SADC ‘inachechemea’ kuisuluhisha Madagascar

Hatima ya mzozo wa kuwania madaraka nchini Madagascar imeendelea kuwa kitendawili kigumu, baada ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ‘kuchechemea’ kuutatua.

Madagascar imeingia katika mzozo huo miaka minne iliyopita, yalipotokea mapinduzi yaliyomwondoa madarakani Rais Marc Ravalomanana na nafasi yake kuchukuliwa na Andry Rajoelina.


Baadaye viongozi wa nchi za SADC, yaani Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Swaziland, Tanzania, Zambia, Zimbabwe, Afika Kusini, Seychelles na Madagascar ambayo imesimamishwa uanachama kutokana na mzozo huo, wakisisitiza kutomtambua Rajoelina kama Rais wa Madagascar na kutaka Ravalomanana aliyekimbilia Afrika Kusini arejee nchini kwake bila masharti.


Nchi za SADC ziliwataka Rajoelina na Ravalomanana kutogombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao (Mei mwaka huu) kama hatua muhimu ya kurejesha uelewano nchini Madagascar.


Hata hivyo, viongozi wa SADC wameshindwa kulipatia ufumbuzi suala hilo katika mkutano wao uliomalizika Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.


Ingawa Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa, Amani, Ulinzi na Usalama wa SADC (Troika), Rais Jakaya Kikwete, amewambia waandishi wa habari kwamba majadiliano kuhusu suala hilo yanaendelea, dalili zinaonesha kuwa, ama jumuiya hiyo itatumia muda mrefu, au itashindwa kutatua mzozo huo.

 

Mkutano wa SADC iliomalizika Dar es Salaam, ulitarajiwa kutoa suluhu kwa kumbana Rajoelina asigombee urais kwenye uchaguzi mkuu ujao lakini umekosa ujasiri wa kufanya hivyo. Inadaiwa kiongozi huyo anaendelea kujipanga kugombea madaraka hayo.


Kama mkutano huo umeshindwa kutoa tamko na msimamo rasmi wa SADC kuhusu hatma ya mzozo na siasa za Madagascar, ni akina nani watapata fursa na uthubutu wa kushughulikia tatizo hilo? Wakati SADC ‘ikichechemea’ kushughulikia mzozo huo, duru za kidipromasia zinasema Rajoelina anaendelea kuungwa mkuno na baadhi ya dola za magharibi, achilia mbali maofisa wa jeshi la nchi hiyo.


Inaelezwa kuwa pande hizo mbili ndizo zinazomtia morali na kumwongezea Rajoelina nguvu za kusimamia kauli yake ya kugombea urais Madagascar. Binafsi sitaki kuamini kwamba SADC hailijui hilo. Inawezekana SADC, ama haijitambui, au haijiamini kwamba ina uwezo wa kumaliza mzozo wa kisiasa nchini Madagascar, ndio maana imeshindwa kutoa tamko la kumbana Rajoelina.


Lakini pia, jumuiya hiyo inapaswa kuangalia iwapo kweli juhudi za kumzuia Rajoelina kugombea urais zitarejesha uelewano wa kisiasa Madagascar kuliko ambavyo ingemwacha agombee.


Itakuwa aibu kwa SADC kuendelea na juhudi ambazo mwisho wa siku haziwezi kuleta ufumbuzi thabiti wa mgogoro wa kisiasa unaoendelea kuhatarisha amani na utulivu Madagascar.


Kitendo cha viongozi wa jumuiya hiyo kuendelea ‘kuchechemea’ katika kutafuta suluhu ya mzozo wa kisiasa nchini Madagascar kinaweza kutoa mwanya wa kuongeza kasi na kufukuta kwa mzozo huo.


FIKRA YA HEKIMA inadhani SADC inapaswa kuongeza juhudi, kujiamini na kuhakikisha inakuwa makini zaidi katika juhudi zake za kushughulikia mzozo huo kuepuka aibu ya kushindwa kuutatua na kurejesha uelewano nchini Madagascar.