2015 tuwakatae wabunge, mawaziri wa aina hii

Kwa hakika Watanzania hatuna sababu ya kuwarejesha madarakani wanasiasa hawa, kwa vile wametudhihirishia wazi kuwa nia yao ilikuwa ni zaidi ya kutuongoza na kututumikia.

Ninazungumzia wabunge na mawaziri wasiopokea simu za wananchi wa kawaida. Waswahili wanasema kufanya kosa si kosa; kurudia kosa ndiyo kosa.

Basi, kwa kutambua na kuzingatia hilo, Watanzania tuhakikishe kuwa katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015 nchini, haturudii kosa la kuwapatia uongozi wanasiasa wa aina hiyo.


Wabunge na mawaziri wengi siku hizi wamejenga kasumba mbaya ya kutopokea simu wanazopigiwa na wananchi wa kawaida. Ni kama wamesahau kuwa wananchi hao ndiyo mtaji wao uliowawezesha kupata wadhifa huo.


Kwa sasa wabunge wengi wanawathamini watu wenye wadhifa kama wao na wa juu zaidi. Wapo waliofikia hatua ya kuwaona wananchi wa kawaida kama kichefuchefu kwao!


Tumekuwa tukishuhudia kabla ya kupata ubunge wanasiasa hawa wakionesha unyenyekevu wa hali ya juu mbele ya wananchi. Wengine hufikia hatua ya kusalimia watoto na wajukuu zao kwa kupiga magoti kama ishara ya kuwathamini na kuwaheshimu.


Leo wabunge hawa walioahidi kuwatumikia wananchi kwa kiwango cha juu, wamewageuka wapigakura wao, hawawathamini tena wala hawataki kupokea simu zao. Ni kama hawakumbuki maneno ya wahenga yanayosema “kataa neno usikatae wito.”Imebainika kuwa baadhi ya wabunge wanakwenda majimboni kwao kwa kujificha nyakati za usiku, lakini pia wanafunga vioo vya magari yao, na kutopeperusha bendera zao wawapo majimboni mwao.


Hali hii inatudhihirishia wazi kuwa wabunge wenye tabia hiyo waliomba uongozi kwa nia ya kutumia madaraka hayo kujipatia maslahi binafsi; na si kushughulikia maendeleo na maslahi ya umma. Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipata kusema, “Kutokana na umri wake mkubwa, watu wengi wenye kasoro wamejiingiza kwenye chama hiki. Sasa kimekuwa kama kokoro ambalo wakati mwingine hubeba viumbe visivyohitajika. Tunao watu wa ajabu ndani ya CCM ambao hawafanani na CCM.”


Vivyo hivyo, kutokana na tasnia ya siasa kutazamwa kama njia ya kufuta umaskini nchini, watu wengi wa ajabu, wasio na sifa za uongozi na wasiofanana na taaluma ya siasa wamejiingiza huko.


Wananchi wengi wamekuwa wakilazimika kutumia njia ya simu kuwasiliana wabunge na mawaziri, kwa vile si rahisi sana kukutana nao ana kwa ana ili kuwasilisha hoja zao mbalimbali. Lakini viongozi hao wameendelea kuwapuuza na kukwepa kuwasikiliza.


Wananchi wengi wameendelea kupata matatizo mbalimbali ambayo kimsingi yangetatuliwa ama na wabunge, au mawaziri, kwa njia ya mawasiliano ya simu. Wananchi wengi wanajuta kuchagua viongozi hao.


Ingawa imedhihirika kuwa wabunge wengi hukwepa kupokea simu za wananchi kwa hofu ya kuombwa misaada na kuulizwa utekelezaji wa ahadi lukuki walizotangaza wakati wa kampeni, lakini hayo hayawezi kuwa ufumbuzi wa matatizo yaliyopo.


Ndiyo maana ninasisitiza kwamba kwa vile wabunge hawa wamewapuuza wananchi kiasi hicho na kuwaona ni wa nini, basi na wananchi nao wawaone ni wa kazi gani wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao, maana karibu wote watajidai wamesahau dharau waliyowaonesha wananchi, hivyo kuthubutu kurudi kuwaomba ridhaa ya kuendelea kuwa wabunge wao.


Wananchi tuhakikishe tunakuwa makini tusije fanya kosa la kuwarejesha madarakani wabunge hawa wasiothamini madaraja waliyovuka kutoka uraiani kwenda kwenye neema ya madaraka. Mwaka 2015 tuhakikishe tunawaonesha madhara yanayompata mtu anayemtukana mamba kabla hajavuka mto.

 

Umefika wakati Watanzania tujenge ujasiri na uthubutu wa kuwakataa viongozi wababaishaji, wabinafsi na wasiojali wala kutumikia watu waliowawezesha kupata madaraka.


Hatuwezi kuendelea kuwakumbatia wabunge wanaotumia wadhifa huo kujineemesha na familia zao, huku wakipuuza hata kupokea simu wanazopigiwa na wapigakura wao.

 

Tuwakatae hao katika Uchaguzi Mkuu ujao, tuwape madaraka watu wenye uwezo na nia thabiti ya kutumikia wananchi kwa uzito unaostahili.