Kilio cha wafanyakazi wa OSHA kisipuuzwe

Dalili mbaya zinanyemelea Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA). Kuna hatari ya ofisi hiyo kutokalika ikiwa mamlaka za juu zitaendelea kupuuza malalamiko ya wafanyakazi dhidi ya Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo ya serikali.

Wafanyakazi wa OSHA wanamlalamikia Mtendaji Mkuu, Dk. Akwilina Kayumba, wakimhusisha na uongozi wa kimabavu, matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma.

 

Tayari malalamiko hayo yamewasilishwa mbele ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Taifa, Dk. Diwani Mruttu, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya OSHA, Gideon Nassari, na vyombo vya habari.

 

Katika malalamiko hayo, Dk. Kayumba anadaiwa kuwagawa, kuwanyanyasa wafanyakazi wa OSHA, kusimamisha maslahi yao na kuendekeza upendeleo katika kuwapandisha madaraja.

 

Inafafanuliwa kuwa Dk. Kayumba anajiandalia safari za mara kwa mara ndani na nje ya nchi, huku akijilipa posho kinyume cha taratibu za uendeshaji wa ofisi ya umma.

 

Mtendaji Mkuu huyo wa OSHA analalamikiwa pia kuwa amejiamulia kufuta mpango wa wafanyakazi wa taasisi hiyo kushiriki mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) na kutumia watu wasio waajiriwa kufanya kazi zinazopaswa kufanywa na waajiriwa.

 

“Kusimamishwa kwa maslahi ya wafanyakazi (incentives) kumesababisha wafanyakazi kukosa ari ya kazi na kukata tamaa, mfanyakazi anakaa katika ngazi moja bila kupandishwa daraja kwa muda mrefu.

“Utawala wa OSHA umewagawa wafanyakazi… kuna wafanyakazi wanaopata upendeleo wa wazi wa kimaslahi huku wengine wakitaabika. Mara kadhaa Mtendaji Mkuu amekuwa akisikika kwa wafanyakazi akisema “asiyekuwa upande wangu hataifaidi OSHA”.

“Baadhi ya kero za wafanyakazi na tofauti zilizopo kati ya Mtendaji Mkuu na wafanyakazi hazitatuliwi,” inaeleza sehemu ya risala ya Tawi la OSHA-TUGHE iliyosomwa kwa Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Dk. Mruttu, alipozuru ofisi za OSHA Dar es Salaam, hivi karibuni.

 

“Mtendaji Mkuu anajilipa posho nyingi, kwa mfano, kwa siku anajilipa posho ya Sh 80,000 kwa kila kipindi anachofundisha, Sh 100,000 za ufunguzi na Sh 100,000 nyingine za ufungaji wa mafunzo, jambo ambalo si sahihi kwa mujibu wa sheria na taratibu.

“Jambo la kushangaza ni kuwa huyu Mtendaji Mkuu amejigeuza kuwa mhasibu, ofisa ununuzi na utumishi wa OSHA, kwa mfano, yeye ndiye anayefanya kazi ya kulipa malipo yote ikiwa ni pamoja na posho kwenye mafunzo kana kwamba ofisi haina wahasibu,” inaongeza sehemu ya risala hiyo.

 

Wafanyakazi hao walimwomba Dk. Mruttu kuingilia kati unyanyasaji na uonevu wanaofanyiwa na Mtendaji Mkuu huyo wa OSHA ili kunusuru mparaganyiko katika taasisi hiyo ya Serikali.

Akijibu malalamiko hayo, Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Dk. Mruttu, alieleza kusikitishwa na vitendo viovu vinavyodaiwa kufanywa na kiongozi huyo wa OSHA. Aliahidi kufuatilia na kuchukua hatua zinazostahili.

Aliahidi kutumia kofia ya TUGHE kushughulikia malalamiko hayo kwa ufanisi kama hatua mojawapo ya kurejesha uhusiano na ari ya utendaji kazi kwa wafanyakazi wa OSHA.

 

Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Dk. Akwilina Kayumba, alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alikana kuguswa na malalamiko yanayotolewa na wafanyakazi hao dhidi yake.

 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Ajira, Eric Shitindi, alipoulizwa alisema kwamba hajapata malalamiko kutoka kwa wafanyakazi wa OSHA.

Lakini pia, katika tukio lisilo la kawaida, Dk. Kayumba alithubutu kuwazuia waandishi wa habari waliofuatana na Dk. Mruttu kushiriki katika mkutano wa Mwenyekiti huyo wa TUGHE Taifa na wafanyakazi wa OSHA.

“Mimi kama Mtendaji Mkuu wa OSHA na familia yangu hapa sijawaalika waandishi wa habari kuja hapa, nimemwalika Mwenyekiti wa TUGHE na si waandishi,” alisema Dk. Kayumba kwa jazba kubwa.

Waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari waliokuwa wamefuatana na Mwenyekiti huyo wa TUGHE Taifa walitii na kuondoka katika ofisi za OSHA lakini baada ya mkutano huo walipata fursa ya kuzungumza na Dk. Mruttu ambaye alilaani kitendo hicho.

Kitendo cha Dk. Kayumba kuwazuia waandishi kushiriki mkutano huo ni dalili nyingine kwamba mambo si shwari ndani ya OSHA.

 

Ni katika msingi huo, ninasisitiza kuwa kuna haja ya mamlaka za juu zikiwamo Wizara ya Kazi na Ajira, TAMISEMI na TUGHE kuingilia kati kwa kuyafanyia kazi malalamiko lukuki yanayotolewa na wafanyakazi dhidi ya Mtendaji Mkuu wa OSHA, Dk. Kayumba.

 

Mambo mengi yamekuwa yakiborongwa katika ofisi nyingi za serikali kutokana na kasumba mbaya ya baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu kupuuza malalamiko ya watumishi wa ngazi ya chini.

 

Wafanyakazi wa OSHA wana hoja, wasikilizwe, kilio chao kisipuuzwe, kifuatiliwe na kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu. Kupuuza malalamiko ya wafanyakazi hao kutazidi kuhatarisha mustakabali wa taasisi hiyo ya serikali.