Wawekezaji wazawa waungwe mkono

Watanzania tumejenga kasumba mbaya ya kuwathamini wawekezaji wa kigeni. Wakati huo huo tumekuwa kikwazo kwa wawekezaji wazawa!

Kasumba hii inatawaliwa na msukumo wa kijicho, unafiki, kinyongo, chuki za kisiasa na wivu wa kubomoa badala ya wivu wa maendeleo.

 

Kuna watu miongoni mwetu Watanzania wasiopenda kuona na kusikia wenzao wanasonga mbele na kufanikiwa maishani. Hao siku zote wanafurahia kuona wageni kutoka mataifa mengine wanapewa kipaumbele cha kuwekeza hapa nchini kuliko wazalendo wenzao.

 

Unahitajika moyo wa uvumilivu mkubwa kwa mzawa kuwekeza hapa nchini kwa sababu maadui wakubwa ni baadhi ya Watanzania wenyewe. Hii ni dhana yenye shabaha ya kuwadidimiza wazawa katika maendeleo ya uchumi.

 

Wawekezaji wazawa wamekuwa wakipata vikwazo na misukosuko lukuki kutoka kwa baadhi ya Watanzania wenzao. Mara nyingi husingiziwa na kuzushiwa tuhuma za uporaji wa ardhi na mashamba ya wanyonge.

 

Taswira hii imeendelea kuonekana sehemu tofauti hapa nchini, licha ya Serikali yetu kuendelea kutoa wito ikiwataka wazawa kujitokeza kuchangamkia fursa za uwekezaji kwenye sekta mbalimbali.

 

Uchunguzi uliofanywa na Fikra ya Hekima katika maeneo mbalimbali hapa nchini, umebaini kuwa kasumba hii inaendekezwa zaidi katika baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.

 

Kuna wazawa kadhaa wameonesha dhamira nzuri ya kuitikia wito huo wa Serikali, wamejitokeza kuwekeza katika sekta mbalimbali zikiwamo za elimu, kilimo, afya, michezo, utalii na kadhalika. Lakini hawathaminiwi, hawaungwi mkono ila wanapigwa vita na wazawa wenzao!

 

Imefika mahali baadhi ya wawekezaji hawa sasa wanajutia uamuzi wao wa kuwekeza hapa Tanzania, na wengine wamelazimika kufunga miradi yao waliyowekeza kwa mitaji mikubwa kwa juhudi zao binafsi.

 

Miongoni mwa madhara ya kufunga miradi iliyowekezwa na wazalendo wenzetu ni kupunguza idadi ya ajira na huduma za kijamii kwa Watanzania.

 

Binafsi nimekuwa nikijiuliza kwamba Watanzania tutaendelea kupigana vita hadi lini? Tutaendelea kuthamini wageni na hasa Wazungu mpaka lini? Tutaendelea kutojithamini na kutojikubali hadi lini? Jamani, tuamue kwamba sasa imetosha.

 

Siku zote wengi wetu tumekuwa tukilalamika kwamba baadhi ya wawekezaji wa kigeni ndiyo wanaonufaika na rasilimali za nchi yetu kupitia uwekezaji. Basi, tujitambue sasa na kuona kuwa njia sahihi ya kudhibiti tatizo hilo ni sisi wenyewe kujikakamua kwa kuchangamkia uwekezaji katika nyanja mbalimbali.

 

Kasumba ya kupigana vita katika suala la uwekezaji haina tija yoyote katika jamii yetu ya Watanzania. Tubadilike na tujitahidi kuungana mkono ili tujiimarishe katika uwekezaji hapa nchini, na hata nje ya Tanzania.

 

Kasumba ya Watanzania kuwekeana vikwazo katika uwekezaji itaendelea kutoa mwanya mkubwa kwa wawekezaji wa kigeni hapa nchini, hata kwa vitu ambavyo tuna uwezo wa kuvifanya kwa ufanisi. Ni aibu kwetu wazawa kuendelea kuwa wategemezi hata kwa mambo yaliyo chini ya uwezo wetu.

 

Umefika wakati hata Serikali yetu ilitambue tatizo hili la wazawa kuwekeana vikwazo katika uwekezaji, na hivyo, iweke mikakati thabiti ya kulidhibiti ili kuhamasisha uwekezaji wa kizalendo kwa manufaa ya Taifa letu kwa jumla.

 

Wawekezaji wazawa wathaminiwe na kuungwa mkono na kila mmoja wetu kwa maendeleo ya Watanzania kwa jumla. Tujiondoe katika jela ya utegemezi kwa wageni. Inawezekana, ni sisi tu.