Msanii wa muziki wa hip-hop, Farid Kubanda, maarufu kama Fid Q, kila ifikapo Agosti 13, husherehekea siku yake ya kuzaliwa.
Mashabiki wa muziki wa Fid Q wanafahamu Agosti 13 hufanya nini kwa mashabiki wake. Fid Q hutumia fursa hiyo kukonga nyoyo za mashabiki wake kwa kuachia wimbo mpya ambao ndani yake hudhihirisha kila mwaka kwamba yeye ni mwamba wa hip-hop nchini.
Fid Q hutumia siku hiyo kukonga nyoyo za mashabiki wake huku akitambulisha wimbo mpya ambao ndani yake hudhihirisha kwamba yeye ni mwamba wa muziki wa hip-hop nchini.
Zikiwa zimebaki siku saba kwa Fid Q kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa, tayari mashabiki wake wameanza kusubiri siku hiyo kwa hamu, huku wakitaka kujua mwaka huu atakuja na kitu gani kipya?
Farid Kubanda anafahamika kwa uwezo wake wa kuandika mashairi yanayohitaji kutumia fikra na uwezo mkubwa wa akili kuyatafakari ili kuyaelewa.
Tayari kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram mwaka huu amewataarifu mashabiki wake kwamba anawaletea albamu mpya aliyoipatia jina la ‘Kitaaolojia’.
Ni albamu ambayo imesubiriwa kwa muda mrefu tangu alipoanza kuitangaza kwa mashabiki wake kwamba ameandaa albamu yenye jina hilo.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Julai 27, mwaka huu Fid Q aliandika: “KITAALOJIA ni jina la album yangu ya 3….ninawashauri muanze kukichanga mapema ili ikitoka mjipatie nakala zenu coz hata mimi nitajipatia nakala yangu ili kuipa heshima sanaa.”
Moja ya wachangiaji kwenye andiko lake hilo aliandika: “ Tumechanga, tumekula, tumechanga tumekula, rasta hebu itoe hii kitu u-focus na albamu ya saba,” aliandika shabiki huyo.
Mchangiaji mwingine kwenye ukurasa wa Fid Q aliandika: “Huhitaji kujichanga, tunachohitaji ni kuvunja vibubu, kwa sababu hii albamu imepromotiwa kutoka tangu niko form one mpaka leo nina degree ya pili na haijatoka.”
Miaka sita iliyopita Fid aliwahi kutoa maana halisi ya neno ‘Kitaalojia’ ambavyo alisema kuwa KITAAOLOJIA ni mjumuiko wa mambo yote ambayo amejifunza mtaani, aidha kwa kumtokea yeye mwenyewe kwa njia ya kuona na kusikia.
Wakati wa kuandaa albamu hiyo Fid Q alieleza kuwa ndoto yake ni kuhakikisha anaanzisha mradi ambao mapato yatokanayo na kuuzwa kwake yataingizwa vitabuni kwa ajili ya kufundisha wanafunzi shuleni na vyuoni.
Alieleza kuwa kupitia mradi huo watu wataelewa kuwa pamoja na kupata elimu ya darasani bado wanahitaji kupata elimu ya mtaani ili iwasaidie kukabiliana na hali watakayokumbana nayo wakiwa mtaani.
Fid Q akieleza chanzo cha kupata jina hilo anasema alikuwa na dada mmoja mwenye taaluma inayohusu mambo ya kijamii (sociology) wakaanzisha wazo la mradi.
Wazo hilo la mradi walilipeleka mahali kwa ajili ya kuomba udhamini lakini walielezwa na mtu waliyemfuata kuwa endapo akiwapa Sh 500 wakapata Sh 600, Sh 100 atachukua yeye halafu wao watabaki na Sh 500 kwa ajili ya kuendeshea mradi wao.
Amesema dada huyo hakukubaliana na wazo hilo lakini Fid Q akamweleza ili kuelewa hali hiyo anatakiwa kupata elimu ya KITAAOLOJIA, na huo ukawa ndio mwanzo wa kupata jina la albamu hiyo ambayo haijulikani anaiachia lini.
Je, ataiachia siku yake ya kuzaliwa kama ilivyozoeleka au ataiachia siku gani? Mimi na wewe hatujui. Wakati ni jibu.