LAAC imechelewa kugundua
madudu hazina, halmashauri

Ijumaa iliyopita, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ilitangaza kugundua mtandao wa wizi wa mabilioni ya shilingi za umma. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Rajab Mohamed Mbarouk, alisema mtandao huo unahusisha ofisi za Hazina na halmashauri mbalimbali hapa nchini.

Kwamba viongozi wa Hazina na halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji wamekuwa wakiongeza ziada ya kati ya Sh milioni 500 na 600 kwenye fedha zinazoidhinishwa kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.

 

Mbarouk alifafanua kuwa tayari mtandao huo umeshaidhinisha mamilioni ya shilingi katika halmashauri za wilaya za Mbarali, Korogwe Mjini na Mvomero kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi hewa!

 

“Katika vikao vyetu tumebaini kwamba Hazina na halmashauri nchini zinashirikiana kula fedha za Serikali,” alisema mwenyekiti huyo wa LAAC na kuendelea:

 

“Mfano halisi ni huu: Halmashauri ya Mbarali katika mahesabu walitakiwa kupewa shilingi milioni 70, lakini Hazina waliidhinisha shilingi milioni 700.

 

“Fedha hizi zinapofikishwa kule zinaidhinishwa kupokewa kwa shilingi milioni 70 zilizokuwa zikihitajika, zile zilizoongezwa zinarudi mikononi mwa mtandao huo ambao ni katika Hazina na halmashauri.

 

“Kama unataka kuona mtandao huo umeota mizizi mikubwa, tumebaini utakaswaji wa fedha umefanyika Halmashauri ya Korogwe Mjini shilingi milioni 500 huku mahitaji yao yakiwa chini ya shilingi milioni 100.

 

“Hivyo hivyo, utakaswaji huo umefanyika Halmashauri ya Mvomero kwa kupelekewa shilingi milioni 500 ambapo mahitaji yao hayakuwa yanafikia kiasi hicho. Kama wanakamati tumechukizwa na utoroshwaji wa fedha hizo na tutalifikisha bungeni kwa hatua zaidi.”

 

Kimsingi kitendo cha kugundua na kufichua ubadhirifu wa fedha za umma serikalini ni kizuri, lakini katika hili LAAC imekumbuka kujifunika shuka kumekucha.

 

Kwanini ninasema hivyo? LAAC haijaanza jana wala juzi. Imekuwapo kwa miaka mingi. Hujuma ya fedha za Serikali haijaanza jana wala juzi. Imekuwapo kwa miaka nenda miaka rudi, ndiyo sababu miradi mingi ya maendeleo ya wananchi imeendelea kujikongoja licha ya kuongezewa bajeti kila mwaka.

 

Ninaweza kuamini tu kwamba ama LAAC sasa imeamua kujisafisha kwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, au imenyooshewa kidole na uongozi wa juu serikalini. Sitaki kuamini kwamba madudu yanayotendeka Hazina na halmashauri zetu ni kitu kipya mbele ya kamati hiyo.

 

Ukiacha halmashauri za Mbarali, Korogwe Mjini na Mvomero zilizotajwa na LAAC, halmashauri za Tarime, Rorya, Mwanza, Bukoba, Tabora, Geita na nyingine nyingi hapa nchini zimekuwa zikilalamikiwa kwa ubadhirifu wa fedha za umma kwa muda mrefu sasa.

 

Lakini pia halmashauri hizo zimekuwa zikipata hati chafu na za mashaka, wakati mwingine kwa miaka miwili hadi mitatu mfululizo. Sitaki kuamini kuwa LAAC haijapata kusikia malalamiko ya ubadhirifu katika halmashauri hizo.

 

Viongozi (sio wote) katika halmashauri mbalimbali hapa nchini wamekuwa wakijiidhinishia malipo ya posho za ziara na vikao kinyume cha taratibu. Huduma bora katika sekta za afya, elimu, maji na barabara zimeendelea kukwazwa na ubadhirifu wa fedha unaoendekezwa na viongozi wa umma wasio waadilifu.

 

Ni aibu kubwa kwa watu tuliowakabidhi dhamana ya kusimamia matumizi sahihi ya fedha za Serikali kujigeuza wahujumu wakubwa wa fedha hizo. Hatuwezi kutokomeza umaskini miongoni mwa Watanzania kwa mtindo wa viongozi wachache kutumia fedha za umma kujineemesha binafsi na familia zao.

 

Bado ni mapema kuipongeza moja kwa moja LAAC kwa kitendo cha kufichua mtandao wa ubadhirifu wa fedha za umma. Tunahitaji kuona na kusikia kamati hiyo ikianika ubadhirifu zaidi wa fedha za Serikali na matumizi mabaya ya madaraka ndani ya Hazina na halmashauri zetu.

 

Lakini kwa upande mwingine, LAAC sasa ituoneshe kwa vitendo iwapo kweli imedhamiria kwa dhati ya moyo kudhibiti wizi wa fedha za umma. Ianze kushusha panga lake kwa watumishi waliohusika kuiba mamilioni ya shilingi kupitia halmashauri za Mbarali, Korogwe Mjini na Mvomero.

 

Adhabu kali kwa watumishi hao itakuwa fundisho kwa wengine wenye nia ya kufanya ubadhirifu huo. Vinginevyo fedha zinazotolewa na Serikali kwa nia nzuri ya kugharimia utekelezaji wa miradi ya maendeleo zitaendelea kuishia mifukoni mwa wajanja wachache huku Watanzania wengi wakiendelea kutafunwa na umaskini mkubwa.

 

Kikubwa zaidi LAAC ikae ikijua kwamba imechelewa kuanika madudu katika Hazina na halmashauri zetu hapa nchini, na sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya kukomesha tatizo hilo na kujijengea utumishi uliotukuka mbele ya jamii.