Kampuni za simu za mkononi zinaiba umeme, hatutapona
Wakati Wizara ya Nishati na Madini ikiwaaga vijana 10 wazawa wanaokwenda China kusomea shahada ya uzamili kuhusu fani ya mafuta na gesi wiki iliyopita, Shirika la Taifa la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kubaini wizi wa nishati ya umeme kwenye minara ya kampuni za simu za kiganjani.
Habari zaidi zinasema kwamba tayari baadhi ya mameneja, wahandisi na watendaji kadhaa wa Tanesco wameachishwa kazi na wengine kushushwa vyeo kutokana na kushindwa kudhibiti wizi huo.
Inaelezwa kuwa walioangukiwa na ‘panga’ hilo ndani ya Tanesco ni waliokuwa wakishughulikia mitambo ya minara iliyobainika kuiba umeme.
Ukaguzi uliofanywa na shirika hilo umebaini kuwa kampuni nyingi za simu za mkononi hapa nchini zimekuwa zikiiba umeme kupitia minara yao. Ukaguzi umefanyika kwenye minara yote na imeelezwa kuwa umeme wenye thamani ya shilingi zaidi ya bilioni tatu umeibwa na kampuni hizo!
Hadi sasa kampuni zinazotoa huduma za simu za mkononi hapa Tanzania ni Vodacom, Airtel, Tigo, Zantel na TTCL. Inaelezwa kuwa mnara wa simu za kiganjani hutumia kilowati nane za umeme wenye thamani ya Sh milioni 1.1, na mnara mkubwa hutumia kilowati 22 zenye thamani ya Sh milioni 3.1 kwa mwezi.
Kuna habari kwamba baada ya kubaini wizi huo sasa Tanesco imeamua kuanza kufunga mita za umeme katika kila mnara wa simu za mkononi. Mita hizo zitakuwa zinafanyiwa ukaguzi mara kwa mara na zitakuwa zinasomwa makao makuu ya shirika hilo.
Siwezi kubeza ufuatiliaji huo wa Tanesco ingawa umekuja huku kukiwa na malalamiko ya muda mrefu kwamba baadhi ya watu katika majumba, kampuni, viwanda na taasisi mbalimbali wanajihusisha na vitendo vya wizi wa umeme hapa nchini.
Wafanyabiashara wakubwa, wabunge na watu wengine maarufu wamekuwa wakitajwa kujihusisha na hujuma hizo zinazokwaza ufanisi ndani ya Tanesco katika suala zima la utoaji wa huduma ya umeme. Serikali imekuwa ikijizatiti kuongeza uzalishaji wa nishati hiyo, lakini kumbe hujuma nyingi zinachangiwa na watumishi wachache wasio waadilifu na waaminifu katika shirika hilo la umma.
Ni kwa mantiki hiyo ninaona kwamba kuna haja ya mamlaka husika kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya kampuni zilizobainika kuiba umeme katika minara husika. Ninasema hivyo kwa sababu hasara iliyotokana na wizi huo ni kubwa na madhara yake ni makubwa serikalini na kwa Watanzania kwa jumla.
Ni aibu kubwa kusikia na kuona kuwa kampuni za simu za mkononi zinajihusisha na wizi wa umeme, huku zikiendelea kupandisha gharama za matumizi ya simu hizo bila kuzingatia kipato duni kwa Watanzania walio wengi.
Kitendo cha kuiba umeme kinaashiria kuwa kampuni za simu za kiganjani haziishii kufanya hujuma hiyo pekee. Inawezekana kampuni hizo zinawaibia hata wateja wao kupitia huduma mbalimbali za simu hizo.
Ndiyo maana wateja wengi wamekuwa wakilalamika kuwa kuna wakati salio la fedha kwenye simu zao linakatwa katika mazingira ya kutatanisha. Wakati mwingine baadhi ya wateja huunganishwa katika huduma ambazo hawakuziomba na kukatwa fedha.
Imefika mahali simu za mkononi sasa zimegeuka kuwa adha, karaha na kero kwa wateja kutokana na ‘kupelekeshwa’ katika matumizi ya huduma za mawasiliano. Kwa vitendo hivyo, kampuni za simu za mkononi haziwezi kukwepa lawama ya kuchangia kuwaongezea wananchi umaskini.
Ndiyo maana ninasema hata katika suala hili la kuiba umeme kwamba kampuni hizo zinastahili kupewa adhabu kubwa ikiwa ni pamoja na kuzitoza faini kubwa na kuzifikisha mahakamani kujibu mashtaka ya uhujumu uchumi wa nchi, zitatoa fundisho na onyo kwa wengine wenye nia ya kutenda makosa hayo.
Watumishi wa Tanesco waliohusika katika wizi wa umeme katika minara hiyo nao wasiishie kufukuzwa kazi na kushushwa vyeo, bali washtakiwe sambamba na kampuni husika.
Watanzania wengi tusingependa kusikia na kuona suala hilo linayeyuka katika mazingira ya kutatanisha kama ambavyo imekuwa ikitokea kwa mengine mengi hapa nchini. Ni vizuri Tanesco ikatutangazia pia hatua ambazo imezichukua mpaka sasa dhidi ya waliojihusisha na hujuma hiyo.