Mishahara mipya isiwe kinadharia
Hivi karibuni Serikali imetangaza viwango vipya vya mishahara kwa watumishi wa umma, vitakavyoanza kutumika mwezi huu, ikitaja kima cha chini kuwa ni Sh 240,000. Mei 29, mwaka huu, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, aliliambia Bunge kuwa Serikali imekamilisha pia mchakato wa kuongeza kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi kitakachoanza kutumika rasmi Julai 1, mwaka huu.
Akizungumza katika sherehe za Mei Mosi, mwaka huu zilizoadhimishwa kitaifa mkoani Mbeya, Rais Jakaya Kikwete aliahidi unafuu wa maisha kwa wafanyakazi.
Hatuwezi kukataa ukweli kuwa jitihada hizi ni dalili kuwa Serikali inapenda kuona Watanzania wanaishi maisha bora yasiyokuwa na bughudha ya umaskini.
Hata hivyo, hofu ya wengi wetu ni kwamba utekelezaji wa maelekezo hayo ya Serikali, unaweza kuishia kuwa wa kinadharia kutokana na ukiritimba na ukaidi wa baadhi ya viongozi wa umma na sekta binafsi.
Serikali yetu ina dosari moja kubwa. Haina ujasiri wa kusimamia utekelezaji wa maelekezo yake. Maagizo mengi ambayo imekuwa ikiyatoa, hususan kuhusu nyongeza ya kima cha mshahara, mara nyingi yamebaki kuwa ya kinadharia.
Kwa mfano, kuna wakati Serikali ilitangaza kwamba kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa nyumbani, wahudumu wa hoteli na baa kimeongezwa hadi Sh 80,000. Lakini utekelezaji wake umeendelea kuwa wa kinadharia kwa waajiri wengi.
Hadi Serikali inatangaza mishahara mipya mwezi huu, wafanyakazi wengi wa maeneo hayo wameendelea kutumikishwa kwa ujira mdogo. Wengi wanalipwa kati ya Sh 30,000 na Sh 60,000, kiwango ambacho hakitoshi kumudu mahitaji ya kawaida ya mfanyakazi wa aina hiyo kwa mwezi.
Tafsiri ya taswira hii ni kwamba Serikali ilionesha uhodari wa kutangaza kima hicho cha mshahara, lakini imedhihirisha udhaifu wake kwa kutosimamia utekelezaji wake kwa vitendo. Hii ni taswira mbaya kwa Serikali iliyoahidi kuwatumikia wananchi wake.
Serikali yetu iliyopaswa kuwa kimbilio la wanyonge, inaelekea kuwa chanzo cha kuwakandamiza. Baadhi ya wafanyakazi wa sekta za umma na binafsi wanalipwa mishahara duni licha ya kufanyishwa kazi kubwa. Unyonyaji na ukandamizaji huu dhidi ya wananchi wanyonge unafanyika si kwamba Serikali haiujui!
Kasumba ya Serikali kutosimamia utekelezaji wa vitendo wa maagizo yake yakiwamo ya nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi inachangia kuwafanya baadhi ya wananchi kuichukia na kujuta kuikabidhi madaraka. Watanzania tungependa kuona Serikali yetu inasimama kwenye maneno yake bila kutetereka.
Kitendo cha Serikali kuendekeza udhaifu katika kusimamia maagizo yake, kimechangia hata Mifuko ya Hihadhi ya Jamii (si yote) kuwa na kiburi cha kuwanyanyasa wanachama wao. Baadhi ya mifuko hiyo haitekelezi jukumu lake la kukusanya kwa ajili ya kuwatunzia wanachama wao fedha wanazokatwa kutoka kwenye mishahara yao katika mashirika na kampuni mbalimbali.
Serikali yetu haiwezi kukwepa lawama za kujenga mazingira kandamizi dhidi ya wanyonge, kwa sababu kama ikiwajibika ipasavyo wafanyakazi hawatapunjwa na kudhulumiwa mishahara na haki zao nyingine. Baadhi ya waajiri wamejigeuza miungu-watu, wanajiamulia kiwango cha mshahara wa wafanyakazi wao na mara nyingi hawawalipi kwa wakati.
Kiongozi mstaafu wa chama cha FDC nchini Uganda, Dk. Kizza Besigye, amepata kusema, “Nafikiri umefika wakati sasa kuorodhesha idadi ya wasomi wakiwamo maprofesa ambao ni sawa na janga katika nchi yetu [Uganda] ili kuwachukulia hatua kwa kuwa hawatusaidii chochote.”
Maneno hayo ya Dk. Besigye yana maana hata katika Serikali yetu ambayo imeajiri wasomi lukuki wa kada mbalimbali, ambao hata hivyo, baadhi yao hawawajibiki ipasavyo.
Wizara za Kazi na Ajira, Katiba na Sheria hazijawajibika ipasavyo katika kushughulikia waajiri wanaopuuza maelekezo ya Serikali kuhusu nyongeza ya viwango vya mishahara ya wafanyakazi wao. Katika baadhi ya sekta, maelekezo ya Serikali yameendelea kuwa ya kinadharia badala ya kutekelezwa kwa vitendo.
Umefika wakati Serikali ijitafakari upya kuhusu usimamiaji wa maelekezo yake. Uhodari inaoutumia kutoa maelekezo iutumie pia kusimamia utekelezaji wake.
Serikali imekuwa ikijipambanua kuwa ni sikivu kwa wananchi wake. Tunaomba itudhihirishie usikivu huo kwa kusimamia ili kuhakikisha viwango vipya vya mishahara ilivyovitangaza vinalipwa kwa vitendo. Uwezo huo inao.