Serikali imeongeza fedha kwa ajili ya kulipa madeni kutoka Sh9.1 trilioni mwaka 2022/23 hadi Sh10.4 trilioni kwa mwaka 2023/24.

Hayo yamesemwa leo Juni 7, 2023 na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2023/24.

Amesema ili kuwa na taarifa sahihi kuhusu udhibiti wa deni la Serikali, wizara imefanya tathmini ya uhimilivu wa deni hilo kwa miaka 20 ijayo, kuanzia 2022/23 hadi 2041/42.

“Matokeo ya tathmini yanaonesha kuwa, deni la Serikali ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri huyo mwenye dhamana na hazina ya taifa, inaonesha kuwa thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa pato la Taifa ni asilimia 31.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55.