DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Yupo mchezaji mmoja wa Tanzania kwa sasa anayenivutia. Bila shaka huwavutia mashabiki wengi wa soka nchini. Mchezaji huyu anaitwa Feisal Salum Abdallah.

Inasemekana kwamba ni bibi yake ndiye aliyeanza kulifupisha jina lake na kumuita ‘Fei Toto’. Hakuna haja ya kujali, kwa kuwa haya ni mapenzi ya wazi kabisa ya bibi kwa mjukuu anayempenda.

Kitu muhimu ninachotaka kusema kwa ufupi kabisa ni kwamba, mwanasoka huyu, Feisal, ananivutia sana.

Fei Toto ni kiungo maridadi kabisa awapo uwanjani. Ana utulivu wa hali ya juu akiwa kwenye eneo lake la kujidai. 

Kwa utafiti wangu ambao si rasmi, Feisal kwa sasa ndiye kiungo bora mzawa; yaani miongoni mwa wachezaji wa Kitanzania, huyu bwana mdogo yupo juu sana kwa sasa.

Hata hivyo, kuna mambo ya kufanya, pia kuna hatua muhimu anapaswa kuipiga Feisal katika maisha yake ya soka, hata kama kwa sasa yupo kwenye kipindi sahihi katika kila kitu chake; kuanzia muda, umri na hata wakati wenyewe.

Miaka michache iliyopita Mbwana Samatta alikuwa na wimbo aliokuwa anapenda sana kuuimba kuhusu wachezaji wa Tanzania kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Sijui kama amechoshwa na wimbo huo ambao ni kama haukuwa ukisikilizwa kwa umakini na wadau. Lakini sasa wimbo huo wa Samatta umehamia kinywani mwa Msuva.

Majuzi baada ya mechi ya mwisho ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia huko Qatar mwakani kati ya Taifa Stars dhidi ya Madagascar, nilimsikia Msuva akiimba wimbo huo alipokuwa akihojiwa na Gift Macha.

Msuva, Mtanzania anayepiga soka la kulipwa nchini Morocco, alizungumza mambo mengi, lakini mwisho akasema njia nyingine ya kuisaidia Stars na Tanzania kwa ujumla ni wachezaji kuondoka nchini kwenda kukipiga ughaibuni.

Mimi ninawaheshimu sana Yanga, haina maana wao hawawezi kumpa Feisal anachokitaka, lakini kwa kusema ukweli Fei Toto anapaswa kuondoka Yanga, kwa kuwa akienda nje ya nchi atapata nafasi ya kuimarisha kiwango chake cha soka zaidi ya ilivyo sasa.

Ni nani anayemkumbuka Simon Msuva wa Yanga? Nimewahi kuandika sana wakati ule. Huyu alikuwa Msuva aliyekuwa anazomewa kila leo! Baadaye akabadilika kidogo. Lakini kitendo cha kwenda nje kimemfanya Msuva awe hatari zaidi.

Siku hizi Msuva ni mmoja wa mastaa muhimu sana wa Tanzania na anategemewa na hata kupendwa na mashabiki wengi kwa sasa.

Yote haya yamefanyika wakati Msuva alipokuwa katika umri, muda na wakati sahihi.

Kama Msuva angekuwa amepishana na vitu hivyo vitatu, sidhani kama muda huu angekuwa bado nje. Kwa hakika angekuwa amesharudi nchini kama ilivyo kwa wengine.

Fei Toto anapaswa kuanza kuitazama kesho yake sasa hivi. Ziko faida nyingi za kucheza nje, japo siku za mwanzo huwa kunakuwapo na ugumu.

Ugumu wa kucheza nje unaanzia katika ‘life style’. Vitu vingi viko tofauti na hapa nyumbani, lakini baadaye ukizoea mazingira inakuwa poa.

Nimesikia mahala fulani mkataba wa Fei Toto ni mrefu. Kwangu si shida. Kwanza Yanga wamefanya jambo jema kumfunga Feisal mkataba mkubwa unaowahakikishia kupata fedha nzuri kama ikitokea ofa nono ya nje.

Kuna sehemu soka letu limekwama. Unaweza kukuta Feisal hana wakala. Kama yupo huenda ni mjomba wake ambaye huwa anaonekana kila mpwa wake akitaka kusaini mkataba mpya na Yanga akiwa na koti lake jeusi katika kochi jeupe pale Salamander.