Lissu ni malaika, waziri au mwanasiasa?


Ni takriban wiki tatu sasa tangu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kipate mtikisiko mkubwa, mithili ya pata shika na nguo kuchanika, baada ya Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kuwavua nyadhifa zote viongozi wake watatu.

Viongozi hao ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu (Bara), Zitto Kabwe, Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, na kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.

Viongozi hao wamevuliwa nyadhifa hizo na kikao cha CC kilichofanyika Novemba 20-22, mwaka huu baada ya kukamata na kujadili waraka unaohusu ‘’mkakati wa mabadiliko 2013’’.

Uamuzi huo wa CC ya Chadema umetoa mshindo mkubwa, si kwa wanachama wa Chadema tu, bali hata wanachama, wapenzi na mashabiki wa vyama vingine vya siasa nchini. Chadema imechafuka na inahitaji maji na sabuni kutakatishwa!

CC ya Chadema inadai kuwa waraka huo una lengo la kuhujumu chama na wahusika wamefanya uhaini kwa kuandaa mkakati wa ushindi katika Uchaguzi Mkuu kwa mgombea wamtakaye.

Waandishi wa waraka huo — Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba — wanasema madai hayo si kweli. Wanasema madhumuni ya waraka huo ni kufunga hoja ya kufanya mabadiliko ya uongozi na kuimarisha mikakati ya ushindi kwa mgombea mlengwa katika Uchaguzi Mkuu ndani ya Chadema.

Si nia yangu kuendelea kueleza madhumuni ya waraka na mgogoro uliopo ndani na nje ya Chadema, kwa sababu wahusika wa pande zote mbili wamejieleza kwa umma wa Watanzania. Nao Watanzania wanaendelea kutoa fikra, maoni na rai zao kuhusu suala hilo.

Dhamira yangu ni kutoa maoni na kumsihi Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, kuacha tabia ya kushawishi, kushabikia na kutia vigingi masuala chanya kuwa hasi katika mwenendo wa ustawi wa jamii ya Tanzania.

Katika sakata lililoko Chadema, Lissu amekuwa mstari wa mbele kushawishi umma wa Watanzania uwaone Zitto, Mkumbo na Mwigamba ni wahaini na wahujumu wa chama, jambo ambalo si kweli. Hakuna hujuma wala uhaini. Ni demokrasia tu.

Vyombo vya habari, wananchi hata baadhi ya wanachama na viongozi wenzako katika chama chako wanakusema vibaya kuhusu ushabiki wako. Hiyo si sifa njema kwako. Unajijengea uhasama. Kiongozi kama wewe kuwa na inda na taji si vema. Acha!

Mheshimiwa Tundu Lissu, kwa hadhi zako za kuwa Mwanasheria, Mbunge wa Singida Mashariki, Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Mjumbe wa CC ya chama chako, hustahili hata chembe ya punje ya mtama kutaka kuwaangamiza au kuwasulubu wenzako.

Tabia zako za kupenda kudharau na kukejeli uwezo na hadhi za wanasheria wenzako katika vyombo vya sheria si nzuri. Kadhalika, tabia unayaoifanya bungeni ya kuonesha dharau kwa Bunge na Serikali na kujiona wewe ndiyo bora si nzuri.

Kauli zako zimechangia kuyumbisha Bunge, kudhalilisha Serikali na leo unashika kasuku mkononi kung’oa misumari iliyoshikilia Chadema. Unajua vitendo hivyo vina maanisha nini?

Usiwe kama Majivuno, Waziri wa nchi ya Kusadikika, aliyekuwa imara na tayari kumwangamiza Karama, raia mwema na mtii katika serikali ya ufalme wa nchi hiyo kwa kumfungulia mashtaka ya kuanzisha taaluma ya uanasheria.

Waziri Majivuno alimshtaki Karama na kumpa sifa nyingi mbaya. Alisema, “Raia mmoja anayelindwa na ulinzi wa mfalme, lakini si mwaminifu, anayefaidi haki na maendeleo ya utawala huu, lakini hana shukrani, na aliye chini ya bendera ya nchi hii, lakini si mtii.” (Kitabu cha Kusadikika kilichoandikwa na Shaaban Robert).

Pili, naomba usiwe malaika Israili mtoa roho za watu, ambaye siku ya kiama naye atakufa baada ya kila kiumbehai atakaposikia parapanda litalopulizwa na malaika Israili. Baada ya viumbe vyote kufa, atabaki Israili na Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu atamtaka Israili akalete roho moja iliyobaki. Israeli atakwenda pande nne zote za dunia, hatakuta kitu. Ndipo atakaporudi kwa Mwenyezi Mungu na kusema hakuna roho labda roho yake yeye! Ndipo Mwenyezi Mungu atapotoa roho yake Israeli.

Nakuomba sana, chonde chonde, Tundu Lissu zingatia sana mifano hiyo miwili. Karama alishinda kesi kwa kutoa ushahidi wa ukweli katika baraza na malaika Israili atatolewa roho.