Wanafunzi IFM nao wachunguzwe

Kero za uvamizi, uporaji mali, ubakaji na ulawiti dhidi ya wanafunzi wa Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM), zitapatiwa ufumbuzi wa kudumu ikiwa uchunguzi unaofanywa na Jeshi la Polisi utawalenga pia wanafunzi hao.

Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Suleiman Kova, limeahidi kushughulikia kero hizo kwa uzito unaostahili baada ya wanafunzi hao kuandamana hadi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani jijini Dar es Salaam, hivi karibuni.


Wanafunzi hao walifikia hatua hiyo baada ya kuvamiwa, kuporwa mali mbalimbali zikiwamo simu za mkononi, laptop na fedha, huku ikielezwa kuwa wawili kati yao walidhalilishwa kwa kulawitiwa na kundi la vibaka.


Askari polisi walilazimika kutumia nguvu ya ziada ya kufyatua mabomu ya machozi kutawanya mamia ya wanafunzi hao waliojaribu kulazimisha kuingia bila utaratibu kwenye kivuko cha MV Magogoni kuelekea Kigamboni, na baadhi yao kutumia mwanya huo kupora mali za wafanyabishara ufukweni mwa Bahari ya Hindi.


Binafsi ninalipongeza Jeshi la Polisi kwa sababu kama lingepuuza kudhibiti vurugu hizo pengine yangetokea maafa makubwa ambayo yangeliingiza kwenye lawama kama si kulichafua mbele ya jamii.


Hata hivyo, maandamano hayo hayakuwa na kibali kutoka Jeshi la Polisi, na katika tukio lisilo la kawaida, hapakuwepo na kiongozi wa wanafunzi hao aliyejitokeza mapema kuzungumza kwa niaba yao mbele ya uongozi wa jeshi hilo.


Lakini kwa upande mwingine, FIKIRA YA HEKIMA inaamini kuwa ni vigumu vibaka wasio na uhusiano na baadhi ya wanafunzi hao kupata ujasiri wa kutekeleza uhalifu wa kuvamia, kupora mali, kubaka na kulawiti baadhi yao.


Kitendo cha wanafunzi hao kulazimisha kuingia kwenye kivuko na baadhi yao kupora mali za watu wengine kinaashiria kuwa miongoni mwao wamo wasio waadilifu, wanaoweza kuwasaliti wenzao kwa kushirikiana na vibaka kutenda uhalifu unaolalamikiwa.


Mamlaka husika zichunguze kubaini iwapo kweli wanafunzi wote wa IFM wamejengeka katika misingi ya maadili na uadilifu wanapokuwa darasani, hosteli na katika jamii inayowazunguka.


Wanafunzi watakaothibitika kujihusisha na uhalifu huo waadhibiwe iwe fundisho kwa wengine wenye nia ya kutaka kufanya hivyo.

 

Kuwaweka kando wanafunzi wa taasisi hiyo katika uchunguzi wa vitendo vya uvamizi, ubakaji, ulawiti, wizi na uporaji mali kwenye hosteli zao kunaweza kukosesha ufumbuzi thabiti wa vitendo hivyo vya uhalifu.


Pia kuna haja ya wanafunzi wa IFM kuhusishwa katika mpango wa polisi wa  ulinzi shirikishi jamii kama hatua mojawapo ya kuwaimarishia ulinzi na usalama katika makazi yao.


Lakini pia, ifike mahala Jeshi la Polisi nalo lijipange sawasawa kwa kuhakikisha linakuwa na wepesi wa kushughulikia matatizo ya kiusalama katika hosteli za wanafunzi hao kwa kuwa ni sehemu ya Watanzania wasomi wanaotazamiwa kuchangia ujenzi wa taifa letu.

 

Wakati Jeshi la Polisi likikumbushwa wajibu huo, wanafunzi wa IFM nao wanapaswa kuzingatia umuhimu wa kujijenga katika maadili na uadilifu, lakini pia kujenga dhana ya kutii sheria bila shuruti.