viongozi wengi wa nchi za barani Afrika wamejivisha dhana mbaya ya kutanguliza maslahi yao binafsi na kuweka kando misingi thabiti ya uongozi bora wa kidemokrasia, unaoheshimu haki za binadamu na unaoshughulikia kwa uzito unaostahili maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi husika.

Mwaka jana, niliandika makala kuchambua mazingira yanayosababisha marais wastaafu barani Afrika kukosa Tuzo ya Mo Ibrahim. Nashukuru utabiri wangu kwamba tuzo hiyo itaendelea kukosa mshindi umetimia mwaka huu. Bado kuna dalili kuwa itaendelea kukosa mshindi katika miaka ijayo ikiwa viongozi wa mataifa ya barani hapa wataendelea kukiuka misingi ya utawala bora.

Hatua ya Tuzo ya Mo Ibrahim ya kuendelea kukosa mshindi ni ishara mbaya inayokwaza dhamira nzuri ya bilionea huyo, inayolenga kuboresha maisha ya jamii barani Afrika kupitia utawala bora unaotii sheria na kuheshimu haki za binadamu.

Tuzo ya Mo Ibrahim kukosa mshindi kwa mara ya nne mfululizo ni changamoto kubwa kwa marais wa nchi za barani Afrika. Kwamba watafakari na kujitathmini kwa hatua ya kujiondolea kasoro zilizosababisha watangulizi wao kukosa tuzo hiyo.

Hofu kubwa ni kwamba Bara la Afrika likiendelea kukosa marais wastaafu wenye sifa za kutwaa Tuzo ya Mo Ibrahim, linaweza kutoa mwanya kwa mataifa ya mabara mengine kulikandamiza na kulinyima bara hili fursa muhimu zikiwamo za kiuchumi na kijamii kwa kisingizio cha ukosefu wa uongozi bora.

Marais wa sasa barani Afrika wana changamoto kubwa ya kuhakikisha wanasimamia ili kuwezesha wananchi wa mataifa yao kunufaika na rasilimali zilizopo ipasavyo na kwa usawa.

Baadhi ya viongozi waliotangulia katika mataifa ya Bara la Afrika ni pamoja na Kwame Nkrumah wa Ghana, Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Nelson Mandela wa Afrika Kusini.

Umefika wakati viongozi wa sasa barani Afrika warejee misingi ya uongozi bora iliyojengwa na viongozi hao wa Ghana, Tanzania na Afrika Kusini. Marais wa sasa barani Afrika watambue kwamba uongozi wa kimabavu, kidikteta na kidhalimu hautaishia kuwakosesha Tuzo ya Mo Ibrahim pekee, bali utawaweka katika hatari ya kuadhibiwa na nguvu ya umma kama si kushtakiwa baada ya kuondoka madarakani. Lakini pia watakuwa wametenda dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Bara la Afrika limejaaliwa na Mwenyezi Mungu neema ya utajiri wa rasilimali nyingi zinazostahili kutumiwa ipasavyo katika kuinua uchumi na maendeleo ya Waafrika kwa jumla ili kulifanya Bara hili kuwa mahali pazuri pa kuishi duniani.

Waafrika wengi tunapenda kama si kutamani kuona viongozi wetu wanauenzi utukufu huo wa Mwenyezi Mungu kwa kuonesha uongozi bora unaojali maslahi ya umma badala ya kujikita katika kujitafutia maslahi yao binafsi kiasi cha kukosa sifa za kutwaa Tuzo ya Mo Ibrahim.

Hadi sasa marais wastaafu katika nchi za barani Afrika waliopata kuibuka washindi wa Tuzo ya Mo Ibrahim na miaka waliyotangazwa ikiwa katika mabano ni Joaquim Chissano wa Msumbiji (2005), Festus Mogae wa Botswana (2008) na Pedro Pires wa Cape Verde (2011).