Kwa kawaida Serikali hutwaa maeneo. Huhamisha wahusika, wamiliki, na kuchukua eneo kwa malengo maalum yaliyokusudiwa. Yaweza kuchukuliwa nyumba yako, kiwanja, au hata shamba.
Mara kadhaa Serikali hufanya hivi panapo mahitaji maalum ya shughuli za umma kama ujenzi wa miundombinu kama barabara, reli, huduma za umeme na maji, ujenzi wa shule, vyuo, vituo vya afya na miradi mingineyo kwa manufaa ya umma.
1. FIDIA YA ARDHI NI NINI
Fidia ya ardhi ni stahili ambayo mwenye ardhi mmiliki anatakiwa kupata pale ardhi yake inapotwaliwa/inapochukuliwa na Serikali kwa matumizi maalum ya Serikali/umma.
2. JE, UNAWEZA KUIKATALIA SERIKALI ARDHI YAKO ISICHUKULIWE?
Serikali inapotaka kumhamisha mwananchi na kuchukua ardhi yake kupisha mradi wa umma kisheria, mwananchi hana uwezo wa kukataa. Hii ni kwa sababu ardhi yote ni mali ya umma ambayo mdhamini wake mkuu ni Serikali kupitia mamlaka ya Rais. Hivyo tunaweza kusema kuwa ardhi ni mali ya umma inayodhaminiwa na Serikali/Rais.
Kwa hiyo, mwananchi hawezi kuikatalia Serikali kuchukua mali hiyo isipokuwa kisheria ni kuwa anayehamishwa apewe fidia.
Hata ukiamua kwenda mahakamani kupinga kutwaliwa ardhi hutapinga kuwa Serikali isichukue ardhi yako kabisa, isipokuwa utapinga kuhusu fidia, labda fidia ndogo au utaratibu mbovu uliotumika kukadiria fidia, riba n.k.
Labda kuwe na uonevu au hila katika kutaka kutwaliwa ardhi yako au namna nyingineyo ya nia ovu ndipo unaweza kupinga ardhi yako kutwaliwa. Lakini haitawezekana kupinga hatua hiyo ikiwa kuna malengo maalum ya kutwaa ardhi kwa ajili ya shughuli za umma.
3. ZIJUE AINA ZA FIDIA
Watu wengi wamekuwa wakijua kuwa fidia ni pesa tu. Linapokuja suala la fidia ya ardhi watu hudhani kinachotakiwa kutolewa na Serikali ni pesa. Hili si kweli kwa kuwa fidia haimaanishi pesa pekee kama tutakavyoona hapa chini.
(a) Fidia ya pesa. Hii ni fidia inayojulikana sana na ni aina ya fidia ambayo imekuwa ikipendwa mno na ndiyo aina ya fidia ambayo hutumiwa na Serikali mara kwa mara kuliko fidia nyinginezo. Maeneo ya watu hukadiriwa na hulipwa pesa kutokana na bei ya soko ya eneo husika. Imefanyika hivyo sehemu nyingi na inaendelea kufanyika.
(b) Fidia ya ardhi. Hii ni aina ya fidia ambayo huhusisha kupewa ardhi. Inachukuliwa ardhi yako kwa ajili ya shughuli za umma unapewa ardhi nyingine kufidia iliyochukuliwa. Muhimu ni kuwa usipewe ardhi nyingine kama fidia ambayo hadhi yake, ubora wake, matumizi yake, na ukubwa wake uko chini ya ile ya kwako iliyochukuliwa.
Unatakiwa upewe ardhi yenye ubora uleule, ukubwa uleule, matumizi yaleyale na hadhi ileile. Hadhi, ubora na ukubwa vinaweza kuzidi lakini visipungue. Ikiwa utapewa ardhi kama fidia na ikawa chini ya ile kiukubwa, ubora na hadhi basi unayo malakamiko ya msingi ambayo utayapeleka kwa Kamishna wa Ardhi au mahakamani ili kupata kiwango cha haki kilichoporwa.
Isipokuwa hutaenda mahakamani kulalamika kuwa umepewa ardhi kubwa zaidi na yenye ubora zaidi kuliko ile ya kwako iliyochukuliwa.
(c) Fidia ya jengo. Badala ya pesa unaweza kupewa jengo au majengo yanayofanana na lile ambalo limechukuliwa au kubomolewa kupisha mradi wa umma. Kama nilivyoeleza hapa juu kuwa utatakiwa kupewa jengo lenye ubora, hadhi na ukubwa uleule. Malalamiko utakuwa na haki nayo ikiwa umepewa jengo lililo chini ya ubora na hadhi ya lile lililochukuliwa.
(d) Fidia ya kutumia mali za umma. Hii ni aina ya fidia ambapo baada ya kuchukuliwa ardhi yako, kwa mfano, jengo ambalo ulikuwa ukipokea kodi unapewa jengo jingine si kwa kulimiliki bali kulitumia ambapo unaweza kuwa ukichukua kodi kama mmiliki kwa muda fulani utakaokubaliwa mpaka hapo kiwango cha pesa ambacho ungelipwa kama fidia kitaisha. Hii pia hutumika kufidia mashamba ambapo utapangiwa kutumia shamba la umma kwa muda fulani kufidia la kwako lililochukuliwa.
(e) Fidia ya miche na mimea. Hii hutolewa panapo uharibifu wa miche na mimea katika eneo lako. Yawezekana eneo lililochukuliwa lilikuwa na miche na mimea na imeharibiwa. Si lazima upewe pesa unaweza pewa miche na mimea yenye hadhi na ubora kama wa ile ya kwako. Hii hujumuisha fidia ya mazao na nafaka pia.
( f) Fidia kwa makubaliano. Hii ni aina ya fidia ambapo mdai na Kamishna wa Ardhi hukaa meza ya mazungumzo na kukubaliana aina ya fidia inayofaa kwa kiwango cha ardhi, jengo lililochukuliwa kupisha mradi. Hapa fidia inaweza kuwa yoyote kutegemea na makubaliano ya pande hizo mbili.
Haya yote ni kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya 1999 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya 1999.
Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.